Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ile shoo inarudiwa kwa Mkapa

Show Show Ile shoo inarudiwa kwa Mkapa

Mon, 16 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama mambo yataenda vyema, Yanga leo inaweza kuwafanyia mashabiki wake sapraizi kwa kumchezesha kwa mara ya kwanza nyota wake mpya, Kennedy Musonda lakini hamu ya kulipa kisasi inaweza kuwa jambo kubwa wanalotamani kuona likitokea wakati watakapokabiliana na Ihefu SC.

Ihefu ndio timu pekee msimu huu iliyoifunga Yanga na kuitibulia rekodi ya kucheza mechi mfululizo bila kupoteza kwa kuifunga mabao 2-1 kwenye mechi iliyopigwa Novemba 29 mwaka jana jijini Mbeya na kuikwamisha Yanga kufikisha mmechi ya 50 ikiwa Unbeaten na leo itakuwa wageni wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 12;30 jioni.

Kipigo kile cha ugenini hakijaacha kumbukumbu nzuri kwa Yanga kwani sio tu kiliwavuta shati katika mbio za kutetea ubingwa wa ligi, lakini kilihitimisha rasmi rekodi ya kucheza mechi nyingi mfululizo na leo itakuwa na kazi ya kujiuliza ilikuwaje ikafungwa, wakati Ihefu ikitaka kuendeleza ubabe tena.

Tangu hapo, timu hizo mbili kila moja imepita njia yake, Yanga ikiwa haijapoteza muelekeo baada ya matokeo hayo, lakini Ihefu ikiwa na homa ya vipindi kuna muda inashinda na pia kupoteza mechi.

Kwa Yanga, ushindi katika mchezo wa leo utaifanya izidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo kwani itafikisha pointi 53, tisa mbele ya Simba iliyopo nafasi ya pili itakayoshuka uwanjani keshokutwa.

Ihefu yenyewe kama ikaendeleza ubabe kwa kushinda itafikisha pointi 23 zinazoweza kuwasogeza hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi, lakini ikizidi kuivimbia Yanga ambayo kabla ya kipigo cha Novemba 29, ilikuwa haijafungwa tangu Aprili 25, 2021 ilipolazwa na Azam kwa bao 1-0.

Watetezi hao wamekuwa na mwendelezo mzuri wa ubora katika mechi za hivi karibuni ambapo wamecheza mechi sita mfululizo bila kupoteza huku Ihefu wenyewe wakiwa na matokeo ya wastani ambapo katika mechi sita zilizopita, wamepata ushindi mara nne na kupoteza mbili.

Pamoja na kupoteza mchezo uliopita baina yao, Yanga imekuwa na historia ya ubabe dhidi ya Ihefu ambapo kiujumla zimekutana mara tatu katika Ligi Kuu, Yanga wakipata ushindi mara mbili na moja ndio iliyopoteza, wakati Ihefu ikinolewa na aliyewahi kuwa kocha wa Jangwani, Juma Mwambusi.

Wakati wenyeji Yanga wakiingia katika mchezo wa leo huku wakiwa na historia ya ubabe katika mechi zao za nyumbani, Ihefu wenyewe wamekuwa wanyonge kupitiliza ugenini na michezo iliyopita ya Ligi Kuu kwa timu hizo inathibitisha hilo.

Tangu Ihefu imeanza kushiriki Ligi Kuu hadi sasa, imecheza jumla ya mechi 27 ugenini ambapo kati ya hizo imepata ushindi mara mbili tu tena dhidi ya Ruvu Shooting, imetoka sare mechi sita na imepoteza michezo 19 huku ikifunga mabao 10 tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 39.

Yanga yenyewe katika mechi zake 27 zilizopita za Ligi Kuu ambazo ilikuwa nyumbani, imepata ushindi mara 21, ikitoka sare tano na kupoteza mchezo mmoja ambapo imefunga jumla ya mabao 54 na yenyewe imefungwa mabao 10 tu.

Katika mchezo wa leo Ihefu huenda ikawa na sura mpya baada ya kuingiza vifaa vipya kupuitia dirisha dogo akiwamo Adam Adam, David Mwantika na Said Mudathir, huku Nelson Okwa, Victor Akpan na Yacouba Songne nao wakitajwa kutua kikosini hapo na kumpa kazi Zubery Katwila.

Chanzo: Mwanaspoti