Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Indoor ya kwanza, alama aliyoweika Dk Mwinyi

Rais Mwinyi Aitaka Afrika Kutekeleza Mikakati Ya Rasilimali Watu.jpeg Indoor ya kwanza, alama aliyoweika Dk Mwinyi

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Unaambiwa walianza kumuita Mwinyi Mabati, ghafla upepo umegeuka sasa wanamuita Mwinyi Ma-fly over, Mwinyi mabarabara, masoko na majina mengine kama hayo kulingana na namna kazi za maendeleo zinavyoendelea visiwani Zanzibar katika awamu hii ya uongozi wa Seikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dk Hussein Mwinyi.

Nilipoadadisi chimbuko la majina hayo wenyeji wakasema mwanzoni wakati ujenzi wa maeneo mbalimbali unaanza, mengi yalizungushiwa mabati, hivyo wengi waliamini maeneo hayo yataishia kuzungushiwa mabati tu.

“Nyuma hatukuzoea kuona miradi mingi inafanyika kwa wakati mmoja. Masoko ya kisasa yanajengwa, barabara katika maeneo mengi zinajengwa, viwanja vya michezo na flyover, vyote vinafanyika kwa wakati mmoja katika kipindi kifupi,” anasema mmoja wa wakazi wa Jang’ombe, Ally Idrisa Salum..

“Ni miaka mitatu tu, lakini vitu vikubwa vimefanyika. Wengi hatukutarajia katika miaka mitatu tena ya mwanzo miradi mingi ifanyike. Hatukuzoea hivyo tulitegemea kuyaona haya mwishoni kabisa mwa kipindi chake au muhula wake wa pili, lakini imekuwa ni tofauti tunaona hivi sasa miradi mingi inafanyika kwa wakati mmoja”

Kwenye michezo, Rais huyo wa nane wa Zanzibar, Dk Mwinyi ameweka alama nyingine ambayo itabaki katika kumbukumbu kwa Wazanzibari kwa kuwa kiongozi wa kwanza wa visiwa hivyo kujenga uwanja wa ndani (Indoor) visiwani humo.

“Haijawahi kutokea. Nakumbuka wakati bado nacheza kikapu mwaka 1996 kulikuwa na fununu kwamba kuna Indoor (Uwanja wa Ndani) itajengwa. Lakini hadi nastaafu kucheza haikuwa imejengwa,” anasema katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Said Marine.

Anasema katika kipindi cha miaka mitatu ya Dk Mwinyi madarakani fursa nyingi na maendeleo makubwa yamepatikana kwa kuzingatia dira ya michezo visiwani humo.

“Dira yetu inasema ifikapo 2030 Zanzibar iwe kitovu cha maendeleo ya michezo kikanda na kitaifa. Hiyo ndiyo inatuongoza kwa kuhakikisha kwanza tunakuwa na miundombinu iliyo bora, pia kuwa na wachezaji bora na vyama vyenye uongozi bora, mathubuti na vyenye hali nzuri.

Anasema katika miaka mitatu ya Dk Mwinyi eneo la miundombinu ya michezo mafanikio yameonekana kuanzia kwenye uwanja wa kimataifa wa Amaan unaofanyiwa maboresho kwa sasa.

“Ukarabati huu sio kwenye soka tu, tumetengeza kapeti ya kukimbilia (tartan) kwa kiwango cha kimataifa, hivyo kwenye riadha pia kuna fursa ya kuwa wenyeji wa mashindano ya kimataifa,” anasema.

INDOOR YA KWANZA

Katika siku 1,095 alizokaa madarakani, Dk Mwinyi ameweka alama ya kuwa Rais wa kwanza kujenga Uwanja wa Ndani wa Michezo (Indoor).

“Awali tulikuwa na uwanja wa judo na sanaa za mapigano ambao huo nao ulikuwa mdogo sasa umeongezwa na kuboreshwa kuwa wa kisasa,’ anasema Marine.

Anasema ukiachana na uwanja huo wa judo na sanaa za mapigano, Zanzibar haikuwahi kuwa na uwanja wa ndani kwa ajili ya michezo mingine kipindi chote.

“Katika kipindi cha Rais Mwinyi ndipo uwanja huu unajengwa kama nilivyosema awali miaka 27 iliyopita ndipo kulikuwa na fununu za uwanja wa ndani kujengwa, lakini haikuwa hivyo hadi nimestaafu kucheza kikapu na sasa ni kiongozi. Rais Mwinyi amelifanikisha hili katika kipindi cha miaka mitatu tu madarakani,” anasema kiongozi huyo mwandamizi wa michezo visiwani hapa.€

UWANJA HUO UKO HIVI

Marine anasema kwa kuanzia kutakuwa na viwanja vya netiboli, kikapu, mpira wa wavu (volleyball), mpira wa mikono (handball), tenisi na vinyonya na kwenye hafla ya sherehe za Mapinduzi uwanja huo utaanza kutumika.

“Uwanja wetu wa ndani utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 1200 waliokaa kwenye viti. Utakuwa na mghahawa na vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji,”€ anasema na kuongeza:

“Kwa mara ya kwanza Zanzibar tunakuwa na Indoor Zanzibar. Ndoto ya kujenga uwanja huu imesubiriwa muda mrefu lakini imewezekana katika miaka mitatu ya Dk mwinyi.

Uwanja huo umejengwa ndani ya Uwanja wa Amaan, ambao umeunganishwa katika mradi wa ukarabati wa uwanja huo.

“Kulikuwa na changamoto (upande wa) michezo hii ya ndani, nyakati za mvua ilisimama kuchezwa na haikuwa na uwanja wake maalumu, lakini sasa imekwisha.

“Uwanja huu ni project (mradi) moja ya ukarabati wa Uwanja wa Amaan ambao umegharimu bilioni 52, ndani yake pia kuna gym, ofisi na mghahawa.”

VIWANJA VINGINE HIVI HAPA

Mbali na uwanja wa ndani na ule wa judo na sanaa za mapigano, mtendaji huyo wa BTMZ anasema katika ukarabati wa Uwanja wa Amaan, pia kuna viwanja vingine viwili vya mazoezi vinajengwa.

“Hivi vitatumika kwa ajili ya mazoezi wakati wa Afcon (Fainali za Mataifa ya Afrika 2027 ambapo Tanzania, Kenya na Uganda ndiyo wenyeji. Kwa Tanzania Uwanja wa Amaan ni miongoni mwa vitatu vitakavyotumika).

“Mbali na Afcon, pia viwanja hivi vitakuwa vinatumika kwenye mashindano yetu mengine ya mikoa, hata baadhi ya mechi za ligi zitachezwa hapo,” anasema.

“Viwanja hivyo vinawekewa majukwaa yenye uwezo wa kuchukua mashabiki takriban 500 waliokaa kila kimoja. Pia vitakuwa na vyumba vya kubadilishia nguo kwa wachezaji.

“Kile kilio cha muda mrefu kwa wanamichezo wa Zanzibar kwa Serikali yao kupata facilities (miundombinu) kama hii kimesikika. Kabla ya kuwepo kwa Uwanjawa Ndani ilikuwa ni tabu kwa michezo mingine kuchezeka hata mashindano ya kimataifa ilikuwa ni shida kuandaa.

“Tunafahamu michezo inahitaji pesa. Kwa kuanzia kama Serikali tumeanza kwa miundombinu ambayo uwekezaji wake ni mkubwa. Baada ya miundo mbinu tutaelekeza nguvu kwenye michezo yenyewe.”

Marine anasema hadi ifikapo Desemba, mwaka huu ujenzi wa uwanja huo utakuwa umekamilika na mashindano ya Mapinduzi Cup yatachezwa hapo katika kuadhimisha sherehe ya miaka 60 ya Mapinduzi.

“Uimarishwaji wa Uwanja wa Gombani, Pemba napo kunafanyiwa marekebisho. Pia kuna mradi wa ujenzi wa viwanja vya wilaya ambako kutajengwa kiwanja kimoja kila wilaya na baadhi ya wilaya viwanja viwili. Hii ni kwenye soka na michezo mingine.

“Kwenye michezo mingine kutakuwa na uwanja wa 4 in 1 ambako patachezwa kikapu, mpira wa mikono (handball), wavu na netiboli katika kila wilaya ambavyo vitawezesha wananchi kila wilaya kushiriki kwa kiwango bora michezo hiyo,”€anasema.

Mtendaji huyo anasema kuna mradi pia wa GIZ, Shirika toka Ujerumani ambalo linafadhili mradi mwingine wa kujenga uwanja wa 6 in 1.

“Haya yote yamefanyika ndani ya miaka mitatu ya Dk Mwinyi. Huu mradi utajenga viwanja vinne Pemba na vinne Unguja. Kwenye miundombinu ya michezo, Rais amewawekea Wazanzibar mazingira rafiki tena ndani ya kipindi kifupi,” anasema.

UWANJA MKUBWA ZAIDI

Ukiachana na Uwanja wa Amaan ambao ni wa asili wa Zanzibar wenye uwezo wa kubeba mashabiki 15,000, Serikali ina mkakati wa kujenga uwanja mwingine mkubwa utakaochukua mashabiki 40,000.

Marine anasema mchakato wake bado kwani kunaangaliwa eneo utakapojengwa uwanja huo na mipango mingine.

“Huu bado ni mpango wa ndani. Tunafahamu Serikali yetu haitaishia hapa katika masuala ya miundombinu,” anasema kwa kifupi mtendaji huyo bila kufafanua zaidi ujenzi wa uwanja huo mkubwa zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti