Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ihefu yaifuata Yanga kibabe

Ihefu Ushindiiii Ihefu yaifuata Yanga kibabe

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ihefu imeungana na timu nyingine za Ligi Kuu, Yanga, KMC, Namungo, Singida Fountain Gate, Geita Gold, Mashujaa, Tabora United, Geita Gold na Mtibwa Sugar kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), baada ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa raundi ya tatu dhidi ya Mbuni.

Timu hiyo yenye maskani yake Mbarali mkoani Mbeya, imesonga mbele leo Februari 22, 2024 kwa kuifunga Mbuni FC ya Arusha mabao 2-0 katika mchezo ambao umepigwa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Ihefu ilifunga bao la kwanza dakika ya 15 kupitia kwa winga Mkongomani, Emmanuel Lobota aliyesajiliwa dirisha dogo akitokea FC Lupopo, likiwa ni bao lake la kwanza tangu atue nchini.

Bao la pili limefungwa na kiungo Mkenya, Duke Abuya dakika ya 55 na kuipeleka timu hiyo hatua ya 16 bora, ambayo mpaka sasa imetawaliwa na timu za Ligi Kuu, baada ya Geita Gold na Tabora United nazo kushinda mechi zake leo na kuzipukutisha timu za Championship na madaraja mengine ya chini.

Huo ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Ihefu katika mashindano yote, ikiifunga Mtibwa mabao 3-2, Geita Gold 2-1 na Mbuni 2-0, ikiwa haijapoteza mchezo tangu ianze kunolewa na kocha Mecky Maxime aliyetua klabuni hapo Desemba 27, 2023.

Mara ya mwisho Ihefu kupoteza mchezo ilikuwa ugenini dhidi ya Dodoma Jiji Desemba 18, 2023 ilipochapwa bao 1-0, ambapo Jumapili itakuwa ugenini tena katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kuvaana na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu.

Baada ya leo Mbuni FC ya Arusha inayoshiriki Championship, timu nyingine ambazo tayari zimeshaaga mashindano hayo ni Stand United, Biashara United, Transit Camp, Pamba Jiji, Copco, Ken Gold, FGA Talents na Polisi Tanzania.

Sasa matumaini pekee ya Championship yamebaki kwa Green Warriors inayocheza na Azam FC muda huu  katika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, huku First League ikibakisha timu moja ya TRA FC kutoka Kilimanjaro itakayomenyana na Simba.

Nayo, Tabora United, imesonga mbele kwenye michuano hiyo ya Shirikisho baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Nyamongo FC ya mkoani Mara, katika Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi, Tabora, huku mabao ya ushindi huo yakifungwa na Daud Milandu na Yohana Mkomolwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live