Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ihefu kuendeleza ubabe kwa Yanga?

Mzize Yanga Konkoni Skudu Mwamnyeto Ihefu kuendeleza ubabe kwa Yanga?

Tue, 3 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ligi Kuu Bara inaendelea tena leo kwa michezo miwili kupigwa ambapo Azam watakuwa wageni wa Dodoma Jiji huku Mashujaa wakipambana na JKT Tz lakini macho na masikio ya mashabiki yakielekezwa kwenye Uwanja wa Highland Estate jijini Mbeya ambapo wenyeji Ihefu itaikaribisha mabingwa watetezi Yanga kesho Jumatano.

Timu hizi zinakutana kwenye uwanja huo huku Ihefu ikiwa na kumbukumbu nzuri mara ya mwisho ilipokutana na Yanga Novemba 29, mwaka jana ambapo ilishinda mabao 2-1, yaliyofungwa na nyota, Never Tigere na Lenny Kissu.

Mchezo huo uliwashangaza mashabiki wengi nchini kutokana na kitendo cha kutotegemea Yanga kupoteza kirahisi kwa sababu ya kiwango ilichokuwa nacho hali iliyosababisha kuvunja rekodi yao ya kutopoteza kwenye ligi.

Kabla ya mchezo huo Yanga ilikuwa imecheza mechi 49 za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza ikiwa imeifikia rekodi iliyowekwa na klabu ya Arsenal ya nchini England msimu wa 2003/2004 kuanzia Mei 7, 2003 hadi Oktoba 16, 2004.

Rekodi hiyo ilivunjwa na Ihefu baada ya Yanga kucheza muda mrefu bila kupoteza tangu mara ya mwisho kuchezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Azam FC Aprili 25, 2021, lililofungwa na nyota wa timu hiyo, Mzimbabwe Prince Dube.

Mchezo huu wa mzunguko wa nne unazikutanisha timu hizo huku Yanga ikiwa tishio zaidi kwani katika michezo mitatu iliyocheza imefunga mabao 11 bila nyavu zao kutikiswa wakati Ihefu ikifunga moja na kuruhusu matatu.

Huu utakuwa ni mchezo wa tano kwa timu hizo kukutana ambapo Yanga imekuwa na rekodi nzuri mbele ya wapinzani wao kwani imeshinda mitatu na kupoteza mmoja tu ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao saba na kuruhusu mawili.

Akizungumza Kocha mkuu wa Ihefu, Zuberi Katwila alikiri mchezo huo utakuwa ni mgumu na licha ya ubora wa wapinzani wao ila wamejipanga vyema kwa ajili ya kuhakikisha wanabaki na pointi zote tatu.

"Tumekuwa na maandalizi mazuri na tumeiona Yanga, kimsingi ni kudhibiti mashambulizi kucheza mtu na mtu, makosa yaliyoonekana katika mechi iliyopita tumeyarekebisha hivyo vijana wana ari na morali kubwa," alisema.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo huku akieleza licha ya ugumu uliopo mbele yao ila wamejipanga vyema ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: