Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ingekuwaje kama Dabi ya Kariakoo ingeamuliwa na VAR?

Mayele Hatari Simba.jpeg Yanga vs Simba

Wed, 26 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Oktoba 23, 2022 mashabiki wa soka walishuhudia mechi kali, ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ya Watani wa Jadi, Yanga na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Ni mechi ambayo ilivuta hisia kwa mashabiki wa mpira wa miguu, siyo tu Tanzania tu, bali hata kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, Kusini, Kaskazini na Magharibi ya Afrika.

Naweza kusema ni mechi ambayo imesababisha baadhi ya watu kuhairisha shughuli zao za kutafuta riziki kwa muda ili kuweza kuishuhudia, iwe ndani ya Uwanja wa Benjamini Mkapa, kwenye televisheni na hata kusikiliza kupitia redio.

Shamrashamra za mechi hiyo huanzia si chini ya wiki mbili, ndiyo maana Kituo cha Televisheni cha Azam (Azam TV) huanza promo yake mapema katika chaneli mbalimbali za kituo hicho.

Kwa mashabiki wa soka, tambo na ‘vurugu’ huanza ndani ya kipindi cha wiki mbili au zaidi huku kila mmoja akitamba kuwa ataibuka kuwa mshindi.

Mavazi ya rangi ya kijani, njano na nyeusi, nyekundu na nyeupe hutawala mitaani, kwenye vyombo vya usafiri mbalimbali na zaidi ndani na nje ya uwanja na mitaa ya karibu ya uwanja huo.

Siku kadhaa kabla ya mechi hiyo, mashabiki wafurukutwa hujipa shughuli ilisiyo rasmi ya kuulinda uwanja huo usiku na mchana kuogopa masuala ya ushirikina huku wengine wakijipa kazi ya kulinda kambi ambazo timu hizo mbili huweka kujiandaa na mchezo.

Miaka ya nyuma, timu hizo zilikuwa zinaweka kambi za kificho nje ya Jiji la Dar es Salaam, japo siku hizi timu hizo zimeacha tabia ya kuhama Jiji la Bandari Salama.

Wakati Yanga ambao walikuwa wenyeji waliweka kambi yao Avic Town, Simba iliweka kambi yake katika Hoteli ya Crowne Plaza Hotel iliyopo eneo karibu na Mahakama ya Kisutu.

Pia, umuhimu wa mechi hiyo kubwa, husababisha Shirikiso la soka la Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kutopanga ratiba nyingine yamechi zaidi ya hiyo.

Nimeanza na maelezo hayo kwa lengo la kuwapa picha halisi mashabiki wa soka ambao labda hawajawahi kuonja ladha ya mechi ya pilipilika za mechi nje ya uwanja.

Ndani ya uwanja, hali huwa zaidi ya matarajio ya mashabiki wa soka kwani kuna wale ambao wanazimia kutokana na presha ya mchezo huo hasa kwenye suala la matokeo na mwendeno wa mchezo.

Kwa wachezaji, ni mechi ya kujenga jina au kuharibu kwani hisia potofu hutawala mara itapotokea mmoja wao kufanya makosa na kuigharimu timu yake.

Kwa wachezaji ambao ung’ara katika mchezo huo, basi hapo inakuwa faraja kubwa kwao.

Ukiachana na wachezaji, waamuzi huwa katika wakati mgumu zaidi. Naweza kusema kuwa ndiyo ‘chimbo’ la kukimbilia endapo matokeo yanakuwa tofauti kwa timu moja.

Lawama zote huelekezwa kwake na wengine wakitoa ‘historia feki’ kuwa mwamuzi huyo ameipendelea timu moja wapo kwa kuwa ana mapenzi nayo.

MWAMUZI YA MECHI YA YANGA NA SIMBA

Ni wazi kuwa Mwamuzi Ramadhani Kayoko amechezesha mechi hiyo vizuri na kuweza kumudu presha kutoka kwa mashabiki, wachezaji na makocha.

Kayoko amethibitisha kwa nini TFF na TPLB walimchagua kuichezesha mechi hiyo na kutokana na kutokuwa na masihara hata kidogo.

Mwamuzi huyo ‘aliwazawadia’ kadi za njano wachezaji tisa ambapo Yanga ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo, wakionyeshwa kadi wachezaji wanne huku Simba wakionyeshwa wachezaji watano.

Ni wazi kuwa kuna maeneo ambayo Kayoko alifanya maamuzi kwa malengo ya kuufanya mchezo huo kuwa na ushindani zaidi na siyo kuigharimu timu nyingine ipoteze kwa uwezo huo.

Naamini kama TFF na Bodi ya Ligi zingewapa jukumu waamuzi kutoka mabara mengine tofauti na Afrika kuchezesha mechi hiyo, kungekuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao wangeonywa kwa kadi za njano na nyekundu.

Vilevile, ni wazi kuwa kama kungekuwa na matumizi ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (VAR), hali ingekuwa mbaya zaidi kwani kuna matukio ambayo Kayoko ‘aliyachunia’ kwa busara zake pamoja na ukweli kuwa yangeweza kusababisha adhabu na madhara kwa timu husika. Ni wakati sasa, TFF na Bodi ya Ligi kuanza kufikiria matumizi ya VAR kwa mechi ambazo zina mvuto wa aina yake.

Matumizi ya VAR yatawafanya wachezaji wetu kuanza kuizoea teknolojia hiyo ambayo inasambaa kwa kasi pamoja na kuwa na changamoto nyingi ambazo zinaboreshwa kila kukicha.

Japo kuna suala la miundombinu na gharama, lakini kwa sekta ambayo inahitaji maendeleo, gharama haiwezi kuwa kikwazo ukizingatia kazi kubwa iliyofanywa na TFF ya Rais Wallace Karia ya kuleta tija katika soka na kuifanya Ligi Kuu kuwa na uwekezaji mkubwa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati na hata kwa baadhi ya nchi za Kusini, Kaskazini, Magharibi ya Afrika na duniani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live