Beki wa Kati wa Simba SC Henock Inonga Baka, amefunguka kuwa, msimu uliopita wa 2022/23 ulikuwa ni mgumu kutokana na klabu yake kushindwa kutimiza malengo kwa kukosa mataji yote ya mashindano waliyoshiriki.
Inonga ameongeza kwamba, msimu ujao wa 2023/24, atapambana kuisaidia timu yake kufikia malengo, huku akiwaomba mashabiki na viongozi kuendelea kumuamini.
“Msimu ulikuwa mgumu lakini ulikuwa mzuri japokuwa hatukufanikiwa kupata kile ambacho tulikitarajia, niwapongeze wachezaji na viongozi kwa kazi na ushirikiano 3 mkubwa ndani ya klabu.
“Ninawaahidi kuwa msimu ujao nitapambana zaidi kuisaidia timu yangu kufikia malengo, nawashukuru mashabiki na viongozi ambao wamekuwa pamoja na mimi kwa nyakati zote kwa sababu nilikuja Simba niliikuta timu inabeba makombe, lakini sasa tumekosa kwa misimu miwili, hivyo tutajitahidi msimu ujao kurudisha furaha kwa mashabiki wetu,” amesema Inonga.
Inonga ambaye alijiunga na Simba msimu wa 2021/22, ameshuhudia kwa misimu miwili aliyokuwa hapo timu yake ikikosa taji la Ligi Kuu Bara, Azam Sports Federation Cup na Ngao ya jamii ambayo yote yamebebwa na Young Africans.