Manchester United kwa msimu huu inaonekana ni kama imeanza kurudi katika ramani ya soka tofauti na ilivyokuwa kwa msimu uliopita.
Msimu wa 2021-22 mambo yalionekana kuwa magumu kwa United ambayo ilishindwa kuonesha cheche zake ikiwa na staa wake Cristiano Ronaldo ambaye ni kama alijitahidi kuibeba timu kwa namna fulani.
Mambo hayakuwa mazuri, wachezaji wengi kama Marcus Rashford viwango vyao havikuwa kwenye ubora kabisa, safu ya ulinzi huko mambo nako yalikuwa hovyo kabisa wakiongozwa na nahodha, Harry Maguire.
Kwenye kiungo wakiwa na Bruno Fernandes, pia hapakuwa katika ubora wa hali ya juu japo kiungo huyo tangu ametua 2020 ndiye alionekana kubadilisha mambo kwa kiasi kikubwa kikosini hapo.
Msimu huu chini ya Kocha Erik ten Hag, Bruno amesalia kuwa mchezaji muhimu wa eneo la kiungo na ushambuliaji kutokana na kazi ambayo amekuwa akiifanya ndani ya kikosi hicho.
Bruno ameonekana kuwa imara tena msimu huu na kuwa msaada ndani ya Man United akiwa ni kati ya wachezaji ambao wametumika zaidi.
Kiungo huyo amefanya kazi kubwa na ametumika ndani ya kikosi hicho pamoja na kipa, David de Gea.
Bado Bruno ni imara kwani rekodi zake zimeendelea kuonekana wazi katika hilo msimu huu.
Mpaka sasa ni kati ya wachezaji ambao wamecheza mechi nyingi Ulaya, ndani ya Man United akiwa amecheza jumla ya mechi 53, kumbuka pia hivi karibuni alikuwa kwenye majukumu na timu ya Taifa ya Ureno.
Bruno katika mechi hizo 53, amefanikiwa kutoa mchango wa mabao 31. Amefunga mabao 15 katika michuano yote na asisti 16.
Lakini kiungo huyo katika michuano yote amefanikiwa kutengeneza nafasi 157 akiwa na timu hiyo.
Kumbuka kuwa rekodi hizi ni za Premier League, Kombe la FA, Carabao Cup na Europa League.
Bruno amefanikiwa kuwa mchezaji bora wa mechi mara 16 katika michuano yote msimu huu.
Zile nafasi muhimu ametengeneza mara 44 ikiwa pia ni rekodi bora kwa kiungo huyo wa Man United.
Wastani wake wa takolini kwa mechi ni 2.7 huku akiwa na dribo za uhakika kwa asilimia 80, kwa kiungo, hizi ni rekodi bora. Ameshinda mipira ya chini kwa asilimia 70.
Huyo ndiye Bruno Fernandes, mwamba wa Manchester United akiwa ameonesha ubora wake baada ya mechi 53, bado msimu unaendelea, kuna mengi zaidi tunatarajia kutoka kwake.