Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ihefu Maji ya Shingo Ligi Kuu NBC

Ihefu Vs Dodoma Jiji.jpeg Polisi Tanzania wameibuka na ushindi ugenini

Thu, 17 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uwanja wa Highland Estate umeendelea kuwa mgumu kwa wenyeji Ihefu baada ya leo kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania, huku bao la kujifunga kwa mchezaji wake, Samuel Onditi likiizima timu hiyo na kuendelea kubaki mkiani kwa pointi zao sita.

Mchezo huo ambao ulikuwa wa tano kwa Kocha wake Mkuu, Juma Mwambusi Ihefu ndio wakitangulia kupata bao dakika ya 14 kupitia kwa Andrew Simchimba kwa penalti baada ya Joseph Mahundi kuangushwa eneo la hatari na zofuatazo ni dondoo za dakika 90 za mtanange huo.

Kabla ya mchezo huo timu hizo zilikuwa zimekutana mara mbili, ambapo hakuna aliyekuwa amewahi kumfunga mwenzake ikiwa ni sare tu na leo rekodi imewekwa na Maafande hao.

Katika mechi ya mwisho kukutana timu hizo msimu uliopita zilitoka sare ya 1-1 huku mabao yakifungwa na Rafael Daud (Ihefu) na Kassim Haruna aliyeosawazishia Polisi Tanzania.

Ihefu unakuwa mchezo wake wa tatu kupoteza nyumbani kati ya tano iliyocheza nyumbani kwenye uwanja wa Highland Estate Mbarali huku ushindi ikiwa mechi moja sawa na sare.

Bao alilofunga Straika Andrew Simchimba leo kwa penalti linakuwa la 17 kwake akiitumikia Ihefu tangu alipoipandisha daraja msimu wa 2020/21.

Bao la Vitalis Mayanga kwa Polisi Tanzania linamfanya kufikisha mawili msimu huu huku yote akiyavuna kwa timu za Mbeya akianza na Mbeya City walipolala 3-1 kwenye uwanja wa Sokoine.

Samuel Onditi wa Ihefu anafikisha idadi ya wachezaji nane waliojifunga hadi sasa kwenye ligi kuu baada ya mpira wake wa kichwa akiokoa kona kujaa wavuni.

Matokeo hayo yanaifanya Polisi Tanzania kuishusha Dodoma Jiji kwa wastani wa mabao ya kufunga (18-15) japokuwa pointi zinakuwa sawa alama tisa huku Maafande wakiwa mbele kwa mchezo mmoja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live