Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huyu Phiri ni mtu na nusu

Phiri Robertinho Moses Phiri na Kocha Robertinho

Sat, 26 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni wakati wa straika wa Simba, Moses Phiri kujitetea baada ya mashabiki kumpambania, wakihoji kwa nini kocha wa timu hiyo, Oliveira Roberto ‘Robertinho’ hampangi kwenye kikosi.

Hilo lilikuja baada ya Kocha Robertinho kumuanzisha nahodha wa timu hiyo, John Bocco dhidi ya Yanga katika mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii, ambayo penalti ziliamua Simba kunyakua taji hilo.

Ingawa Phiri aliingia dakika za jioni na alikuwa kati ya wachezaji waliopiga penalti na kupaisha, lakini bado upendo wa mashabiki haukuondoka kwake.

Kocha alilifafanua hilo, kwamba anajaribu kumtumia kila mchezaji na anaona kwa sasa Phiri ameanza kurejea kwenye makali yake, akisisitiza anaitengeza timu ambayo itakuwa hatari siku za usoni.

“Naitengeneza timu, mfano mzuri unaona kina Phiri, Baleke (Jean) wameanza kufunga, siwezi kuacha kumtumia mchezaji ambaye anakuwa kwenye kiwango cha kuisaidia timu,” anasema.

Aliyekuwa kipa wa Simba, Beno Kakolanya anazungumzia umahiri wa Phiri wa kucheka na nyavu akisema msimu huu akiwa fiti na kupata nafasi ya kucheza anaweza kufanya makubwa.

“Jamaa umakini wake unaanzia mazoezini, naamini akipata nafasi, anaweza akafanya makubwa sana msimu huu, msimu uliopita majeraha ndio yalimharibia, binafsi namuona ni straika hatari,” anasema.

Mwanaspoti linakuchambulia kibarua alichonacho Phiri, baada ya mashabiki kumtetea kwa kupaza sauti wakijua kipi kinamuweka benchi na sasa kocha anamtumia.

KAANZA KUTUPIA

Phiri amefungua akaunti ya mabao kwenye Ligi Kuu baada ya kutupia moja dhidi ya Dodoma Jiji, Simba ikishinda 2-0 na alisema jambo hilo limempa morali ya kuhakikisha hawaangushi mashabiki ambao wamemuonyesha upendo mkubwa, wakitamani acheze.

“Nawapenda mashabiki wa Simba, kwanza niwahakikishie bado nipo, naheshimu mkataba wangu, nimefurahia kufunga bao, nitapambana ili kuwaonyesha kile wanachokitaka kutoka kwangu, hivyo kazi yangu ni moja kufunga,” anasema.

Ndani ya kikosi cha Simba, Baleke ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mawili, akifunga dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji, kitu kinachomfanya Phiri aone hakuna kulala katika kushindania namba.

“Ushindani ni mzuri, unafanya kila mchezaji aiheshimu nafasi anayopewa na kocha kucheza, kikubwa nipo fiti, kuhusu kupangwa kocha ndiye anajua aanze nani na nani akae benchi,” anasema.

Mastaa wengine waliofunga ndani ya kikosi hicho ni Clatous Chama, Willy Essomba Onana na Fabrice Ngoma waliofunga dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Simba ikishinda mabao 4-2.

PHIRI WA MSIMU ULIOPITA

Endapo Phiri akicheza kwenye kiwango alichokionyesha msimu uliopita, hatii shaka kuwapa raha mashabiki wake, kwani alikuwa mchezaji muhimu akiifungia Simba jumla ya mabao 15 katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF).

CAF MABAO 5, ASISTI 2

Licha ya ugeni kwenye Ligi Kuu Bara na kutumia muda mrefu akiwa majeruhi, Phiri alifunga mabao 10 katika ligi na mengine matano katika mechi 10 za Ligi ya Mabingwa Afrika alizocheza ambako pia alitoa asisti mbili.

Raundi ya kwanza dhidi ya Big Bullet ya Malawi Septemba 10, 2022, alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0, mchezo wa ugenini na marudiano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa (Septemba 18) alifunga katika ushindi wa mabao 2-0.

Mchezo wa raundi ya pili dhidi ya C.D Primeiro de Agosto ya Angola, uliopigwa ugenini Oktoba 9, Phiri alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 3-1 na mchezo wa marudiano uliopigwa Oktoba 16 Benjamin Mkapa, Phiri alifunga bao 1-0.

Hatua ya makundi Phiri alihusika na pasi za mwisho za mabao dhidi ya Vipers ya Uganda, Simba ikishinda jumla ya mabao 2-0 nyumbani na ugenini.

Kwa jicho la kiufundi la kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Boniface Pawasa, anaona Kocha wa Simba, Robertinho bado hajapata kikosi cha kwanza, hivyo anaona Phiri na safu yote ya mbele ina kazi ya kupambana kupata nafasi ya kucheza.

“Simba ina kikosi kizuri sana, huenda ikawa timu ambayo itatisha zaidi na kufunga mabao mengi, ninachoona ni kocha kujua jinsi ya kumtumia kila mchezaji kwa faida ya timu, nina imani Phiri atafanya vizuri,” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti