Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ihefu, Yanga ni kisasi na ubabe

Kisasi Ubabe Yanga Ihefu, Yanga ni kisasi na ubabe

Wed, 4 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hamu ya kuendeleza ubabe kwa Ihefu na ile ya kulipa kisasi kwa Yanga ni mambo yanayoipa mvuto mechi ya Ligi Kuu baina ya timu hizo leo kwenye Uwanja wa Highland Estates, Mbalali kuanzia saa 10:00 jioni.

Matokeo ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu uliozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja huo msimu uliopita ambapo Ihefu iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 ndio yanayoonekana kuchangia zaidi kuongeza msisimko wa mechi hiyo ya leo kwani yaliifanya Ihefu kuizuia Yanga kuweka rekodi ya kucheza mechi 49 za Ligi Kuu bila kupoteza.

Yanga inaingia katika mechi ya leo ikiwa na historia ya ubabe dhidi ya Ihefu kwani zimekutana mara nne kwenye Ligi Kuu, ikipoteza mechi moja na kuibuka na ushindi katika michezo mitatu.

Mbali na hilo, mabingwa hao watetezi wanaonekana kuwa na mwanzo mzuri katika ligi kuu msimu huu ambapo wameibuka na ushindi katika mechi zao zote tatu zilizopita dhidi ya KMC, JKT Tanzania na Namungo FC, huku wakifunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara mbili tu.

Ni tofauti na Ihefu ambayo katika michezo mitatu iliyopita, imepata ushindi mara moja tu na kupoteza mechi mbili, ikifunga bao moja na yenyewe imefungwa mabao mawili.

Kocha wa Ihefu, Zuberi Katwila alisema wameifatilia Yanga katika mechi zao na alikiri mchezo utakuwa mgumu lakini lengo lao ni kupata pointi tatu.

Katwila alisema walikuwa na maandalizi mazuri kwa muda mrefu hivyo walipata nafasi ya kufanya marekebisho ambayo yalionekana katika mchezo wao uliopita dhidi ya Mashujaa Fc.

"Tumekuwa na maandalizi mazuri na tumewaona Yanga. Kimsingi ni kudhibiti mashambulizi, kucheza mtu na mtu, makosa yaliyoonekana katika mechi iliyopita tumeyarekebisha.

"Lazima tutumie udhaifu wao tuliouona kuweza kushinda mchezo huo na kujiweka pazuri. Sisi tunahitaji kujinasua nafasi za chini na kupanda juu, vijana wana ari na morali kufikia malengo,"alisema Katwila.

Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema hawakuwa na muda mwingi wa maandalizi baada ya kutoka kucheza mechi ya kimataifa lakini anaamini watafanya vizuri.

"Tumefanya vizuri katika mechi zetu tatu za mwanzo na tunataka kuendelea jinsi tulivyoanza. Tunawaheshimu wapinzani wetu lakini tunataka pointi tatu.

"Wapo wachezaji ambao wana matatizo lakini mazoezi ya leo ya mwisho (jana) tutajua tunaingia na wachezaji gani katika mchezo huu," alisema Gamondi.

Mzunguko wa nne wa Ligi Kuu, utafungwa rasmi kesho kwa Tanzania Prisons kuialika Simba katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Mtibwa Sugar itakuwa nyumbani kucheza na Singida Big Stars.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: