Wakati timu za ligi kuu, Championship na firs league zikiendelea kuimarisha vikosi vyao, Ihefu nayo imezidi kusuka kikosi chake ikiwaongezea mikataba mastaa wao waliong'ara msimu uliopita.
Timu hiyo inayojiandaa kushiriki ligi kuu kwa mara ya tatu imewaongezea mkataba wachezaji Jafari Kibaya, Lenny Kissu na Rafael Daud 'Loth' na kumsajili Mbaraka Amza aliyekuwa kinara wa mabao (8) katika kikosi cha Coastal Union.
Ihefu inatarajia kuingia kambini wiki ijayo kuanzia kesho Jumatatu ikielezwa kujificha wilayani Tukuyu kutokana na marekebisho yanayoendelea kwenye uwanja wake wa Highland Estate wilayani Mbarali.
Timu hiyo ambayo ilinolewa na makocha watatu kwa muda tofauti ikianza na Zuberi Katwila ambaye aliongezewa nguvu ya Juma Mwambusi kabla ya kutemana na kumpa kazi John Simkoko imeanza kujisuka kwa ajili ya msimu ujao.
Hadi sasa timu hiyo ya mkoani Mbeya, imeondokewa na nyota watatu ikiwa ni Yahya Mbegu aliyetimkia Singida Fountain Gate, Adam Adam (Mashujaa), Nico Wadada na kipa James Ssetuba aliyetimka mwishoni mwa msimu.