Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Zuberi Katwila, amesema mechi ijayo ataingia na mbinu mpya na silaha zake zote zilizosajiliwa kipindi cha dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu.
Ihefu FC imefanya usajili wa nyota wapya akiwamo Adam Adam aliyecheza mechi dhidi ya Yanga, Victor Akpan na Nelson Okwa wakitokea Simba na Yacouba Songne.
Nyota hao wanatarajia kuonekana kwenye mechi ijayo Ihefu itakapocheza na Prisons Jumamosi hii.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katwila alisema ameona madhaifu yaliyojitokeza katika mechi dhidi ya Yanga na kufanyia kazi haraka huku akitarajia kufanya mabadiliko katika kikosi chake kwenye mchezo huo dhidi ya Prisons.
Alisema mechi iliyopita na Yanga alifanya mabadiliko madogo safu ya ushambuliaji kwa kumwanzisha Adam na anatarajia mechi ijayo kikosi kuwa na mabadiliko makubwa.
“Mechi iliyopita na Yanga , tumefanya makosa na tunarudi uwanja wa mazoezi kufanyika kazi mapungufu yetu na kuboresha ubora tuliokuwa nao, nina matarajio mechi ijayo kutakuwa na mabadiliko ya kikosi na kuingia na mbinu tofauti na mechi iliyopita,” alisema Katwila.
Alisema mabadiliko hayo ni kuhakikisha anawapa nafasi nyota wapya waliowasajili kipindi cha dirisha dogo ninaimani ni wachezaji wazuri na watasaidia timu kufikia malengo yetu ya kunusuru timu kutoshuka daraja.
Ihefu inashika nafasi ya 13 ya nne kutoka chini, ikiwa tayari imecheza mechi 20, imeshinda sita, sare mbili na amepoteza michezo 12 wakikusanya alama 20 katika msimamo wa ligi hiyo.