Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Inawezekana Barbara ni tatizo kweli pale Simba

Barbara Gonzalez CEO.jpeg Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez

Mon, 12 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Nimeona kelele nyingi mitandaoni kuhusu Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez. Inasemekana amekuwa shida pale Simba. Inasemekana.

Nimeona baadhi ya watu wakisema kuwa Barbara amekuwa akikwamisha baadhi ya vitu pale Simba. Tena wanaosema, wanaongea kwa kujiamini kweli.

Ni ngumu sana kuamini hivyo. Unajua kwanini? Subiri nitakueleza. Simba kama zilivyo taasisi nyingine kubwa ina changamoto zake nyingi. Ni kweli. Hakuna taasisi kubwa inayokosa changamoto.

Lakini hili la watu kujitokeza hadharani na kusema mtendaji mkuu ndiye chanzo cha matatizo makubwa pale Simba limenishtua zaidi. Mtendaji mkuu ndiye roho ya taasisi yoyote. Mipango yote huanzia na kumalizikia katika ofisi yake. Ila katika soka hii ni ofisi nyeti zaidi.

Unajua kwanini? Ni kwa sababu soka lina njia zake. Soka lina mipango na uendeshaji wa aina yake. Kuna fitina kubwa sana katika soka. Na kuna watu wa soka. Sasa ukisikia kuwa mtendaji mkuu amekuwa tatizo hadi watu wa mpira wanakaa pembeni, basi ni tatizo kubwa. Hiki ndicho kinaelezwa pale Simba. Inasemekana baadhi ya watu wamejiweka pembeni kwa sababu ya mtendaji wao.

Msimu uliopita tatizo hili lilizungumzwa chini chini. Baadaye baadhi ya wajumbe wa bodi kama Kassim Dewji walijitokeza hadharani na kumlalamikia wazi mtendaji mkuu kuwa anataka kufanya kila kitu peke yake.

Ni wachache kama Kassim wenye ujasiri wa kujitokeza hadharani na kusema haya. Ila yawezekana msimu uliopita maji yalimfika shingoni akaamua kusema ukweli hadharani.

Huyu ni mtu mkubwa ndani ya Simba. Amefanya makubwa Simba na soka la Tanzania analifahamu kwelikweli. Simba itakwendaje kama watu kama yeye hawashirikishwi? Inafikirisha sana. Ukisikia mtendaji mkuu Simba amekuwa tatizo unashtuka kwa sababu kubwa mbili.

Kwanza, huyu ni mtu wa karibu sana wa mwekezaji Mohamed Dewji. Ndiye aliyebeba maono ya biashara yote ya mpira Simba. Inawezekana anatenda kwa kufikiria zaidi maslahi ya mwekezaji kuliko ya Wanasimba wenyewe.

Hili ni tatizo kubwa kwasababu Simba ni ya watu. Wenye Simba yao wanataka zaidi furaha ya uwanjani kuliko hayo mambo mengine. Ndio maana wanaweza kupishana maono na wenzake.

Pili, katika picha ya nje, Simba imemtengeneza Barbara kuonekana kama mtu mahiri katika taasisi yao. Maendeleo makubwa yanayofanywa na Simba yanaonekana ni utendaji mahiri wa Barbara. Ni kwanini wameamua kufanya hivyo kama Barbara ni tatizo? Inafikirisha. Pengine wakati wanamtengeneza kuwa hivyo hawakuwaza madhara ya baadaye. Mtu akipewa sifa kubwa sana kuna sehemu lazima atawasumbua. Ila tukirejea katika mafanikio ya Simba ndani ya uwanja tangu Barbara ameingia ni wazi kuwa kuna tatizo mahala.

Katika msimu wake wa kwanza Simba ilibeba makombe yote ya ndani na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Yawezekana ilikuwa ni misingi imara aliyoacha mtangulizi wake, Senzo Mbatha. Inawezekana Senzo alijenga msingi wa mafanikio haya ndiyo sababu ikawa kazi rahisi kwa Barbara katika msimu wake wa kwanza.

Nini kimetokea msimu uliopita? Simba ilipoteza kila taji ililotwaa. Ndio msimu ambao watu walianza kumnyooshea vidole mtendaji mkuu.

Simba ikaondoshwa katika Ligi ya Mabingwa tena nyumbani. Angalau ikajipoza kwa kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Lakini kwa hapa ndani hakukuwa na maajabu sana.

M-simu huu mambo yameonekana kuwa magumu zaidi. Simba ikaanza kwa kupoteza Ngao ya Jamii. Kwenye ligi mpaka sasa ipo nafasi ya tatu na uwezekano wa kutwaa ubingwa ni mdogo.

Kwanini? Ni kwa sababu kuna shida ndani ya taasisi. Kuna shida katika maeneo nyeti. Nitazungumzia baadhi.

Kwanza, msimu uliopita Simba iliuza wachezaji wake wawili mahiri, Luis Miquisone na Clatous Chama. Ni kweli ilivuta mpunga mrefu, ila ndani ya uwanja ikabaki ovyo. Ikafeli zaidi katika usajili wa wachezaji. Haikununua wachezaji mahiri kama ilivyotarajiwa. Ni tatizo la nani? Hapa ofisi ya mtendaji mkuu inawajibika.

Pengine hawakuwa wepesi kusaka wachezaji na kukamilisha dili zao haraka. Mwisho wa siku wakanunua wachezaji wengi wenye uwezo wa kawaida.

Tatizo kubwa likaonekana zaidi katika usajili wa msimu huu. Wachezaji wengi mahiri iliowataka Simba hawakuweza kujiunga na timu hiyo.

Victorien Adebayor ndiye alikuwa wa kwanza kutajwa pale Simba. Hata hivyo dili lake likaenda kwa kasi ya kinyonga na akajiunga na RS Berkane ya Morocco.

Vipi kuhusu Stephane Aziz Ki? Simba ilitajwa kuwa ya kwanza kumhitaji. Kila kitu kilionekana kuwa vizuri mwanzoni, ila cha kushangaza akatua Yanga. Ilikuwa ni pigo kubwa. Ikaonekana kuwa Simba itaachana na Chris Mugalu na Meddie Kagere. Ikaonekana wazi kuwa anahitajika straika mahiri wa kuziba nafasi yao.

Akatajwa Cezar Manzoki. Habari zake zikaandikwa sana. Ikaelezwa kuwa Simba wamemalizana naye. Lakini nini kilitokea? Dili likafeli na Vipers wakamuuza China dakika za mwisho. Inasikitisha sana.

Eneo la pili ambalo limekuwa na shida ni katika makocha. Ghafla Simba ikaachana na Didier Gomes kwa madai kuwa ameshindwa kufikia malengo. Alikuwa amedumu klabuni hapo kwa miezi tisa tu.

Ikamleta kocha Pablo Franco. Mwalimu asiyekuwa na uzoefu na soka la Afrika. Akaja kujifunza Simba na matokeo yake akashindwa kuwapa chochote kikubwa.

Nini kimetokea baada ya hapo? Akaja Zoran Maki ambaye hakutimiza hata miezi miwili kazini. Akatimka zake baada ya kushindwa kuelewana katika baadhi ya mambo. Simba ikalazimika kumchukua mzawa Juma Mgunda kama mbadala wa muda mfupi. Hadi sasa haieleweki kama Mgunda atasalia hadi mwisho wa msimu ama la.

Hivyo kwa ufupi katika utendaji Simba kuna vitu vinapwaya. Inawezekana mtendaji wa sasa anataka kufanya kila kitu peke yake, lakini hana uzoefu wa kutosha katika eneo hilo.

Hili lipo wazi. Barbara hana uzoefu katika soka. Kazi yake kubwa ya soka ameanzia Simba. Ana mengi ya kujifunza kwa wazoefu waliopo pale. Ila kama wazoefu wenyewe wanamuona kama ni tatizo, basi Simba ina safari ndefu.

Chanzo: Mwanaspoti