Kocha kutoka DR Congo Jean-Florent Ikwange Ibengé amepambanishwa tena na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kwenye michuano ya soka Barani Afrika.
Ibenge ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa kikosi cha RS Berkane ya Morocco, atakutana tena na Simba SC kwenye michuano ya Afrika, kufuatia klabu yake kupangwa kundi moja na wababe hao wa Msimbazi.
Kocha huyo amekua na bahati ya kupangwa na Simba SC na hii ni mara yake ya tatu kukutana na Mabingwa hao wa Tanzania Bara.
Mara mbili alikutana nao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika akiwa na AS Vita ya nchini kwao DR Congo na sasa atakutana nao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.
Pia mchezo huo utamuwezesha Kiungo kutoka Zambia Clatous Chama ‘Tripple C’ kurejea jijini Dar es salaam sanjari na Kiungo kutoka DR Congo Tuisila Kisinda ambao walisajiliwa RS Berkane mwanzoni mwa msimu huu.
Timu hizo zimepangwa kundi D lenye timu nyingine kama US Gendarmerie ya Nigeria na Asec Mimosa ya Ivory Coast.
Kundi A lina timu za Pyramids FC, CS Sfaxien, Zanaco FC na Ahli Tripoli huku Kundi B lina JS Kabylie/Royal Leopards, Orlando Pirates, JS Saoura na Al Ittihad SC.
Kundi C linawajumuisha Mabingwa mara tano wa Barani Afrika TP Mazembe kutoka DR Congo, Cotonsport FC ya Camereoon, Al Masry SC ya Misri na AS Otoho d’Oyo ya DR Congo.