Straika wa Mtibwa Sugar, Charles Ilanfya amesema hawezi kukatishwa tamaa na maneno ya watu kuhusu kupata kadi nyingi za njano kwenye ligi kuu kwani hiyo ni moja ya kazi yake kuipambania timu.
Amesema hawezi kuacha mpinzani kuleta madhara kwa timu yao akamuacha apete bali atapambana naye na uamuzi wa refa ndio utaamua kama amecheza rafu au vinginevyo.
Hadi sasa nyota huyo aliyewahi kucheza Mwadui, KMC na Simba tayari ameoneshwa kadi saba za njano na nyekundu moja katika mechi 22 zilizochezwa kwenye ligi.
Akizungumza na Mwanaspoti leo baada ya mchezo wao dhidi ya Prisons uliomalizika kwa suluhu kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa, Ilanfya amesema kadi inaweza kumpata yeyote katika nia ya kuipambania timu.
Kuhusu ufungaji amekiri kuwapo changamoto katika kutumia nafasi akieleza kuwa lazima wenzake wafahamu si jukumu la mmoja bali yeyote anayekuwa uwanjani anaweza kufunga anapopata nafasi.
“Kadi naipata kutokana na kupambania timu, haiwezi kunitoa mchezoni na siwezi kuacha mtu aende kufunga nimuache, kimsingi nashukuru kulinda kiwango changu kutokana na kufuata maelekezo ya kocha,” amesema Ilanfya.