Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ihefu yaziachia msala Prisons, City

Zubery Katwila Kocha wa Ihefu, Zubery Katwila

Tue, 7 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ushindi wa mabao 2-0 walioupata Ihefu juzi katika Uwanja wa Highland Estate, Mbarali dhidi ya Mbeya City umeitoa timu hiyo kwenye orodha ya zile zilizokuwa katika hatari ya kushuka daraja.

Ihefu sasa inawania kumaliza msimu ndani ya ‘top six’ na kuziacha Mbeya City na Tanzania Prisons kuwa kwenye presha kubwa baada ya kuzichapa timu zote msimu huu.

Ihefu ilianza Ligi Kuu vibaya kwani ilichukua dakika 540 bila kuonja alama tatu na mchezo wa kwanza kushinda ulikuwa dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao 2-1 pale Highland Estastes, Oktoba 16.

Timu hiyo iliburuza mkia kwa muda mrefu hadi ilipoichapa Yanga mabao 2-1 Novemba 29 na kuvuna alama tatu ambazo ziliitoa mkiani kwa kufikisha alama 11.

Katika michezo saba ya nyuma imeshinda mitano na kupoteza miwili dhidi ya Yanga 1-0 na 2-0 dhidi ya Namungo FC yote ikicheza ugenini.

Hadi sasa imesaliwa na michezo minane kumalizika msimu, michezo sita nyumbani na ugenini miwili. Michezo ya ugenini ni dhidi ya Dodoma Jiji utakaopigwa Februari 24, Polisi Tanzania (Aprili 21) na ule wa Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Mei 14 ilhali nyumbani itaikaribisha Singida United, Azam FC, Geita Gold, Kagera Sugar na Simba.

Upande wa Mbeya City ina michezo mitano ugenini huku mitatu ikiwa katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting, Yanga kisha itamaliza msimu dhidi ya KMC.

Prisons ina kibarua kigumu mbele yake licha ya kushika nafasi mbaya pia inakabiliwa na michezo mingi - mitano ugenini kati ya minane iliyosalia kufunga msimu huku mitatu ya nyumbani ni dhidi ya Ruvu Shooting, KMC na Yanga.

Kocha wa Ihefu, Zubery Katwila alisema anashukuru kuwaona vijana wake wanapambana kuitoa timu mkiani baada ya kufanya vibaya muda mrefu. “Hizi pongezi zinamhusu kila mmoja wetu kwa kufanya kazi yake vizuri sababu tulikuwa na hali mbaya lakini hatukukata tamaa na vijana wamepigana hadi kutoka mkiani,” alisema.

Ihefu imekuwa na rekodi tamu nyumbani kwani mara ya mwisho kupoteza ikiwa Highland Estates ilikuwa Novemba 17 mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania.

Chanzo: Mwanaspoti