Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Imani za ushirikina klabu zibadilike

Ushirikina Vilabu Imani za ushirikina klabu zibadilike

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh1 milioni na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) kwa makosa ya kulazimisha kupitia mlango usio rasmi katika mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya huku pia beki wa kushoto wa timu hiyo, Gadiel Michael akitakiwa kulipa faini ya Sh500,000 katika matukio mawili yanayohusishwa na imani za kishirikina.

Gadiel ambaye hana namba ya kudumu kikosini kutokana na eneo lake kuhodhiwa na nahodha msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, ametuhumiwa kuingia kwenye uwanja huo mapema kabla ya mechi na kwenda kumwaga vitu vyenye muonekano wa unga katikati ya uwanja.

Matukio haya yamekuja siku kadhaa baada ya mastaa wa kimataifa wa Simba na Yanga Clatous Chama (Mzambia) na Stephane Aziz Ki, raia wa Burkina Faso, kufungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh.500,00 kila mmoja kwa kutoshiriki tukio la kupeana mikono na wachezaji wenzao kabla ya kuanza kwa mechi ya Ligi Kuu kati ya timu hizo mbili kubwa zaidi nchini na zenye upinzani wa jadi.

Tukio hilo pia lilikuja sio muda mrefu sana tangu Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuitoza faini ya dola 10,000 klabu ya Simba kutokana na tukio la uwanjani nchini Afrika Kusini ambako wachezaji walionekana wakiwasha moto ndani ya dimba la kuchezea kabla ya kuanza kwa mechi yao ya marudiano ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates.

Adhabu hiyo imehusishwa na imani za ushirikina ikiaminika kwamba Simba ilikuwa inawaroga Pirates ili iwatoe, lakini bado waliotolewa ni Simba.

Iwe Simba ilikuwa ikiroga bila ya aibu mbele ya kamera za televisheni zilizokuwa zikirusha ‘live’ mechi hiyo Afrika nzima na pengine duniani kote, au ilikuwa ikiwafanyia Orlando rusha roho au ‘mind game’ tu kuwatoa mchezoni, Mwanaspoti tunasema ushirikina ama vitendo vinavyoashiria ushirikina haviwezi kutusaidia katika maendeleo ya mchezo huu.

Matukio haya ya hivi karibuni ni sehemu tu ya matukio mengi tuliyoyazoea yanayofanywa na klabu karibu zote nchini na ndio maana kila zinapotangazwa adhabu na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Ligi imekuwa ni kawaida kukuta timu za Ligi Kuu zikiadhibiwa kwa makosa ya vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina.

Jambo linalosikitisha ni kwamba klabu kubwa, ambazo zinatumia pesa nyingi katika kusajili wachezaji wenye vipaji, zinafundishwa na makocha wa kizungu, zinalipa mishahara mikubwa na kutoa posho nono zinapopata ushindi, unakuta ndizo zinazoongoza kwa kuadhibiwa kutokana na vitendo vinavyoashiria ushirikina.

Hakika hili ni jambo linalosikitisha sana hasa katika soka la kisasa, ambalo vipaji, mbinu za walimu, motisha kwa wachezaji na maandalizi bora ndio huamua mechi.

Imani potofu kwamba kuna nguvu za giza zinazoweza kuamua mechi ni vitu ambavyo kila klabu, na kila mtu anapaswa kujiuliza upya.

Kama kwa kutumia nguvu za giza unaweza kupata matokeo katika mechi, kwanini klabu zinaingia gharama kubwa za kusaka wachezaji wenye vipaji kwa pesa nyingi? Kwanini zinaajiri makocha wa kigeni? Kwanini zinaweka kambi za gharama zikiwamo za nje ya nchi? Kwanini basi wasiepuke gharama hizi kwa kusajili wachezaji wa mchangani tu na kisha kumlipa pesa kidogo mganga? Amkeni.

Chanzo: Mwanaspoti