Beki wa kati wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC anayeitumikia kwa mkopo Mtibwa Sugar Ibrahim Ame, amesema Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Mayele alimpa wakati mgumu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Jumatano (Februari 23), Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.
Ame ametoa kauli hiyo, baada ya Mshambuliaji huyo kuwa tishio kwenye sadfu ya Ulinzi ya Mtibwa Sugar, ambayo iliruhusu kufungwa mabao 2-0, huku Mayele akifunga bao la pili kwenye mchezo huo, akitanguliwa na Saido Ntibazonkiza.
Beki huyo ambaye alisajiliwa Msimbazi akitokea Coastal Union mwanzoni mwa msimu uliopita 2020/21, amesema alipewa jukumu la kumkaba Mayele ili asifunge, lakini alishindwa kufanya hivyo.
“Mayele ni mshambuliaji hatari na wa kuchungwa akiwa uwanjani kutokana na kiwango chake bora.”
“Nakumbuka kabla ya mchezo wetu huo, nilipewa jukumu la kutembea na Mayele kila sehemu kwa lengo la kutofunga, lakini ikashindikana na kupata upenyo akafunga.”
“Kwa kweli nilifanya jitihada nyingi za kutosha za kuhakikisha Mayele hafungi lakini nimeshindwa, alitumia nafasi moja aliyoipata kufunga, kiukweli siku yangu imeharibika baada ya bao hilo, sitaweza kupata usingizi,” amesema Ibrahim Ame.
Ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar umeifanya Young Africans kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 39, wakiiacha Simba SC inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama 8.