Tukiwa tunahesabu saa tu dirisha la usajili kufungwa kesho Jumatatu saa 5:59 usiku uongozi wa Ihefu FC umeibomoa Singida Fountaine Gate baada ya kunyakua mastaa wake sita wa kikosi cha kwanza akiwemo kiungo fundi Marouf Tchakei.
Mbali na staa huyo ambaye ni kinara wa upachikaji mabao akiifungia Singida Fountaine Gate mabao matano msimu huu yumo Bruno Gomes, Joash Onyango, Elvis Rupia, Duke Abuya na Aboubakari Khomeini.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa Ihefu FC kimeliambia Mwanaspoti kuwa tayari wachezaji hao wameingia kambini na wanaendelea kujifua kwaajili ya kumalizia msimu huu wa Ligi Kuu.
"Wachezaji hao sita wa kigeni wapo kambini jijini Arusha wanaendelea kujifua kwaajili ya kujiweka tayari kuipambania Ihefu FC kutoka kwenye nafasi mbaya iliyopo sasa;
"Usajili huo ni mapendekezo ya kocha Mecky Maxime ambaye ameungana na timu akitokea Kagera Sugar anaamini usajili huo utamsaidia kuifanya timu hii imalize nafasi nne za juu," kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake litajwe gazetini.
Kilisema usajili huo ni wazi wachezaji wengi wa kigeni waliokuwa ndani ya kikosi watapicha usajili huo mpya na mastaa wa kigeni ambao wanakalia kuti kavu ndani ya Ihefu ni pamoja na Never Tigere ambaye mkataba wake umeisha, Moubarack Hamza na Victar Akpan.