Mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kati ya Simba na Ihefu utapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi saa 1:00 usiku badala ya kuchezwa Uwanja wa Uhuru kama ilivyotangazwa hapo awali, huku wageni wakisema hata huko wao wanaona freshi tu.
Inadaiwa Uwanja wa Uhuru siku ya mchezo huo una matumizi mengine na kulazimisha waandaaji wa michuano ya ASFC, Shirikisho la Soka (TFF) kuhamishia huko kwa kushauriana na wenyeji wa pambano hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salam, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema sababu kubwa za mabadiliko hayo ni kutokana na Uwanja wa Uhuru uliopangiwa kutumika kwa shughuli nyingine.
"Tumepokea mabadiliko hayo kwa sababu Uwanja wa Uhuru siku hiyo ya Ijumaa utatumika kwa ajili ya mashindano makubwa ya usomaji wa Quran tukufu hivyo tukaona ni vyema tuhamishie mchezo wetu Chamazi," alisema Ahmed.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Ihefu, John Simkoko alisema kubadilishwa kwa uwanja hakuwezi kuathiri kikosi chao kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya kwa sababu hata kabla ya hapo isingekuwa mchezo mwepesi.
Mshindi wa jumla kati ya timu hizo atakutana na Azam FC katika hatua ya nusu fainali baada ya kikosi hicho cha matajiri wa jiji la Dar es Salaam kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar Jumatatu iliyopita.
Simba ilifika hatua hiyo baada ya kushinda mabao 4-0 dhidi ya African Sports huku Ihefu ikishinda 2-0 na Pan Africans katika michezo ya raundi ya 16 bora. Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara timu hizo zilipokutana Simba ilishinda bao 1-0 Novemba 12, mwaka jana lililofungwa na Pape Sakho.
Baada hapo timu hizo zitakutana tena Aprili 10 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Highland Estate Mbeya.
Singida Big Stars ndio timu ya kwanza hadi sasa kutangulia nusu fainali baada ya kuifunga Mtibwa Sugar kwa mabao 4-1 kwenye mechi ta robo fainali iliyopigwa wikiendi iliyopita mjini Singida.