Taarifa za ndani zimeeleza kuwa Kelechi Iheanacho huenda hatimaye akaonja michuano ya Afcon 2023 kwa kuchukua nafasi ya Samuel Chukwueze katika mechi ya mwisho ya Nigeria ya Kundi A ambayo ni lazima washinde dhidi ya Guinea Bissau.
Iheanacho amepona majeraha ya misuli hivyo huenda akamng’oa Chukwueze, ambaye alikosa makali baada ya kuanzishwa katika kikosi kilichoshinda 1-0 dhidi ya wenyeji Ivory Coast.
Straika wa Leicester City, Iheanacho, ambaye ametangaza mwenyewe kwamba yuko “fiti asilimia 100” , ameng’ara mazoezini akifunga mabao na kuonyesha kiwango bora kiujumla.
Hata hivyo, staa huyo bado hajacheza hata dakika moja katika michuano ya mwaka huu ambayo imemaliza raundi mbili za kwanza za mechi.
Kocha Jose Peseiro ameitaka timu yake kuwa na utulivu zaidi katika umaliziaji mbele ya lango na anatumai itakuwa hivyo dhidi ya Guinea Bissau leo.
Ushindi mkubwa dhidi ya Wild Dogs, utaihakikishia ‘Super Eagles’ kutinga 16-Bora kama vinara, Eq Guinea wakizubaa.