Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huyu Moloko atasumbua sana

Moloko Jesus Moloko

Wed, 31 Aug 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ingawa bado ni mapema kuzungumzia kiwango anachokionyesha winga wa Yanga, Jesus Moloko msimu huu, ila ameonekana na mabadiliko tofauti na msimu uliopita.

Msimu ulioisha wakati Yanga ilipomsajili mchezaji huyo kutoka AS Vita ya DR Congo kwa mkataba wa miaka miwili, mashabiki walitarajia angeziba au kuonyesha zaidi kile ambacho kilifanywa na Tuisila Kisinda ambaye aliuzwa Berkane ya Morocco, lakini mambo yakaenda ndivyo sivyo.

Baadaye ikadaiwa kwamba alikuwa kati ya mastaa wa kigeni ambao walitajwa kukatwa kikosini mara kwa mara, hivyo kusalia kwake na kusajiliwa kwa Bernard Morrison kwenye nafasi yake ni kama aliamshwa kupigania kubaki ndani ya timu hiyo.

Katika mechi mbili za Ligi Kuu ambazo Yanga, imecheza Moloko ameonyesha kiwango cha juu ambacho kimewafurahisha mashabiki pamoja na mastaa wa zamani ambao wametoa mitazamo dhidi yake.

Straika wa zamani wa timu hiyo, Edibily Lunyamila alisema Moloko ana kasi, mikimbio mizuri na anayewafanya mabeki muda wote wawe na kazi ya kumzuia na anachotakiwa kufanyia kazi ni umaliziaji wa pasi za mwisho.

Lunyamila alimtabiria Moloko kwamba endapo hatapata majeraha za mara kwa mara msimu huu utakuwa mzuri zaidi kwake kuliko uliopita kutokana na kile alichoonyesha kwenye mechi alizocheza.

“Mfano mechi ya Yanga na Simba kuingia kwa Morrison na Moloko ndio waliobadilisha mchezo. Unaona namna gani ameamka na kufanya kinachotakiwa,” alisema mkongwe huyo.

“Nadhani kilichombadilisha Moloko ni ushindani wa namba. Kama mchezaji wa kigeni lazima achangamke kuonyesha utofauti wake. Nasisitiza kwa msimu huu asipopata majeraha atakuwa kati ya wachezaji ambao watang’ara zaidi.”

Beki wa zamani wa Simba na Yanga, Amiri Maftah alisema timu ikiwa na wachezaji wengi wazuri kwenye nafasi moja, lazima kila mmoja atajituma ili aaminiwe na kocha.

“Kitendo cha Morrison anayecheza nafasi ya Moloko kutua Yanga lazima kitamchangamsha mchezaji huyo kutetea ugali wake. Ila yote katika yote kauanza msimu huu vizuri na kama akiendelea hivyo atafanya makubwa,” alisema.

Mechi dhidi ya Coastal Union, Yanga ikishinda mabao 2-0 Moloko ndiye aliyetoa asisti ya bao alilofunga Morrison kabla ya kuumia na kutolewa nje.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz