Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ihefu ijayo mtaipenda

Ihefu Waitaka Simba Wachezaji wa Ihefu

Tue, 13 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kumaliza nafasi ya sita kwa pointi 39, Ihefu imetamba msimu ujao inasaka nafasi tatu za juu huku ikielezea maandalizi yao ikiwamo maboresho ili kuleta ushindani klwenye ligi kuu.

Timu hiyo ya wilayani Mbarali mkoani hapa iliwahi kupanda na kushuka daraja, haikuwa na mwanzo mzuri kwenye ligi kabla ya kuamka na kufanya vyema ikiandika rekodi ya kuwa wa kwanza kuwasimamisha Yanga iliyokuwa imecheza zaidi ya mechi 40 bila kupoteza.

Hata hivyo, vijana hao wa ‘Mbogo maji’ walijikuta wakiongozwa na makocha watatu tofauti wakianza na Zuberi Katwila, Juma Mwambusi aliyetemwa muda mfupi kabla ya kumpa tena kazi John Simkoko.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Katwila alisema wanashukuru matokeo waliyomaliza nayo japokuwa walitamani kushika nafasi nne za juu na hata kutwaa ubingwa na kwamba kwa sasa wanaenda kujipanga upya na msimu ujao.

Alisema ishu ya kufanya maboresho ni muhimu kwa timu yenye malengo lakini kutegemea na makubaliano ya wachezaji na uongozi kwani mpira ni maisha na kwamba wanaamini watafanya vizuri msimu ujao.

“Tunaenda kufanya tathimini kujua wapi tulikosea ili kurekebisha kwa ajili ya msimu ujao tuweze kufanya vizuri na kuwania nafasi tatu za juu, kubaki kwa mchezaji inategemea mkataba na makubaliano, mpira ni maisha ya mtu,” alisema Katwila.

Naye nyota wa timu hiyo, Raphael Daud 'Loth' alisema mafanikio hayo yalitokana na ushirikiano wa kila mmoja ndani na nje ya uwanja na kujituma na kwamba wanaamini msimu ujao utakuwa mzuri zaidi kwao.

“Kimsingi ni kwenda kujipanga upya na kila mmoja kuangalia wapi aliteleza kujirekebisha lakini kwa ujumla haikuwa msimu mbaya kutokana na nafasi tuliyomaliza ukizingatia ushindani ulivyokuwa,” alisema nyota huyo wa zamani wa Meya City na Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti