Uongozi wa Klabu ya Al Hilal Omdurman ya Sudan umesisitiza kuendelea kufanya kazi na Kocha Mkuu kutoka nchini DR Congo Jean-Florent Ikwange Ibengé, licha ya kushindwa kutinga Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Al Hilal Omdurman ilishindwa kutinga Robo Fainali Jumamosi (April Mosi), kufuatia kufungwa na Al Ahly ya Misri mabao 3-0, na kujikuta ikimaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi B, kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Uongozi wa klabu hiyo umetoa msisitizo huo, kufuatia taarifa za awali kueleza kuwa Al Hilal Omdurman ilikua na mpango wa kumtimua Ibenge kama angeshindwa kufuzu Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tayari Azam FC ya Tanzania ilikuwa imeanza kuhusishwa na mpango wa kumpa ajira Kocha huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya DR Congo pamoja na Klabu ya AS Vita.
Msimu uliopita Ibenge alifanikiwa kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, akiwa na klabu ya RS Berkane ya Morocco akiifunga Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.