Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huyu ndiye Azizi Ki, mwamba wa Ouagadougou

Aziz Ki Azam Huyu ndiye Azizi Ki, mwamba wa Ouagadougou

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiwango cha Stephane Azizi Ki wa Yanga kimeitesa Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao imeshuhudiwa mvua ya mabao ikinyesha huku fundi huyo wa kimataifa wa Burkina Faso akifunga mabao matatu 'hat trick'.

Hat trick aliyofunga Azizi Ki imeifanya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 na kukwea hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 15 sawa na Simba huku wakibebwa na idadi kubwa ya mabao waliyonayo.

Azizi Ki alifungua akaunti yake ya mabao kwenye mchezo huo katika dakika ya nane huku Azam ikichomoa dakika ya 18 kupitia kwa winga, Sillah na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa na bao 1-1.

Dakika ya 62, Azam ilipata bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti uliofungwa na Prince Dube baada ya Sillah kufanyiwa madhambi kwenye eneo la hatari.

Azizi Ki aliisawazishia Yanga dakika ya 68 kwa faulo ambayo ilimshinda kipa wa Azam FC, Idrissu Abdulah, huku fundi huyo akipigilia msumari wa tatu na ushindi kwa Wananchi katika dakika ya 72.

Mbali na mabao aliyofunga Azizi Ki kwenye mchezo huo, alionekana kuipa Yanga uhai katika maeneo matatu tofautu ya ushambuliaji.

Fundi huyo alishambulia akitokea winga ya kulia na hata kushoto na kuna muda alicheza nyuma ya Clement Mzize hivyo hakuwa akizoeleka eneo moja.

Uwezo wake wa kupiga mashiti ulimfanya Idrissu kuwa macho muda mrefu kwani kila ambapo alikuwa katika nafasi nzuri alifanya majaribio kadhaa ya kumfunga.

Baada ya kupoteza mchezo huo Azam imeshuka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 13 baada ya mechi sita ikishinda nne, sare moja na kufungwa mmoja.

Kikosi cha Yanga kilichoanza ni; Djigui Diarra, Dickson Job, Joyce Lomalisa, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Clement Mzize, Azizi Ki na Pacoume Zouzoua.

Azam FC ni; Iddrissu Abdulah, Lusajo Mwaikenda, Cheikh Sidibe, Malickou Ndoye, Daniel Amoah, Sospreter Bajana, Gibril Sillah, James Akaminko, Prince Dube, Feisal Salum, Abdul Seleman.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: