Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Idrisu nje miezi minne

Idrissu Abdulai WFt Idrisu nje miezi minne

Mon, 25 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabosi wa Azam FC kwa sasa wanakuna vichwa kutokana na makipa wawili tegemeo, Abdulai Iddrisu na Ali Ahamada kuwa majeruhi, huku ikifahamika wazi kuwa, Idrissu atakuwa nje ya uwanja kwa miezi minne baada ya kupasuliwa bega lake la mkono wa kushoto Afrika Kusini.

Ahamada kwa upande wake ametimkia Ufaransa ili kwenda kujiuguza na haijulikani atarudi lini nchini wakati vinara hao wa Ligi Kuu Bara wakijiandaa kwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024.

Akizungumza na Mwanaspoti, daktari wa timu hiyo, Mbaruku Mlinga amesema ni habari mbaya kwa timu hiyo na kipa Idrissu kutokana na umuhimu wake kikosini ingawa hawana budi kumuombea apone haraka na kurejea katika majukumu yake ya kawaida.

“Jeraha lake lilionekana siriasi kidogo ndio maana akaenda Afrika Kusini na tunashukuru upasuaji wake umefanyika salama japo ndio hivyo atakuwa nje kwa kipindi kirefu, anaendelea na matibabu chini ya uangalizi mzuri wa madaktari,” alisema Dk Mlinga.

Dk Mlinga aliongeza mbali na Iddrisu, kipa mwingine, Ali Ahamada aliyekwenda pia Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya goti lake la mguu wa kushoto ameondoka na kwenda kwao Ufaransa kwa lengo la kufanyiwa uchunguzi zaidi wa jeraha lake.

“Vipimo vya awali vinaonyesha Ahamada anaweza kukaa nje kwa zaidi ya miezi mitatu ila tunasubiria majibu yake ya mwisho tutakayoyapata kutoka Ufaransa ndipo ambapo tutaweza kuthibitisha ni muda gani atakosekana katika timu yetu,” amesema.

Kuumia kwa makipa hao tegemeo kunaifanya timu hiyo kubakiwa na kipa chaguo la tatu, Zuberi Foba ambaye naye amekuwa sio wa kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza jambo linalowafanya mabosi kuanza kutafuta mwingine atakayeziba nafasi zao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live