Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ihefu: Kwani mlitakaje?

Ihefu Yanga Ns Ihefu: Kwani mlitakaje?

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga jana ilionja kipigo cha kwanza kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kufungwa mabao 2-1 na Ihefu kwenye mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Highland Estate, jijini Mbeya, huku mashabiki wa timu hiyo wakiulizwa kwa kejeli na wenyeji wao...'Kwani nyie mlitakaje...?

Mashabiki hao walikejeli wenzao wa Yanga, wakirejea rekodi ya msimu uliopita walipoifumua pia Yanga kwenye uwanja huo huo kama ilivyofanya jana na kuwanyima furaha wapenzi wa Yanga ambao kwenye mechi nane zilizopita za mashindano walikuwa wakipata burudani ya soka tamu la kikosi hicho.

Kama ilivyokuwa kwenye mechi ya msimu uliopita iliyopigwa uwanjani hapo, Novemba 29 mwaka jana kwa Yanga iliyokuwa chini ya Nasreddine Nabi aliyetibuliwa rekodi ya kushinda mechi 49 bila kupoteza, ndivyo ilivyotokea tena jana kwa Ihefu

Kipigo hicho kimeifanya Yanga kusalia nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi nne, ikifunga mabao 12 na kufungwa mawili, na kutoa nafasi ya kuporomoka hadi nafasi ya tatu iwapo watani wao, Simba leo itapata ushindi mbele ya Tanzania Prisons.

Mabao ya dakika 40 lililokuwa la kusawazisha kupitia kwa Lenny Kissu na lile la ushindi la Charles Ilanfya la dakika ya 67, yalitosha kumtibulia kipa Diarra Djigui aliyekuwa hajafungwa bao hadi sasa katika ligi, huku akiendelea uteja wa kutunguliwa kwenye uwanja huo kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Katika mechi ya msimu uliopita Diarra pia alitunguliwa na Lenny Kissu, huku bao la kwanza la kusawazisha la Ihefu liliweka kimiani kwa friikikii na Never Tigere ambaye jana alipiga friikiki kabla ya Kissu kuwahi na kutumbikiza wavuni na kuhitimisha rekodi ya Yanga ya kushinda mfululizo katika mechi hiyo ya 50.

Kama ilivyokuwa kwenye mechi iliyopita, Yanga ndio iliyokuwa ya kwanza kufunga bao kupitia Pacome Zouzoua dakika ya nne tu aliyemalizia pasi tamu ya Clement Mzize, likitofautiana kwa dakika tano na bao lililofungwa na Yannick Bangala kwenye mechi hiyo ya msimu uliopita ambaye kwa sasa anakipiga Azam FC.

KIUNGO KILIPOTEA

Kocha Gamondi aliingia uwanjani kingine kabisa na kile kilichozoeleka akiwatumia zaidi wachezaji wa akiba, na athari ilionekana kwa mara ya kwanza msimu huu Yanga kupata shida kubwa eneo la kiungo ikishindwa kumiliki mpira na hata kuzidiwa kwenye mchezo wao huo wa kwanza wa ugenini msimu huu.

Viungo Salum Abubakar 'Sure boy' na Zawadi Mauya walioanza mchezo wa kwanza msimu huu kwenye ligi hawakuweza kufanya vizuri eneo hilo na kuwafanya Ihefu kutulia na kupanga mashambulizi yake.

Yanga ikafanya mabadiliko matatu dakika ya 56 kwa kuwatoa beki wa kulia Kibwana Shomari aliyeonekana kutokuwa sawasawa nafasi yake ikichukuliwa na Yao Kouassi kisha akatoka Sure Boy nafasi yake ikichukuliwa na Mu dathir Yahya, huku pia akitoka winga Mahlatse Makudubela 'Skudu' aliyeanzishwa jana akimpisha Stephanie Aziz KI.

Mabadiliko hayo yaliwatuliza kwa nafasi flani Yanga lakini bado haikusaidia wakajikuta wanaruhusu bao la pili dakika ya 67 mfungaji akiwa mshambuliaji Charles Ilamfya akipokea pasi ya mkongwe Joseph Mahundi.

Bao hilo hakuna kingine ambacho Yanga watalazimika kujilaumu zaidi ya kushindwa kukaba kwa nidhamu wakiwa nyuma watu watano huku Ihefu ikiwa na watu watatu pekee na bao hilo likafungwa.

IHEFU ILIFANIKIWA

Ihefu ikiwa chini ya kocha Zubery Katwila, iliingia na mbinu za kiufundi za kuibana zaidi Yanga kwa kuzuia kutembeza mpira kama ilivyozoeleka kwa viungo wake wakiongoza na Victor Akpan wakitibua kila aina ya shambulizi, huku mabeki Juma Nyosso na Lenny Kissu wakiwa makini kumlinda kipa Seleman Fikirini.

GAMONDI AJIPANGE UGENINI

Huo ni mchezo wa kwanza kwa Yanga kupoteza msimu huu tena akiwa ametoka nje ya kwao lakini pia wakishindwa kucheza kwa utulivu kwa soka lao la pasi ambapo kocha wa Yanga Miguel Gamondi anatakiwa kukuna kichwa jinsi ya kuifanya timu yake icheze kwa ubora ugenini ambako viwanja vyake sio rahisi kuruhusu mpira wa kuwekwa chini.

Vikosi vilivyoanza;

IHEFU: Fikirini, Kunambi, Baba Ubaya, Nyosso, Kissu, Akpan, Saadun, Manyasi, Martin, Amza nas Tigere

YANGA: Diarra, Kibwana, KIbabage, Bacca, Mwamnyeto, Mauya, Moloko, Sure Boy, Mzize, Pacome na Skudu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: