Vigogo vya soka nchini Simba na Yanga vinazidi kuchanja mbuga katika ukanda wa Afrika kutokana na uwakilishi mzuri kwenye michuano ya kimataifa tofauti na zamani.
Simba na Yanga zimebarikiwa kuwa na mashabiki wengi ambao wanazipenda timu hizo na kujaza viwanja zikiwa katika majukumu yao.
Wingi wao viwanjani umeonekana hasa katika Uwanja wa Benjamini Mkapa unaochukua watu 60,000 timu hizo zimeweza kuujaza hasa zinapokutana au katika matamasha Simba Day na Wiki ya Wananchi.
Jicho la Mwanaspoti limebaini baadhi ya mashabiki ambao hawakosi timu hizo ziwapo katika majukumu yao iwe Ligi Kuu, FA, mechi za kimataifa na hata Mapinduzi hawakosekani majukwaani.
Ligi Kuu inachezwa katika mikoa mbalimbali ndani ya wiki na hata wikiendi hawawezi kukosekana licha ya kuwa na majukumu yao ya kujiingizia vipato katika siku hizo.
Hawa ni baadhi ya mashabiki ambao huwaambii kitu timu zao zikiwa katika majukumu yao wengine wakidai 'wamechanjiwa' kuzipenda timu hizi na kamwe hawawezi kuziaacha.
JUSTINE JOEL
Kutokana na mahaba yake kwa Simba, Joel anasema hata akifariki ashamwambia mkewe jeneza lake lifunikwe na bendera ya Simba kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya nyumbani kwao.
"Simba kwanza mengine baadaye yaani ikicheza hata Simba Queens mimi sikosi najipangia muda wangu usiingiliane na kazi maana mke wangu ni Yanga anajua kabisa Simba ikiwa sehemu siwezi kukosa hata kama naumwa naenda hivyo hivyo," "Niliwahi kutoa drip mimi ili nitoke hospitali nikamuone Mnyama nyie mimi Simba imechukua maisha yangu sana, naumwa kwa ajili ya Simba,"anasema.
DAUDI SIMBA
Daudi Simba unaweza kudhani ni jina la utani kumbe baba yake anaitwa Simba, anasema kutokana na mahaba aliyonayo kwa wekundu hao wa msimbazi anatumia pesa zake kwenda popote inapoenda timu hiyo.
"Mimi ni Simba damu hata jina langu ni Simba, nafanya shuguli binafsi ratiba inapotoka najipanga kulingana na muda najua kabisa siku fulani timu yangu inacheza wapi, nisipoenda labda niwe mgonjwa maana Simba ndio burudani yangu mimi," anasema Daudi.
Anasema anapanga bajeti yake anaweza kukaa siku tatu kama ambavyo alivyokaa Tanga katika Ngao ya Jamii na gharama ni zake hapati sapoti ya mtu yeyote kwa kuwa amejiajiri na hiyo ni furaha yake.
AGGY DANIEL (MISS SIMBA)
Miaka ya nyuma wanawake walikuwa mbali na mpira wa miguu lakini hivi karibuni imekuwa tofauti kwani wamekuwa wakijitosa kama wanaume wanavyofanya.
Mwanadada huyu anasema anapanga ratiba yake vizuri isiweze kuharibu majukumu yake ya kujiingizia kipato kwa kuwa maisha lazima yaendelee na anaingia gharama kubwa kuifuata Simba inapoenda.
Anasema ana mchango mkubwa kwa timu yake: “Kwanza kuisapoti timu yangu na kuitangaza ni mchango mkubwa sana, pili kuwakutanisha Wanasimba na kufanya mambo ya kijamii mfano kwenda katika hospitali, vituo vya watoto yatima na mambo mengine mengi."
Mwanadada huyo kulingana na mahaba yake na wekundu hao wa Msimbazi aliamua kuchora tattoo zinazoonyesha nembo ya klabu hiyo katika mabega yake mawili, moja akichora kichwa cha Simba na lingine nembo huku mkononi akiandika jina lake.
NYAMBISE (KIGELEGELE YANGA)
Anasema anaipenda Yanga na haoni shida kuhairisha shughuli zake za kumuingizia kipato kwa siku ili akaishangilie Yanga na hupata sapoti kutoka kwa wengine.
"Inapokuwa inacheza mfano mkoani napanga ratiba zangu ili kujiweka sawa kwa safari na kama itaingiliana na siku zangu za biashara maana nauza mitumba katika minada mbalimbali naweka watu mimi naenda kudamshi.
"Unajua kutokana na umaarufu wangu wa kupiga kigelegele hata wasiponiona mashabiki wenzangu wananitafuta, maana kwa gharama zangu nisingeweza kwenda kila Yanga inapokuwa kwa kuwa nashikwa mkono naachaje sasa," anasema.
Anasema wakati mwingine maji yanazidi unga anajilipia na maisha yanasonga na siku za minada Jumamosi Loliondo Kibaha na Jumapili Mlandizi huwa anawaachia vijana wa kumshikia wakati akiwa safarini wanawasiliana kuweka mambo sawa.
YONATHAN NELSONE (WHITE MAPESA)
Anasema anajishughulisha na biashara ya vifaa vya ujenzi anapangilia mambo yake ili muda wa kwenda uwanjani kuishangilia Yanga awepo kwani hawezi kuangalia kwenye runinga.
"Gharama ni kubwa inategemea mechi ni wapi tunakodi gari tunaenda pamoja unakuta mechi za karibu haipungui 100,000 za mbali tunatumia zaidi ya hapo na ni pesa kutoka mfukoni.
"Yanga ikipoteza najisiki vibaya sana maana ndiyo furaha yangu, ila safari inakuwa ngumu sana mechi za nje nasafiri pia nilienda Congo nilitoa takribani Sh700,000 nililipa kwenda na kurudi haijawahi kutokea Yanga ikiwa na mechi nisiende kuitizama ligi zote mechi zote nakuwepo.
"Japokuwa kuna changamoto hasa mke wangu anajua naipenda Yanga inampa wasiwasi mkubwa lakini zaidi ni kuaminiana. Yeye ni Simba anapenda kuangalia ndani haendi uwanjani mara kwa mara."
AKILIMALI MAKAME
Anabainisha kwa namna ambavyo anaipenda Yanga haoni shida changamoto anazokumbana nazo ikiwemo gharama kuhakikisha anakabiliana nazo.
"Mimi ni mfanya biashara nauza vifaa vya simu na huduma za miamala ya simu nikisafiri namuacha mwenzangu yeye ni shabiki wa Simba nikiondoka mimi yeye anabaki tunagawana, japokuwa yeye sio mpenzi sana kama mimi.
"Mimi sijali najitosa tu sikulazimishwa kupenda, nimeipenda mwenyewe na ikitokea timu ziko mkoani yule wa Simba anabaki mimi naenda yeye sio Simba lialia hata uwanjani haendi anaangalia kwenye runinga,"anasema.
Anasema hawezi kuangalia kwenye tv anaenda kushuhudia kabisa na ikitokea siku akakosekana uwanjani labda awe anaumwa.
"Safari zangu zinamkwaza mke wangu kwa asilia 99 ila sielewi najua kabisa namkwaza na siko sahihi lakini ndio mapenzi yangu yalipo, anaona hiyo pesa nikiziingiza kwenye kazi zangu inaweza kuongeza kipato zaidi ananiacha tu kwa kuwa na yeye anaipenda Yanga pia lakini kwa kweli namchukiza kwa kiasi fulani," anasema.