Unaweza ukaona unavumilia kumbe unapoteza muda na unaweza ukaona unapoteza muda kumbe ndio unafanikiwa, hili ndio jambo lililowakuta baadhi ya wachezaji mbali mbali wa soka Duniani.
Baadhi yao walizihama timu walizokuwa wanachezea kwa ajili ya kutafuta nafasi sehemu nyingine lakini mambo yakawa magumu.
Mmoja ya wachezaji hawa ni Paul Pogba ambaye tangu atue pale Juventus akitokea Man United amekuwa na nyakati ngumu sana akicheza mechi mbili tu.
Leo tunawaangalia mastaa watano ambao waliondoka Man United na wakaenda kukutana na nyakati ngumu kwenye timu walizojiunga nazo.
5. EDINSON CAVANI
Kama ilivyokuwa kwa Pogba, huyu pia aliondoka Man United akiwa huru baada ya mkataba wake kumalizika na alienda kujiunga na Valencia.
Lakini tangu atue hapo amekuwa kwenye wakati mgumu kwani amekumbwa sana na majeraha yaliyosababisha acheze mechi 18 tu za michuano yote.
Licha yakuwa mchezaji tegemeo ameshindwa kuisaidia timu hiyo ambayo hadi wakati huu inapambana kukwepa janga la kushuka daraja.
4. JESSES LINGARD
Kabla ya kujiunga na Nottingham Forest kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, misimu miwili iliyopita akiwa na Man United alicheza mechi 16 tu za michuano yote.
Alijiunga na Nottingham akiwa na matumaini makubwa ya kurudisha makali yake lakini mambo yameenda ndivyo sivyo hadi sasa licha yakuwa mmoja kati ya mastaa wanaolipwa zaidi kwenye kikosi hicho.
Amcheza mechi 19 na kufunga mabao mawili tu, huku mkataba wake ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na Nottingham haionyeshi nia ya kumuongeza.
3. JAMES GARNER
Alikuwa anaonekana kama mmoja kati ya vijana wanaoweza kuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Manchester United.
Lakini katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi alijiunga na Everton ili kupata nafasi ya kucheza kwenye Ligi Kuu England lakini mpango wake huo umefeli kwani amecheza mechi saba tu hadi sasa na amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha ya mara kwa mara na mbali ya kupona kwenye mechi tatu za mwisho alianzia benchi.
Katika mazungumzo yake akielezea sababu kuondoka Man United Garner aliliambia gazeti la The Times "Nilikuwa sijikii vizuri kwa kukosa nafasi kwenye timu ambayo nilikuwa nafanya nayo mazoezi kila siku, niliondoka kwa sababu sikuwa nahitaji kuendelea kuwa hapo"
2. DANIEL JAMES
Baada ya usajili wa Cristiano Ronaldo, James aliamua kuondoka na kujiunga na Leeds United kwenye dili la Paun 25 milioni na licha ya kupewa nafasi ya kuendelea kusalia kwenye kikosi cha mashetani hao wekundu na kuendelea kupambania nafasi staa huyu aligoma.
Msimu wake wa kwanza akiwa na Leeds, lakini dirisha lililopita la majira ya kiangazi alijiunga na Fulham kwa mkopo kwenye dili lililoshangaza watu wengi na tangu ametua kwenye timu hiyo amecheza mechi saba tu ambazo ametumia dakika saba tu.
1. PAUL POGBA
Baada ya mkataba wake wa miaka sita kumalizika, Pogba mwenye umri wa miaka 30, aliondoka kwenye kikosi cha Manchester United na kwenye mahojiano yake aliwaambia kwamba watajuta.
Lakini tangu atue kwenye Juventus amecheza mechi mbili tu za Ligi Kuu England na muda mwingi amekuwa akiutumia nje ya uwanja kuuguza majeraha.
Majeraha hayo yakasababisha asipate hata nafasi ya kuichezea Ufaransa kwenye Kombe la Dunia na hivi karibuni kulikuwa na taarifa kwamba Juve inafikiria kuvunja mkataba wake ingawa wenyewe walikanusha.