Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Inasikitisha, Nyota Simba Queens anyimwa nauli Morocco

Mwanahamis Pic Inasikitisha, Nyota Simba Queens anyimwa nauli Morocco

Fri, 10 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna somo kubwa kwa wazazi kufuatilia vipaji vya watoto wao, ambavyo vinaweza kuamua hatma ya maisha yao, badala ya kuwalazimisha kufanya vitu vilivyo nje ya uwezo wao.

Kuna funzo analotoa straika wa Simba, Mwanahamisi Omary, anayesema haikuwa rahisi kwenye familia yake kumruhusu kucheza soka, aliamua kujitosa kupigania anachokiamini na sasa kageuka msaada kwa familia yake.

Anasimulia wakati anafanya mahojiano na Mwanaspoti kwamba 'Nimetoka familia ya dini sana (Uislamu), nakumbuka nikiwa mtoto nilikuwa napenda sana kujichanganya na kucheza mpira wa miguu na wanaume;

Anaendelea kuelezea 'Mama alikuwa ananichapa sana akinikuta nacheza soka, nikaamua kutoroka kuja Dar es Salaam, hata kwa ndugu yangu nilikofikia haikuwa rahisi, kifupi Mwanahamisi wanayemuona leo, kapitia mengi ila hakukata tamaa kutetea ndoto yake.'

KAJENGA KWAO

Anasema kidogo alichokuwa anakipata kwenye karia yake, akaamua kumjengea nyumba mama yake mzazi akisaidia na mdogo wake, jambo analosisitiza wazazi wasiwazue watoto wao kuonyesha vipaji vyao.

'Familia yangu inajivunia mimi, niliamua kupambana na kuonyesha kwamba sijachagua soka kwa bahati mbaya, nashukuru Mungu kidogo ninachokipata nahakikisha namsaidia mama yangu kuishi vizuri,' anasema.

Pia anajenga nyumba yake, anayosema inaweza ikakamilika ndani ya miaka miwili, huku akiwatia moyo mabinti wanaotamani kucheza, kujiandaa kwa uvumilivu na wajue kazi hiyo ni ajira.

"Kwa sasa soka limeanza kulipa, tofauti na miaka 10 nyuma ambayo tulisota sana, hivyo wanaopenda na kutamani kufikia hatua yangu wapambane watafanikiwa.' anasema.

NJE ILIKUAJE

Nchini Morocco ambako Mwanahamisi alikwenda kucheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Chabab Atlas ambayo alisaini miaka minne, anakiri wapo mbali kwa miundombinu na wana misingi thabiti ya kufanya soka lao liwe juu.

'Nimegundua kwa nini timu zao za taifa zinafanya vizuri, wanapoibuka mastaa ujue huku nyuma wanatengeneza wengine wapya, hivyo hawaachi pengo la mastaa waliozoeleka wanapostafu, mbadala wao wanakuwa wameandaliwa;

'Tofauti na hapa nyumbani ambapo baadhi ya majina yamedumu kwa muda mrefu kwa sababu wanaokuja nyuma hawaonyeshi muendelezo wa viwango vyao, ingawa TFF inapambana kulifanya soka letu liwe juu ndio maana kuna wageni wengi, hilo liwafanye wazawa wachangamkie fursa hiyo'.

Anasema sababu ya kurejea kucheza ligi ya nyumbani, hiyo timu haikumlipa pesa yake ya usajili, hivyo hakuona sababu ya kuendelea kucheza kama fasheni. Anasema baada ya timu yake ya kwanza kutomlipa pesa zake za usajili, akapata dili la klabu nyingine ya Chabab Mohammedia ambapo hakujua nini kipo nyuma ya pazia.

'Kumbe Chabab Mohammedia imamalizana kimyakimya na Chabab Atlas mimi bila kujua timu za Kiarabu zinapeana wachezaji bila shida ila ngumu kumruhusu kuvunja mkataba ama kwenda nje yao;

'Chabab Mohammedia nayo haikunipa pesa ya usajili na wakati nadai nilikuwa nazungushwa huku na kule, nikawaomba wanipe nauli nirudi nyumbani kusalimia wakakataa, nikarejea Tanzania kwa pesa zangu mwenyewe, ila nilijua tu wakianza msimu mpya lazima watanitafuta kwa kiwango nilichokionyesha.

'Maana nilicheza nusu msimu tu, sasa wakati unakaribia kuanza msimu mpya viongozi wakatuma tiketi, nikawaambia kama hawataingiza pesa zangu kwenye akaunti sirudi, wakasema niende nikaongee na rais wa timu wakatuma tiketi ya pili, nikakataa.

'Kiukweli nilikuwa kwenye wakati mgumu sana, nikaamua kukaa kimya ili nisichanganywe na kelele za wanaodhani nimerejea nyumbani kwa kufeli, nikafuatwa na Yanga Princess ila kwa sababu Simba Queens pia ilinihitaji nikaipa nafasi na kuwaeleza viongozi ukweli wa mkataba, wakafanya bidii kuuvunja na sasa nacheza kwa uhuru'.

Anasema amejifunza kitu kipitia hilo na anamtaja Simon Msuva kwamba alimtia moyo kwamba atavuka na asiogope kurejea nyumbani kujipanga upya. 'Kitu kikubwa mchezaji awe na wasimamzi sahihi ndipo anapoweza kufaidi matunda ya kipaji chake, vinginevyo nje sio rahisi kwa namna mikataba yao ilivyo' anasema.

CHIPUKIZI

Anatamani kuona chipukizi wanaokuja nyuma yake, wanapopata nafasi ya kujulikana wasijisahau na kuvimba wakiona wamemaliza kila kitu, jambo linalowatoa kwenye ushindani.

'Majina ya kina Mwanahamisi, Mwalala, Mwasikili, Chaburuma na wengineo wengi yapo kwa muda mrefu, sasa wanaokuja nyuma yetu wakaze msuli ili na wao wajenge yao, lakini hayawezi kujengeka kama hawatazingatia nidhamu ya kazi;

'Hilo siyo tu kwa soka la wanawake, hata wanaume kuna kizazi kilikuja moto na kingekuwa faida kubwa kwa Stars, ajabu kikalewa sifa kimepotea, majina yamebakia yale yale ya kaka zao, hali hiyo inanisikitisha sana.

'Wachezaji tunapoingia kwenye soka siyo maonyesho ama kuivimbia jamii inayotusapoti, badala yake ni kazi tunayopaswa kuifanye kwa nidhamu ya juu, ndipo maendeleo ya soka yatakapopatikana.'

SOKA LA TANZANIA

Analishukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa namna linavyopambana kuinua soka la wanawake, kwamba lina hatua na ushindani kimataifa.

'Sio kazi ndogo na sisi kuanza kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, kilichobakia ni sisi wenyewe kujitoa na kuonyesha tunastahili kwenye michuano hiyo, Simba Queens ilifungua njia kushiriki kwa mara ya kwanza;

'Naamini msimu huu tunachukua tena ubingwa, ingawa sio kazi ndogo tunahitaji kupambana, ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Caf.'

AJIBU

Anasema anakiheshimu sana kipaji cha Ibrahim Ajibu na bado anamuona ana nafasi ya kufanya makubwa endapo tu akiamua kubadili upepo wa namna jamii inavyomchukulia.

'Nimejifunza mengi baada ya kutoka nje, huko wanathamini sana wachezaji wao, wakijua watawatumia kwenye timu zao za taifa, kipaji kama cha Ajibu ni muhimu sana kwa Stars, ingawa siwezi kusema mengi sijui kitu gani kinaendelea kwake.' anasema.

Anasema kuna wakati mwingine akiangalia kwenye Ligi Kuu anaona wapo mastaa wa kigeni ambao wamezidiwa kipaji na Ajibu, isipokuwa kinachowabeba ni muendelezo wa uwezo wao.

'Nasisitiza tena kwa umri wake, anaweza akaamua kufanya makubwa na akaja akastafu soka kwa heshima kubwa, kuliko aliyonayo kwa sasa' anasema.

Chanzo: Mwanaspoti