Unapotaja majina ya nyota wanaofanya vizuri katika Ligi Kuu Bara kwa msimu huu, hutoacha kumtaja kiungo mshambuliaji wa Ihefu, Marouf Tchakei kutokana na kiwango bora anachoendelea kukionyesha licha ya kutozungumzwa sana na mashabiki.
Raia huyu wa Togo amekuwa mmoja wa mihimili mikubwa ndani ya timu hiyo tangu alipotua Januari mwaka huu katika dirisha dogo la usajili akitokea Singida Fountain Gate aliyojiunga nayo Julai mwaka jana baada ya kuondoka AS Vita Club ya DRC Congo.
Uwezo wake ulimfanya kumpoteza kabisa Mbrazili wa Singida, Bruno Gomes ambaye msimu uliopita alionyesha kiwango kizuri baada ya kufunga mabao 10 ya Ligi Kuu Bara na kuzivutia timu kubwa za Simba na Yanga zilizokuwa zinahitaji saini yake.
Tchakei hadi sasa tayari amefunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara ambapo matano kati ya hayo ameyafunga akiwa na kikosi cha Singida huku mawili akiyafunga na Ihefu ambayo ameyafunga mfululizo akianzia mechi dhidi ya Mtibwa Sugar na Geita Gold.
Licha ya wengi kumtambua vizuri akitokea Congo, nyota huyu alianza kuonyesha kiwango kizuri kipindi akiichezea klabu ya Gbikinti na ASKO Kara zote kutoka kwao Togo ambazo ndizo ziliwafanya mabosi wa AS Vita Club kuipigania saini yake.
MAKOCHA WATANO
Kuonyesha ubora wa nyota huyo tayari hadi sasa amefundishwa na makocha watano tofauti na wote wamekubali uwezo wake.
Wakati akiichezea Singida, alifundishwa na makocha wanne akianza Mholanzi, Hans Van de Pluijm aliyeonyesha pia kumuamini na hata alipoondoka Agosti 29, mwaka jana kisha kutua Mjerumani, Ernst Middendorp aliendelea kumtumia na hakumuangusha.
Mjerumani huyo alikabidhiwa mikoba hiyo Septemba Mosi mwaka jana ila hakudumu kwa muda mrefu akaondoka Septemba 19 na hata ujio wa kocha Mbrazili, Ricardo Ferreira ulimfanya Tchakei kuendelea kukiwasha kama kawaida.
Mzimu wa makocha kuondoka ndani ya kikosi hicho uliendelea kwani Desemba 28, mwaka jana Mbrazili huyo aliondoka na timu kukabidhiwa Thabo Senong, raia wa Afrika Kusini, ambaye pia alimuamini kikosini hadi alipoondoka katika dirisha dogo la Januari.
Alipojiunga na Ihefu akakutana na kocha, Mecky Maxime aliyejiunga na timu hiyo Desemba 27, mwaka jana baada ya kuondoka Kagera Sugar na licha ya ugeni wake ameendelea kumuamini kwenye kikosi cha kwanza na matunda yake yanaonekana wazi.
MFALME MPYA
Kwa misimu miwili mfululizo ndani ya kikosi cha Ihefu hakuna mchezaji aliyefikisha mabao saba ya Ligi Kuu Bara ila kwa upande wa Tchakei tayari ameandika ufalme huo wa kuyafikisha licha ya kuzichezea timu mbili tofauti msimu huu.
Msimu uliopita nyota aliyemaliza kinara katika kikosi cha Ihefu alikuwa ni Adam Adam ambaye alifunga mabao matano huku pia akichezea timu tofauti ambapo alianza kuichezea Mtibwa Sugar ya Morogoro kisha kutua jijini Mbeya na kufunga mawili.
Mbali na Adam Adam ambaye kwa sasa anaichezea Mashujaa ya mkoani Kigoma, nyota mwingine aliyefunga idadi kama hiyo msimu uliopita ni Rashid Juma aliyeanza kuichezea Ruvu Shooting aliyoifungia matatu huku kwa upande wa Ihefu akifunga mawili.
VITA YA UFUNGAJI
Mabao saba aliyonayo nyota huyu yanamfanya kukoleza vita ya ufungaji bora msimu huu hadi sasa kwani amebakisha matatu tu kumfikia kinara wa Ligi Kuu Bara, Stephane Aziz KI wa Yanga ambaye anaongoza akiwa amefunga mabao 10.
Nyota wengine ambao wako sawa na yeye ni Waziri Junior wa KMC mwenye saba na Prince Dube wa Azam huku waliomzidi mbali na Aziz KI ni Feisal Salum 'Fei Toto' (Azam FC) na Maxi Mpia Nzengeli anayeichezea Yanga ambao kila mmoja wao amefunga manane.
Katika mabao hayo ya nyota huyo ni timu moja tu aliyoifunga mawili ambayo ni Namungo wakati Singida iliposhinda mabao 3-2, Oktoba 21, mwaka jana kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi huku jingine likifungwa na kiungo Mkenya, Duke Abuya.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu kiwango chake, Tchakei anasema siri kubwa ni kujituma na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi.
"Sio mafanikio yangu pekee kwa sababu tunacheza kama timu hivyo naamini zaidi katika kufanya kazi kwa ushirikiano, jambo la kujivunia kwangu nacheza na wachezaji wenye umoja kitu ambacho kinarahisisha kutimiza majukumu yetu vizuri," anasema.
Wasifu:
Jina: Marouf Tchakei
Kuzaliwa: Des 15, 1995
Mahali: Bassar
Nchi: Togo
Urefu: Mita 1.73
Nafasi: Kiungo Mshambuliaji
Jezi: Namba 20
Klabu: Singida FG
Alikopita: Gbininti FC, ASKO Kara, AS Vita na Singida FG
07 Mabao aliyofunga hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara katika mechi 16.
28 Umri alionao kiungo huyo anayemudu kucheza pia kama winga
263 Dakika alizotumia Tchakei katika mechi nne za Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu akifunga mabao matatu.