Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huyu Charles Ahoua taratibu mtamuelewa!

Ahoua Jean Charles Iii Huyu Charles Ahoua taratibu mtamuelewa!

Thu, 29 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo Mshambuliaji wa Simba, Charles Ahoua ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa msimu huu usajili wake ukivuma sana hata kabla hajacheza.

MVP huyo wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, ametua Simba akitokea klabu ya Stella akipewa mkataba wa miaka miwili na kutambulishwa kama ndiye mrithi wa Chama aliyetua Yanga baada ya kumaliza mkataba aliokuwa nao na Wekundu wa Msimbazi.

Usajili huo ulikuwa gumzo kwa mashabiki wa Simba wakiamini nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 ndiye atakayeenda kumaliza utata wote wa shimo aliloliacha Chama aliyeitumikia timu hiyo kwa miaka sita tangu ilipomsajili akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia na kuandika rekodi mbalimbali za kusisimua Msimbazi.

Ahoua alikuwa MVP wa tatu mfululizo kutoka Ivory Coast kutua nchini baada ya Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua wanaokipiga Yanga.

MVP huyo wa Ligi Kuu ya Ivory Coast alitua Simba akitokea klabu ya Stella akipewa mkataba wa miaka miwili.

TARATIBU ANAZOEA

Simba imefanya marekebisho karibu kila eneo msimu huu ikiongeza wachezaji 14 akiwemo Ahoua kwenye dirisha hili la usajili.

Ndio msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu tena akicheza mechi nne za mashindano akionekana kuwa na muendelezo wa kiwango chake.

Hata hivyo ni mara chache kwa mchezaji aliyetoka Ligi moja kwenda nyingine kukiwasha kama ilivyo kuwa awali kwa kuwa atahitaji muda wa kuzoea mazingira.

Alianza kuonekana kwenye mechi mbili za ngao ya jamii kati ya Yanga na Coastal Union kila mmoja akitoa maoni yake wengine wakisema ni kama mchoyo wa pasi hivi.

Baada ya mechi hizo mbili ni kama kiungo huyo ameanza kubadilika kwenye mechi mbili za ligi ambazo Simba imecheza hadi sasa dhidi ya Tabora United na Fountain Gate FC.

Katika mechi dhidi ya Tabora United pasi nyingi ambazo zilikuwa zikipigwa katika eneo la kiungo, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua na Joshua Mutala walishindwa kuwa na uamuzi sahihi wa kuziunganisha na kuwafanya wapoteze nafasi  nyingi.

Mechi mbili tayari amefunga bao moja na kutoa assisti tatu za mabao.

PRESHA YA CHAMA

Baada ya kuondoka kwa kiungo mshambuliaji, Clatous Chama ambaye alidumu Simba kwa misimu mitano akifanikiwa kukusanya mataji mbalimbali ya Ligi, FA na kucheza michuano ya kimataifa.

Simba ilimsajili Ahoua na matarajio makubwa  kwa klabu hiyo ni kuja kuwa mbadala wa Chama aliyekuwa muhimu kwenye kikosi hicho.

Kiungo huyo anakumbana na presha kubwa ya kuziba pengo la Chama lakini akitulia na kuachana na maneno ya nje ya uwanja atakuwa bora.

REKODI ZA ALIPOTOKA

Msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, Ahoua alimaliza kama Mchezaji Bora (MVP) wa msimu na pia klabu aliyokuwa akiichezea, huku akiifungia mabao 12 na kuasisti tisa akimfunika rekodi alizomaliza nazo Chama ndani ya Simba, kwani Mwamba wa Lusaka alifunga mabao saba na kuasisti saba tu msimu mzima.

Ahoua ni mchezaji anayeweza kumiliki mipira na kuwa sio rahisi kumnyang'anya anapokuwa nao na ana uwezo wa kutumia miguu yote miwili, japo wa kulia ndio una balaa zaidi.

Alipotoa Ivory Coast alisifika kwa kupiga mashuti ya mbali ambalo moja lilishihudiwa kwenye mechi ya juzi dhidi ya Fountain alipoukwamisha mpira nyavuni na kujiandikia bao lake la kwanza akiwa na Simba.

Licha ya rekodi hizo za nyuma lakini mchezaji huyo atakuwa na kazi ya ziada ya kuisadia Simba kiasi ambacho hata akikosekana timu isiwe na maajabu eneo lake.

KAZI ALIYONAYO

Baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi msimu uliopita, Simba ilikata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ilianza kutimua vumbi wiki iliyopita.

Simba imepoteza makombe ya Ligi Kuu, Kombe la FA na kuishia robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa takribani misimu mitatu sasa na msimu huu imesajili ikihitaji kurudisha ufalme wake.

Miongoni mwa wachezaji wanaotazamwa kuleta mapinduzi msimu huu ni Ahoua hivyo atakuwa na ziada ya kuwashawishi viongozi na mashabiki kuwa ni MVP kwelikweli.

Hata hivyo Ahoua hana maajabu katika michuano ya CAF lakini Simba inaweza kuwa mlango wake wa kutimiza yote hayo kama atakuwa tayari kupambania namba na kufanya vyema, kwani Simba inaanza na Kombe la Shirikisho baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga na Azam FC.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live