Mwenendo usioridhisha wa Pan African ya Dar es Salaam katika Ligi ya Championship msimu huu, umegeuka shubiri kwa kocha Iddy Cheche ambaye amejikuta akionyeshwa mlango wa kuotea na uongozi wa timu hiyo.
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa Pan African umesema kuwa aliyekuwa msaidizi wa Cheche, Hemed Waziri ndiye atakaimu kwa muda nafasi hiyo.
"Tunapenda kuutaarifu umma wa wapenda soka, wanachama na wapenzi wa Pan African kuwa tumefikia makubaliano ya pande zote mbili kuvunja mkataba na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi chetu Iddy Cheche.
"Tunamshukuru kocha Cheche kwa kipindi ambacho alikuwa anaifundisha timu yetu na tunamtakia kila la kheri katika majukumu yake. Kikosi chetu kwa sasa kitakuwa chini ya kocha msaidizi Hemed Waziri wakati mchakato wa kumtafuta kocha mkuu ukiendelea," ilifafanua taarifa ya Pan African.
Timu hiyo inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ya Championship yenye timu 16, ikiwa na pointi tatu tu ilizokusanya katika michezo sita iliyocheza hadi sasa.
Pan African ilianza kwa kupata ushindi wa mabao 3-2 mbele ya Copco na baada ya hapo ikapoteza katika mechi tano mfululizo zilizofuata dhidi ya Pamba, Mbuni, TMA na Cosmopolitan.