Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huyu ndiye De Zerbi unayemjua, unayemsikia

De Zerbii (19).jpeg Huyu ndiye De Zerbi unayemjua, unayemsikia

Sat, 28 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni miongoni mwa majina ya makocha ambayo yanatajwa sana pale England.

Na hivi karibuni ziliibuka tetesi zinazodai huenda akapata nafasi ya kwenda kuifundisha Real Madrid, klabu yenye historia kubwa duniani wakati kocha wa sasa, Carlo Ancelotti atakapoondoka mwishoni wa msimu huu. Naye si mwingine, ni Roberto de Zerbi.

De Zerbi ni raia wa Italia na katika nyakati tofauti kutokana na mavitu yake matata kabisa ya uwanjani, amekuwa akifananishwa na Pep Guardiola kutokana na staili ya uchezaji ya kikosi chake.

Ukitaka kulifahamu hilo, itazame Brighton inavyocheza. Ni gongagonga na wala haitegemei mchezaji mmoja mwenye jina kubwa, timu inacheza kimfumo.

Mwanaspoti litaangazia mavitu ya kocha huyo mwenye ufundi mkubwa alikoanzia na kile kinachofanya soka lake kuwa na mfumo mkubwa na kuanza kufikiriwa na klabu kubwa kama za Real Madrid na Manchester United ili akafanye mambo makubwa kwenye vikosi hivyo vya kibabe.

ALIPOANZIA

De Zerbi wakati anacheza soka, hakuwa na mafanikio makubwa sana. Kipindi hicho alikuwa akimudu vyema nafasi ya kiungo mshambuliaji, mtengenezaji na pengine ndio maana amekuwa na ufundi mkubwa.

Maisha yake ya uchezaji yalianzia kwenye timu za vijana za AC Milan ambapo alihudumu kwenye timu za vijana hadi alipopandishwa mwaka 1997 ambapo alikaa mwaka mmoja kisha akatolewa kwa mkopo kwenda Monza, Padova na Avellino kabla ya kuuzwa rasmi mwaka 2001 kwenda Salernitana.

Baada ya hapo alicheza timu mbalimbali ikiwa pamoja na Napoli ambayo alijiunga nayo ikiwa Ligi Daraja la Kwanza na timu aliyoichezea kwa muda mrefu zaidi ni Froga ya hukohuko Italia ambayo aliichezea mechi 60 na kufunga mabao 18.

Pia, aliwahi kuichezea Timu ya Taifa ya Italia lakini ile ya U-20 ambayo kwa mara ya kwanza aliitwa kikosini Desemba 1998 na akaichezea mechi nne na kufunga mabao mawili.

MAISHA YA

UKOCHA

Baada ya kustaafu kucheza soka akiwa na AC Trento ya Italia mwaka 2013 alienda kuwa kocha wa Darfo Boario inayoshiriki madaraja ya chini huko Italia, alihudumu hapo kuanzia mwaka 2013 hadi Juni, 2014 ambapo aliondoka na kutua Froggia ambayo aliifundisha kuanzia mwaka huo hadi 2016.

Ilipofika 2016, ndio rasmi alianza safari yake ya mafanikio kwani alipata nafasi ya kuifundisha Palermno iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu Italia (Serie A)

Alijiunga na timu hiyo akichukua nafasi ya Davide Ballar dini aliyejiuzulu. Maisha ya De Zerbi hayakuwa mazuri katika kikosi hiki.

Aliiongoza timu hii kwenye vichapo saba mfululizo ndani ya miezi mitatu ambapo hakupata alama hata moja. Alifukuzwa Novemba, 30, 2016 na nafasi yake ikachukuliwa na Eugenio Corini.

Oktoba, 2017 alichaguliwa kuwa kocha wa Benevento, hapa pia mambo yalikuwa magumu na mwisho wa msimu timu ilishuka daraja lakini mabosi walimbakisha kwa sababu ya staili nzuri ya uchezaji alioiingiza kwenye timu na pia alikuwa amewezesha kufanyika kwa biashara nyingi za usajili.

Ilipofika Juni, 2018 alitimkia zake Sassuolo ambapo alionekana kufanya vizuri, akimaliza nafasi ya nane mara mbili na msimu wake wa mwisho alishindwa kufuzu michuano ya Uefa Conference League kwa tofauti ya alama moja tu dhidi ya AS Roma.

Mei 2021, ilitangazwa kwamba De Zerbi alikuwa amepanga kuondoka kwenye kikosi hicho mwishoni mwa msimu.

Mara baada ya msimu kumalizika tu, alipata shavu la kuifundisha Shakhtar Donetsk na ilipofika Septemba, 2021 aliiongoza timu hiyo kushinda taji la Ukraine Super Cup kwenye mchezo waliocheza dhidi ya Dynamo Kyiv na akaweka rekodi yakuwa kocha wa kwanza raia wa Italia kuwahi kufanya hivyo. Aliondoka Donetsk, Juni 2022 wakati mapambano kati ya nchi hiyo na Urusi yamezuka.

Baada ya kuondoka hapo alikaa hadi Septemba, 2022 ambapo alichaguliwa kuinoa Brighton akichukua nafasi ya Gharam Potter aliyetimkia Chelsea.

Katika msimu wake wa kwanza Brighton ilimaliza nafasi ya sita na kufuzu kucheza michuano ya Europa League msimu huu. Lakini tangu atue kwenye kikosi hicho wachezaji wengi wameuzwa kama Moises Caicedo, Alexis Mac Allister na Robert Sanchez lakini bado timu imeendelea kufanya vizuri.

MFUMO

Jamaa ni muumini sana wa soka la kumiliki mpira muda mwingi wa mchezo na kufanya shinikizo (pressing), mara nyingi hupendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1.

Aina yake ya ufundishaji inafananishwa kwa kiasi kikubwa na ile ya Guardiola ingawa De Zerbi anasifika sana kwa kipaji chake cha kusajili wachezaji wa kawaida na kuwafanya kuwa bora na kumpa mafanikio makubwa ndani ya uwanja, huku timu pia ikipata faida kubwa kwa kuwauza na kujipatia pesa.

Akiwa Shakhtar alimuibua Mykhailo Mudryk ambaye kwa sasa yupo Chelsea baada ya kununuliwa kwa pesa nyingi.

Tangu kuanza kwa msimu huu Brighton inashika nafasi ya sita ikiwa imecheza mechi saba, ikishinda tano na kufungwa mbili huku kikosi chake kilishuhudia wachezaji wengi wakiondoka kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Mavitu yake ya uwanjani yanavutia timu nyingi kubwa ikiwamo Real Madrid inayomtaka akawe mrithi wa Ancelotti, lakini Man United wao wanafika mbali zaidi, wakifikiria kumchukua De Zerbi akawe mkurugenzi wao mpya wa soka huko Old Trafford, ikiwa ni mpango wa tajiri mpya, Sir Jim Ratcliffe.

Wapi atatua na nini atafanya? Ni suala la kusubiri tu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live