Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ingekuaje Pacome angekuwa na Ivory Coast AFCON?

Pacome 1 Goal Kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua

Wed, 24 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hivi umeshawahi kujiuliza kiungo wa Yanga na timu ya Taifa ya Ivory Coast, Pacome Zouzoua angekuwepo katika Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) inayoendelea nchini humo ingekuwaje? Kwa bahati mbaya tumeukosa uhondo kwa nyota huyo.

Pacome tayari amejijengea jina katika Ligi Kuu Bara kutokana na vitu anavyovifanya uwanjani, akishirikiana na viungo wenzake kina Maxi Nzengeli na Stephen Aziz Ki ambaye yupo Ivory Coast na chama lake la Burkina Faso.

Nyota huyo ambaye angali anatumikia msimu wake wa kwanza Jangwani, ameshatupia mabao manne katika Ligi Kuu, lakini akiwa ameliteka vizuri dimba inapocheza timu yake kutokana na kucheza vizuri akihaha uwanja mzima.

Ni kweli tumeukosa uhondo wake kwa sababu kwa jinsi kikosi cha Ivory Coast kinavyocheza katika Afcon unaona wazi kabisa kwamba kuna pengo la nyota huyo aliyejiunga na Yanga Julai 19, mwaka jana akitokea Asec Mimosas ya nchini humo kutokana na kiwango chake.

Ivory Coast ambao ni wenyeji wa michuano hiyo ya 34 tangu kuanzishwa kwake 1957, inasikilizia bahati tu ya kusonga mbele baada ya kufanya vibaya katika kundi A' kufuatia kumaliza nafasi ya tatu na pointi tatu kwenye michezo mitatu.

Kikosi hicho kinachonolewa na Mfaransa Jean-Louis Gasset kinasubiri kuona iwapo kitapata nafasi ya timu shindwa yenye uwiano mzuri wa matokeo 'best looser' baada ya leo hatua ya makundi kumalizika kutokana na kushinda mechi moja na kupoteza mbili ikifunga mabao mawili na kuruhusu matano.

Katika kila michuano inapofanyika haikosekani timu inayoweza kushangaza wengi kama ilivyotokea kwenye kundi la Ivory Coast, ambapo Equatorial Guinea ilimaliza kinara na pointi saba sawa na Nigeria iliyomaliza ya pili na pointi saba.

Guinea Bissau ndio timu iliyoburuza mkia katika kundi hilo baada ya kupoteza michezo yake yote mitatu na kuaga michuano hiyo. Hatua hiyo ya wenyeji kusubiria bahati ilijiri baada ya kushangazwa mchezo wa mwisho wa makundi kwa kuchapwa mabao 4-0 na Equatorial Guinea inayoongozwa na mshambuliaji wa timu hiyo anayeongoza mbio za ufungaji, Emilio Nsue mwenye matano.

Miujiza hiyo iliendelea katika kundi 'B' ambapo Ghana ilijikuta ikimaliza ya tatu na pointi mbili nyuma ya Cape Verde iliyoibuka kinara na pointi saba ikifuatiwa na Egypt iliyomaliza na pointi tatu huku Msumbiji ikiburuza mkia na pointi mbili.

Ni wazi timu hiyo inakosa huduma bora ya Pacome kutokana na mchango wake ambao ameuonyesha hadi sasa kwani katika Ligi Kuu Bara tu tayari amefunga jumla ya mabao manne akipitwa sita tu na nyota wenzake, Stephane Aziz KI aliyefunga 10.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ameonyesha pia uwezo mkubwa huku asilimia kubwa ya michezo ya Yanga akiibeba mgongoni mwake kwa sababu amefunga mabao matatu nyuma ya mshambuliaji wa Asec Mimosas, Sankara Karamoko mwenye manne.

Mchango wa nyota huyo ni wazi ungekuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Ivory Coast ingawa haina maana kama angekuwepo ndio ingekuwa silaha ya timu hiyo kufanya vizuri licha ya kuzungukwa na majina makubwa ya wachezaji wanaocheza Ulaya.

Moja ya staa ambaye amekuwa akitegemewa na kikosi hicho ni kiungo, Seko Fofana anayeichezea klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia aliyefunga bao moja tu wakati timu hiyo ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Guinea Bissau.

Pacome mbali na kutenengeza nafasi na kufunga, pia ni mchezaji mnyumbulifu katika eneo la mwisho kwani uwepo wake uwanjani unatoa mianya kwa wengine kutumia faida hiyo kuleta madhara kwa timu pinzani, jambo ambalo linakosekana katika timu ya Ivory Coast.

Kwa mujibu wa mtandao wa FotMob unaotoa takwimu za mechi zinaonyesha Ivory Coast inashika nafasi ya tatu katika timu zilizopoteza nafasi nyingi ikipoteza mara tano sawa na Guinea huku Nigeria ikiongoza kwa kukosa mara 11.

Kuonyesha inakosa mchezaji aina ya Pacome, Ivory Coast inaongoza kugusa mipira mingi ndani ya eneo la timu pinzani kwani imeweza kufanya hivyo mara 110 ikifuatiwa na Misri mara 105 hali inayoonyesha kikosi hicho kinakabiliwa na upungufu katika umaliziaji.

Kama haitoshi ni timu pekee inayoongoza kwa kupata kona nyingi ikiwa nazo 22 ikifuatiwa na Algeria yenye 18 sawa na Misri, ingawa imeshindwa kutumia vyema nafasi hiyo na kujikuta ikifunga mabao mawili na kuruhusu matano.

Umiliki wa mpira haipo nyuma sana kwani inashika nafasi ya pili ikiwa na wastani wa asilimia 64.5 nyuma ya vinara Algeria wenye asilimia 65.2 hali inayoonyesha kocha Jean-Louis Gasset ameshindwa au anakosa machaguo sahihi yanayoweza kukipa matokeo kikosi chake.

Katika eneo la kiungo, Ivory Coast imekuwa ikimtumia Ibrahim Sangare anayecheza Nottingham Forest ya England kuunganisha kikosi ili kusukuma mashambulizi pamoja Fofana ambao wameshindwa kuwa na mwendelezo mzuri baada ya kuanza vyema katika mechi ya kwanza.

Pia nchi hiyo inakosa utulivu katika eneo la ushambuliaji waliloaminiwa kina Nicolas Pepe (Gaziantep), Sebastien Haller (Borussia Dortmund), Karim Konate (Salzburg) na Oumar Diakite wa Reims.

Mashabiki wa Yanga walitamani kumuona Pacome akiiwakilisha nchi yake kama ilivyo kwa Aziz KI, Kennedy Musonda (Zambia), Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad 'Bacca', Dickson Job na Mudathir Yahya waliopo katika kikosi cha timu ya 'Taifa Stars'.

MSIKIE MWAMBUSI Akizungumzia kukosekana kwa Pacome, kocha wa zamani wa Yanga, Juma Mwambusi anasema wachezaji huitwa kuzitumikia timu za taifa kutokana na viwango wanavyoonyesha, hivyo kitendo cha kuachwa kwake hakijamshangaza kwani ni matakwa ya benchi la ufundi.

"Ukiangalia wachezaji wengi wa Ivory Coast wanacheza Ulaya. Kwa hali ya kawaida hata kama ni wewe ukiwa kocha ni wazi utawaangalia wao zaidi kuliko wengine. Pacome ni mchezaji mzuri lakini tuheshimu wale ambao wameitwa pia," anasema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live