Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Idris Sultan aachiwa na Mahakama, akamatwa tena

Idris Pic Data Idris Sultan aachiwa na Mahakama, akamatwa tena

Mon, 17 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia, msanii wa vichekesho, Idris Sultani na Innocent Maiga, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani hapo tangu Februari mwaka huu.

Washtakiwa hao wameachiwa chini ya  kifungu cha 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai( CPA).

Hata hivyo, muda mfupi baada ya Idris na Maiga, kuachiwa na Mahakama,  alikamatwa tena na askari polisi waliokuwepo Mahakamani hapo na kupelekwa kituo cha Polisi cha Oysterbay.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili, likiwemo la kushindwa kufanya usajili wa laini ya simu ambayo ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine.

Uamuzi wa kuwaachia umetolewa jana, na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Akitoa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo, hakimu Chaungu alisema upande wa mashtaka hawana sababu ya msingi ya kutoleta shahidi, hata kama kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa Mei 14, 2021 ambayo ilikuwa sikukuu.

Hakimu Chaungu alisema, Februari 22, 2021, alitoa ahirisho la mwisho kwa kesi hiyo kutokana na upande wa mashtaka kutokuwa na shahidi.

" Pia, April 29, 2021, nilitoa tena ahirisho lingine baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuleta shahidi mahakamani hapa, sasa na leo pia upande wa mashtaka mmeshindwa kuleta tena shahidi mahakamani hapa" alisema Chaungu.

Alisema kutokana na mazingira hayo amefuta mashtaka dhidi ya washtakiwa na kuwaachia huru chini ya  kifungu cha 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai.

Awali, kabla ya kufutwa kwa kesi hiyo, wakili wa serikali Sylvia Mitanto aliieleza mahakama kuwa, kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutoa ushahidi kwa upande wa mashtaka, lakini wameshindwa kupata shahidi jana  kwakuwa kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa Mei 14 ambayo ilikuwa sikukuu hivyo aliomba wapangiwe tarehe nyingine.  

Hakimu Chaungu baada ya kusikiliza maelezo hayo, alitupilia mbali ombi hilo na kuwaachia washtakiwa. Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao, wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 78/2020.

Sultan na Maiga wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume cha sheria ya Mamlaka ya Mawasiliani nchini (TCRA).

Katika shtaka la kwanza, linalomkabili Sultani, inadaiwa kuwa kati ya Desemba mosi, 2019 na Mei 19, 2020 katika eneo la Mbezi Beach, alishindwa kufanya usajili wa laini ya simu ambayo ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine, kinyume cha sheria.

Inadaiwa kuwa Idris anadaiwa kutumia laini ya simu iliyokuwa inamilikiwa na Innocent Maiga bila kuripoti kwa mtoa leseni, ambaye ni TCRA.

Katika shtaka la pili, linalomkabili Maiga, inadaiwa siku na maeneo hayo, Maiga akiwa mmiliki halali wa laini hiyo, alishindwa kutoa taarifa  ya mabadiliko ya namba ya simu kama inatumiwana Idris Sultan, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz