Katika mechi ya jana dhidi ya Namungo, Simba iliwakosa nyota wake kadhaa wa Kikosi cha kwanza, mmojawapo akiwepo injini ya timu kiungo mkata umeme Taddeo Lwanga.
Taddeo anasumbuliwa na maumivu ya goti lakini kwa taarifa za awali zilizotolewa na uongozi wa Simba zilidai sio tatizo kubwa lakini kwa hali ya mambo ilivyo huenda akakaa nje kwa muda mrefu.
Jonas Mkude alipata nafasi ya kuanza baada ya nyota katika eneo hilo kukumbwa na majeruhi, licha ya uongozi kutotaka kuweka bayana hasa ni lini watarudi nyota wa eneo la kiungo.
Kukosekana kwa Lwanga kunazidi kuwanyong'onyesha mashabiki wa Simba ambao bado hawajaridhishwa na namna kikosi hicho kinavyopafomu ndani ya kiwanja.
Daktari wa Simba, Yassin Gembe alipoulizwa kuhusiana na afya za wachezaji hao aligoma kufafanua kwa madai kwamba ameshakabidhi taarifa kwa wakuu wake wa kazi kama taratibu zilivyo.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alipoulizwa alisema ni kweli watawakosa wachezaji hao kwenye baadhi ya micheo yao lakini kukosekana kwao hakutaizuia Simba kushinda.