Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ilikuwa wikiendi ya Fei, Mhilu Bara

Fei Toto 9 Goals Kiungo wa Yanga, Feisal Salum "Fei Toto"

Tue, 5 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara iliendelea mwishoni mwa wiki iliyopita, huku ikishuhudia kiungo wa Azam FC, Fei Toto akiibuka na kuongoza msimamo wa wafungaji, ilhali straika wa zamani wa Simba na Kagera Sugar, Yusuph Mhilu akitupia bao la kwanza baada ya siku 442 kupita.

Mwanaspoti linakuleta matukio mbalimbali yaliyojiri wikiendi iliyopita huku yakibamba na kutoa mwelekeo wa ligi.

FEI TOTO MFALME MPYA

Nyota wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwa sasa ndiye kinara wa ufungaji katika Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha mabao 11 na kumpita kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI aliyekuwa anaongoza kwa muda mrefu na mabao 10.

Feisal aliyejiunga na timu hiyo akitokea Yanga msimu huu alimpita Aziz KI baada ya kukifungia kikosi hicho mabao mawili katika ushindi wa 4-1, dhidi ya Dodoma Jiji, mechi iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Kiungo huyo alifunga mabao hayo dakika ya 62 na 64 huku mengine katika mchezo huo yakifungwa na Ayoub Lyanga na, Kipre Junior wakati lile la Dodoma Jiji likifungwa kwa mkwaju wa penalti dakika ya 84 na nyota wa timu hiyo, Emmanuel Martin.

Katika mchezo huo, Feisal alikabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa Novemba mwaka jana baada ya kufunga mabao mawili na kusaidia manne ‘Assisti’ katika dakika 254 za michezo mitatu aliyocheza nyota huyo na kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara.

Feisal alishinda tuzo hiyo baada ya kumshinda nyota wenzake wa Azam FC, Kipre Junior na Maxi Nzengeli wa Yanga alioingia nao fainali.

Msimu huu umekuwa bora zaidi kwa Feisal tofauti na alivyokuwa Yanga misimu miwili iliyopita kwani hajawahi kufikisha mabao zaidi ya saba.

Msimu wa 2021-2022 akiwa Yanga alicheza dakika 2044 katika michezo 26 kati ya 30 ya Ligi Kuu Bara ambapo alifunga mabao sita na kuchangia manne ‘Assisti’ huku msimu uliopita wa 2022-2023 akifunga pia sita tofauti na sasa anapoongoza na 11.

SIKU 442 ZA MHILU

Nyota wa Geita Gold, Yusufu Mhilu ametumia siku 442 kufunga bao la kwanza la Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kukifungia kikosi hicho wakati kilipolazimishwa sare ya 1-1 na KMC, mechi iliyopigwa Machi 2, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex.

Kiungo huyo mshambuliaji aliyejiunga na timu hiyo msimu huu, mara ya mwisho kufunga bao la Ligi Kuu Bara ilikuwa kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam FC wakati akiichezea Kagera Sugar, mechi iliyopigwa Uwanja wa Kaitaba Bukoba Desemba 16, 2022.

Kwa maana hiyo Mhilu ametumia siku 442 ambazo ni sawa na zaidi ya mwaka mmoja na miezi miwili huku akikumbukwa kwani aliwahi kujiunga na Simba Agosti 4, 2021 ingawa mambo yalikuwa magumu na kurejea Kagera Sugar.

TABORA YAFUFUKA

Baada ya mwenendo mbaya wa matokeo katika Ligi Kuu Bara kwa Tabora United, kikosi hicho kilionja ladha ya ushindi wa bao 1-0, juzi dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo mkali na wa kusisimua uliopigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Bao pekee la wenyeji lilifungwa dakika ya tatu tu na nyota wa kikosi hicho Mkongomani, Andy Bikoko na kuhitimisha ukame wa kucheza michezo minane bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Desemba Mosi mwaka jana.

Kwa upande wa Coastal Union hicho kilikuwa kichapo cha kwanza baada ya kucheza michezo sita mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila kupoteza tangu mara ya mwisho ilipofungwa mabao 2-1 na Singida Fountain Gate kwenye Uwanja wa Liti Singida Novemba 27, mwaka jana.

katika michezo sita iliyocheza Coastal bila ya kupoteza, ilishinda mitano huku mmoja tu ukimalizika kwa suluhu dhidi KMC Februari 12, mwaka huu na kuifanya kuendelea kushikilia nafasi ya nne kwenye msimamo na pointi 26 baada ya michezo 18.

KMC, GEITA HAZICHEKANI

Sare ya kufungana bao 1-1 kati ya KMC dhidi ya Geita Gold kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam zimezifanya timu hizo kuendeleza mwenendo mbaya katika Ligi Kuu Bara kwani tangu mwaka huu umeingia hazijapata ushindi.

KMC imecheza michezo minane mfululizo bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mashujaa mabao 3-2, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Desemba 2, mwaka jana ambapo kati ya hiyo iliyocheza imepoteza miwili na sare sita. Kwa upande wa Geita Gold imecheza michezo sita bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Singida Fountain Gate bao 1-0, Desemba 21, mwaka jana kwenye Uwanja wa Nyankumbu ambapo kati ya hiyo imepoteza minne na kutoa sare miwili.

JKT MAMBO BADO

Licha ya JKT Tanzania kushika nafasi ya 13 kwenye msimamo na pointi 19, kikosi hicho kinaendelea kupata wakati mgumu kushinda kwani tayari kimecheza michezo tisa bila kushinda katika Ligi Kuu Bara.

Katika michezo hiyo imetoka sare mitano na kupoteza minne na kuifanya kuendelea kufanya vibaya tangu mara ya mwisho iliposhinda ugenini mabao 2-1, dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu Complex Morogoro Novemba 3, mwaka jana.

DODOMA JIJI BADO

Kocha wa Dodoma Jiji Mkenya, Francis Baraza hajaonja ladha ya ushindi katika michezo ya Ligi Kuu Bara na kikosi hicho tangu alipotangazwa rasmi kukiongoza Desemba 16, mwaka jana akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Mmarekani, Melis Medo.

Baraza aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali hapa nchini huku mara ya mwisho akiifundisha Kagera Sugar 2022, ameiongoza Dodoma Jiji katika jumla ya michezo mitano ambapo kati ya hiyo amepoteza mitatu huku miwili iliyobakia akiambulia sare.

Kocha huyo alitua nchini akichukua nafasi ya Medo aliyeondoka Desemba 4, mwaka jana kwa makubaliano ya pande mbili huku akiiongoza katika jumla ya michezo 12 ya Ligi Kuu Bara ambapo kati yake alishinda minne, sare mitatu na kupoteza mitano.

MSIKIE BARAZA

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Francis Baraza anasema sababu kubwa ya timu nyingi kutofanya vizuri inachangiwa na ugumu wa ligi. “Kila timu ni nzuri kwa sababu hata ukiangalia aina ya wachezaji waliopo unapata picha halisi jinsi ambavyo hali ilivyo, kwangu naona ni suala la kiushindani zaidi na ndio maana ukifanya makosa ni rahisi kuadhibiwa na kukosa pointi tatu,” alisema Baraza.

Chanzo: Mwanaspoti