Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ilikuwa lazima wapewe Thank You

Okrah Morrison Ilikuwa lazima wapewe Thank You

Mon, 26 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba imetangaza kuacha wachezaji nane (hii ni kabla ya jana Jumamosi), huku Yanga ikiwatema wanne, ilihali Azam ikiwapiga chini nyota saba akiwamo aliyekuwa kocha mchezaji, Aggrey Morris aliyedumu katika kikosi hicho kwa muda mrefu.

Simba imewatema Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Beno Kakolanya, Mohamed Ouattara, Augustine Okrah, Nelson Okwa, Gadiel Michael na Victor Akpan, wakati Yanga imewapa 'Thank You' Abdallah Shaibu 'Ninja', Dickson Ambundo, Tuisila Kisinda na winga Bernard Morrison 'BM33'.

Kwa upande wa Azam, mbali na Morris, lakini imempiga chini Bruce Kangwa, Cleophas Mkandala, Ismail Aziz Kader, Kenneth Muguna, Rodgers Kola na kipa Wilbol Maseke (hii ni kabla ya jana).

Huenda idadi ya wachezaji watakaotemwa kwenye timu hizo ikaongezeka kwa vile dirisha la usajili linafunguliwa rasmi Julai Mosi, pia mazungumzo ya ndani kwa ndani kwa klabu hizo na nyingine yanaendelea ili kumalizana na wachezaji ambao hawapo kwenye mipango ya makocha wa timu hizo.

Kuna baadhi ya mastaa walioshangaza kidogo kwa namna walivyoachwa kwenye vikiosi vya timu hizo, lakini ukweli kulikuwa na kila sababu kwa Simba, Yanga na Azam kuwatema iliyowatema na wengine waliopo njiani kupewa 'Thank you', ili kwenda kutafuta changamoto mpya kwingine.

Hapa chini ni sababu kadhaa ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kutemwa kwa wachezaji hao, ikiwemo ukweli kwamba Simba, Yanga na Azam kama ilivyo Singida Big Stars zinajipanga kwa ajili ya michuano ya kimataifa msimu ujao itakayoanza Agosti mwaka huu.

Kwa aina ya mikakati ilizonazo timu hizo ambazo msimu huu ziliiwakilisha Tanzania na Yanga pekee kutoboa hadi kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kung'olewa Ligi ya Mabingwa ambayo Simba iliishia robo fainali na kufungwa na waliokuwa watetezi, Wydad CA ya Morocco.

SIMBA

JONAS MKUDE

Mchezaji huyo mwandamizi aliyeiochezea Simba kwa misimu karibu 12 ameshtusha kuachwa kwake kutokana na nyota aliyedumu na kikosi hicho kwa muda mrefu kuliko yeyote kwa waliopo sasa.

Mkude alianza kuichezea Simba U20 mwaka 2010 kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa msimu wa 2011-2012 na kudumu nayo hadi juzi katyi alipopigwa chini, akiwa na rekodi ya kutwaa na timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tano, Kombe la ASFC mara tatu mbali na mataji ya Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii, akiwamo kuwa nahodha wa timu kwa vipindi tofauti tofauti.

Kuachwa kwake kikosi kumetokana na kumaliza mkataba, lakini hakuwa kwenye miopango ya kocha na hakukuwa na namna ya kumbakisha kwani kwa miaka ya karibu amekuwa mchezaji wa kawaida sana, akiingia matatani kila mara kwa makosa ya utovu wa nidhamu kiasi cha kusimamishwa.

Kwa namna Kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' alivyo na mipango mipya kwa kikosi hicho, ilikuwa ni lazima Mkude atoke ili kupisha damu changa itakayoweza kwenda na kasi ya Mbrazili huyo, kitu cha muhimu ni mabosi wa Simba wampe heshima yake kwa kumuandalizi mechi rasmi ya kumuaga ili kuonyesha kuthamini na kujali mchango wake ndani ya kikosi hicho.

ERASTO NYONI

Ni mmoja ya wachezaji wakongwe kwenye Ligi Kuu Bara, akiwa na umri wa miaka 35 na alikuwa na kikosi cha Simba tangu msimu wa 2017-2018 aliposajiliwa kutoka Azam FC na kuisaidia timu hiyo kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu, mawili ya ASFC mbali na Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi.

Ilikuwa lazima apigwe chini kikosini, kwani ameshindwa kuingia kikosi cha kwanza cha timu hiyo, lakini umri umemtupa mkono, kiasi ule umahiri na uwezo alionao umepungua kwa kiwango kikubwa.

Ingawa kocha Robertinho alikuwa akitaka jamaa akabishwe kwa kazi nyingine, lakini kwa namna ya presha iliyopo nje kwa mashabiki imewalazimisha mabosi wa Simba kuuma jongoo kwa meno na kumpiga chini na zali lake ni kwamba ameshatua Namungo kuendelea kumalizia soka lake.

VICTOR AKPAN

Kiungo huyo Mnigeria aliyesaliwa kwa mbwembwe msimu uliopita akitokea Coastal Union, ilikuwa ngumu kusalia kikosini kutokana na kushindwa kuonyesha makali aliyokuwa nayo kiasi cha kuziingiza vitani Simba na Azam kumwania na Wekundu kufanikiwa kumbeba.

Alikataliwa mapema na Zoran Maki kocha aliyemtangulia Robertinho, akachuniwa na Juma Mgunda na Mbrazili akamkaushia kabvla ya kupelekwa kwa mkopo Ihefu ambako nako alichemsha.

Kwa namna ya mipango iliyokuwepo Simba kwa sasa katika kutaka kujibu mapigo ya watani wao Yanga ya kucgheza fainali za CAF, ilikuwa ngumu Akpan kusalia kikosi cha msimu ujao.

NELSON OKWA

Mnigeria mwingine mwenye kipaji cha soka, lakini aliyeshindwa kufanya mambo Msimbazi tangu aliposajiliwa kutoka Rivers United na kocha Zoran Maki aliyekuwa akimwamini na kumpa nafasi kabla ya kuharibikiwa baada ya kocha huyo kuondoka ghafla Simba.

Alishindwa kuaminika na kukubalika kwa makocha Juma Mgunda na Robertinho na kutolewa kwa mkopo Ihefu ambako japo alijitutumua, lakini haikusaidia kupitishiwa panga Msimbazi, kwani sio sehemu ya mipango ya kocha wa klabu hiyo, hivyo asingeweza kusalia hata kama bado ana mkataba.

AUGUSTINE OKRAH

Mchezaji mwenye uwezo mkubwa aliyesajiliwa kutoka Ghana na kuanza kwa kasi kubwa, kabla ya mambo kumharibikia baada ya kupata majeraha.

Okrah aliyekuwa na mkataba wa mwaka mmoja kati ya miwili aliyoingia wakati akisajiliwa, ana kipaji kikubwa, lakini ukiacha majeraha, inaelezwa tatizo la utovu wa nidhamu umechangia kufupisha maisha yake ndani ya Simba na ilikuwa lazima apewe mkono wa kwaheri.

Ni kweli mashabiki wa Simba wanaukubali uwezo wa Okrah akiondoka akiwa ameifungia mabao manne kwenye Ligi Kuu likiwa lile dhidi ya Yanga mechi ya mkondo wa kwanza iliyoisha kwa sare ya 1-1, lakini hakuwa sehemu ya mipango ya kocha wa timu hiyo, hivyo ilikuwa lazima jamaa apigwe chini kuletwa mashine mpya itakayoisaidia timu kufanya makubwa msimu ujao.

BENO KAKOLANYA

Kipa anayejua kudaka na ambaye imewashangaza mafaza wa timu hiyo kuachwa wakati kipa namba moja akiwa majeruhi atakayekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu wakati msimu mpya ukiwa umeshaanza na kuchanganya.

Kakolanya amemaliza mkataba na alikuwa na nia ya kusalia kikosini, lakini janja janja ya mabosi wa Simba wa kushindwa kumalizana naye mapema, imemfanya akimbilie Singida Big Stars na jambo hilo liliongeza tofauti kubwa baina ya pande hizo hivyo ilikuwa lazima aondoke hata kama angetaka kubadilisha mawazo. Kwa sababu hakuaminika tena Msimbazi, ndio maana mabosi waliridhia kumpiga benchi kwenye mechi muhimu za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika na zile za ASFC.

GADIEL MICHAEL

Beki wa kushoto aliyewahi kung'ara akiwa na Azam, Yanga na Taifa Stars hakuwa na uwezekano wa kusalia kikosini kwa kushindwa kumpa chalenji za kutosha Mohamed Hussein 'Tshabalala' kwenye beki ya kushoto.

Kutokana na kushindwa kwenda na kasi ya kocha Robertinho, ilikuwa ngumu kubakishwa kikosini na utamu zaidi ni kwamba mkataba wake na Simba umefikia ukingoni, hivyo kupewa mkono wa kwaheri lilikuwa ni suala la muda tu.

MOHAMED OUATTARA

Beki wa kati aliyesajiliwa na kocha Zoran Maki akitokea Al Hilal ya Sudan, lakini alishindwa kabisa kuonyesha makali tangu kocha huyo alipotimkia Misri.

Umahiri wa Henock Inonga, Joash Onyango na Kennedy Juma  ilimbana Ouattara kupata nafasi katika kikosi cha kwanza, hivyo ilikuwa lazima apigwe chini kupisha majembe wengine watakaoleta ushindani na kuisaidia Simba kwenye safari yao kwenda 'nchi ya Kaanan'.

YANGA

TUISILA KISINDA

Winga huyu kutoka DR Congo alirejea Yanga kwa mkopo kutoka RS Berkane ya Morocco ilikuwa ni lazima apewe 'Thank You' kwa vile siye yule TK Master aliyewapa raha mashabiki wa Jangwani kipindi alipotua kwa mara ya kwanza.

Kisinda wa safari hii alikuwa hajiamini, hana maamuzi na kushindwa kutumia nafasi zinazotengenezwa, licha ya kuwa kipenzi cha Kocha Nasreddine Nabi aliyeondoka kikosini kwa sasa aliyekuwa akimtumia kila mara hata kwenye mechi usizofikiria anaweza kupangwa.

Kwa vile ameshindwa kuonyesha kile kilichotarajiwa na kwa vile hakuwa mali ya Yanga, ilikuwa ni lazima aachwe ili kupisha wakali watakaoungana na mastaa watakaosalia kuipeleka timu mbali zaidi.

ABDALLAH SHAIBU

Beki huyu wa kati ameshindwa kuonyesha makali tangu arejee kikosini kutoka Marekani kisha kutolewa kwa mkopo Dodoma Jiji na baadaye kurudi Jangwani.

Mchango wake kikosini ni mdogo kwa vile hakuwa chaguo la kocha Nabi, hivyo ilikuwa ngumu kwake kusalia Yanga, kwani alishindwa kupenya mbele ya mabeki wengine wa kati akiwamo Dickson Job, Bakar Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na wakati mwingine Yannick Bangala. Huivyo Thank You ilimhusu zidi kuliko wenzake wengine, kwa vile pia mkataba wake umemalizika.

DICKSON AMBUNDO

Nyota huyu wa zamani wa Alliance, Gor Mahia na Dodoma Jiji alikuwa machachari zaidi kuliko kuwa hatari kama alivyokuwa akicheza kabla ya kutua Jangwani.

Hakuwa chaguo la kwanza, lakini hata alipopewa nafasi hakuwapa raha mashabiki wa Yanga kwa papara alizokuwa nazo na kushindwa kutoa maamuzi ya haraka kuisaidia timu, hivyo kupewa kwake 'Thank You' ilikuwa ni suala la muda, kwani alishamaliza mkataba na klabu.

BERNARD MORRISON

Winga huyu Mghana ana kipaji kikubwa cha soka, lakini hucheza pale anapojisikia na kumfanya ashindwe kuwapa raha mashabiki na hata benchi la ufundi kwa kuonekana hayupo siriazi akiwa ni  mchezaji wa kulipwa tena kutoka nje ya nchi.

Alitua mwanzoni mwaka 2020 na kukaa nusu msimu, akiwa hajafanyaa maajabu yoyote kisha akaenda Siomba ambako nako aliwazingua kwa misimu miwili kabla ya Yanga kuingia upepo na kumbeba kishabiki na kushindwa kuwapa kile ambacho Kocha Nabi alikitarajia kwa winga huyo.

Mwishoni mwa msimu huu, alipambana kutaka kuwaridhisha mabosi wa timu hiyo, lakini kwa aina ya mchango wake kikosini na gharama kubwa za mshahara aliokuwa anapokea ililazimisha kuonyeshwa mlango wa kutoka kwa vile Yanga ijayo mipango yake ni kufika mbali zaidi kwenye mechi za CAF.

AZAM FC

AGGREY MORRIS

Umri alionao na kubadilishiwa majukumu akiwa ni kocha, ilikuwa ni mwanzo wa safari ya nahodha msaidizi huyo na mchezaji mkongwe wa kikosi hicho kusalia kikosini kwa msimu ujao.

Awali ya yote tayari Morris alishatangaza mapema kwamba alikuwa akicheza msimu wa mwisho kabla ya kustaafu ili kupisha damu changa. Alianza kwa kustaafu timu ya taifa aliyofuzu nayo fainali za CHAN 2009.

Kwa vile alishatangaza kustaafu na kuanza kufanya kazi za ukocha, ilikuwa ni safari ya lazima kwa nahodha huyo wa zamani wa Mafunzo aliyesajiliwa Azam na kukaa nao tangu mwaka 2009.

RODGERS KOLA

Mshambuliaji huyo kutoka Zambia, alianza kwa kasi chini ya George Lwandamina kabla ya kupotea taratibu baada ya kundoka kwa kocha huyo na kuja wengine kulimfanya asiendelee kung'ara na kutemwa kwenye kikosi cha kwanza cha Azam.

Uwepo wa nyota wengine wanaocheza kwenye nafasi yake kwa ufanisi ilichangia kuongeza safari ya Kola ambaye naye mktaba wake ulishamalizika na hivyo ilikuwa lazima apewe 'Thank You'.

BRUCE KANGWA

Beki huyu wa kimataifa wa Zimbabwe amemaliza mkataba wake na Wanalambalamba na umri alionao na kile kinachofanywa na mabosi wa Azam ilikuwa lazima apewe Thank You, ili kupisha damub changa ikielezwa tayari kuna kifaa kutoka Senegal, Cheikh Tidiane Sidibé kipo njiani kutua.

Kangwa aliyeichezea Azam tangu 2016 mkataba wake unaisha Julai Mosi na kupungua kwa kasi yake imechangia kumpa nafasi ya kutemwa kikosini, ili Sidibe na Chilambo sambamba na Edward Charles Manyama wanaocheza pia kama beki wa kushoto kuziba nafasi yake kwa msimu ujao.

AZIZ KADER

Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa Azam mwaka 2020 akitokea Tanzania Prisons na kuongezwa mkataba wa mwaka mmoja msimu uliopita uliomalizika, ilikuwa hana nafasi ya kusalia katika timu hiyo kutokana na kushindwa kupenya kikosi cha kwanza.

Mchango wa Aziz Kader sio mkubwa kivile kutokana na mara kadhaa kuwa majeruhi, lakini hata alipopewa nafasi hakuwa na maajabu makubwa na mipango ya mabosi wa Azam kwa msimu ujao ilikuwa ngumu kuweza kubakishwa ndio maana alipewa mkono wa kwaheri kiroho safi.

CLEOPHAS MKANDARA

Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Tanzania Prisons na Dodoma Jiji aliyewahi kuzitoa udenda Simba na Yanga, alishindwa kung'ara katika msimu mmoja aliokuwapo Azam, hivyo ilikuwa ni lazima safari ya kupigwa chini imkute.

Ni mmoja wa viungo mafundi, lakini hakupenya kikosi cha kwanza na ni wazi hayupo kwenye mipango ya kocha mkuu wa timu hiyo,  Youssouph Dabo ndio maana naye kapewa 'Thank You'.

WILBOL MASEKE

Kipa huyo aliyekuzwa ndani ya viunga vya Azam amemaliza mkataba na uwepo wa makipa wa kigeni akiwamo Ali Ahamada, Idrissou Abdulaye imechangia kumfanya Maseke kupigwa chini ili kwenda kutafuta changamoto eneo jingine.

KENNETH MUGUNA

Kiungo huyo Mkenya aliyesajiliwa Azam misimu miwili iliyopita mkataba wake umemalizika na alikuwa na nafasi kubwa ya kuongezwa, lakini kufanya kwake vibaya msimu huu umechangia kwa kiasi kikubwa kupewa 'Thank You'.

Kufanya vizuri kwa Nahodha Sospeter Bajana aliyekuwa tayari ametanguliza mguu mmoja katika klabu ya Simba ili kuvaa uzi wa rangi nyekundu na nyeupe kwa msimu ujao ilikuwa ni sababu kubwa ya kiungo huyo aliyesajiliwa kutoka Gor Mahia kuachwa.

Ndio za ndani zinasema kigogo aliyeshiriki kwa kiasi kikubwa kumsajili alipata wakati mgumu kumtetea Muguna abaki na kumruhusu Bajana na kuamua kuwaangukia Simba wamuache nahodha huyo ili aonmgezwe mkataba na kiungo huyo Mkenya kupewa mkono wa kwaheri bila kupenda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live