Ghafla tu kutoka kusikojulikana, Manchester City imeingia kwenye mchakato wa kutaka kumsajili kiungo Declan Rice wakati Arsenal ikionyesha dhamira ya dhati kabisa ya kunasa saini ya mchezaji huyo baada ya kupeleka ofa mbili tofauti huko West Ham United.
Wanachotaka kufanya Man City ni kubadili mawazo ya mchezaji kwa maana ya kuifanyia umafia Arsenal ili Rice achague kwenda Etihad kwa sababu hata ofa waliyoweka mezani ni kubwa kuliko ya wababe wa Emirates.
Hata hivyo, ishu ya kufanyiana umafia kwenye soka katika kipindi cha usajili si cha ajabu kutokana na kutokea kesi kibao za namna hiyo na kugeuka kuwa kawaida tu kwa timu kufanyiana umafia wa kunyang'anyana mastaa.
Jorginho - Napoli kwenda Man City - akanaswa na Chelsea (2018)
Arsenal bado ina matumaini ya kumnasa kiungo Rice licha ya kwamba Man City wanataka kuingilia dili lao. Lakini, jambo hilo linaweza kuwakuta lililowakuta Man City wakati walipokubaliana kila kitu na kiungo wa Napoli kwa wakati huo, Jorginho. Ilipotokea ishu ya kocha wa Napoli, Maurizio Sarri, kunaswa na Chelsea, basi jambo hilo lilikuwa rahisi kuvamia mawindo ya Man City na kwenda kumchukua Jorginho akakipige Stamford Bridge.
Cody Gakpo - PSV kwenda Man United - akanaswa na Liverpool (2023)
Kwa muda mrefu, staa wa Uholanzi, Cody Gakpo alikuwa akihusishwa na Manchester United na ilionekana angenaswa kwenye dirisha la Januari mwaka huu.
Lakini, kutoka kusikojulikana, Liverpool iliingilia dili hilo na kwa haraka sana walimnasa supastaa huyo kutoka PSV na kumwaacha kocha wa Man United, Erik ten Hag aking'aza tu macho kwa kukosa huduma ya mchezaji ambaye alitamani sana akacheze kwenye kikosi chake Old Trafford.
Mykhaylo Mudryk - Shakhtar Donetsk kwenda Arsenal - akanaswa na Chelsea (2023)
Umafia mwingine uliofanyiana mahasimu wa London, Arsenal na Chelsea. Kilichotokea, kwenye dirisha la Januari mwaka huu, Arsenal walikuwa na nafasi kubwa ya kumsajili winga Mykhalo Mudryk na kila kitu kilionekana kuwa sawa.
Lakini, Chelsea ghafla tu kupitia kwa mmiliki wao bilionea, Todd Boehly alikwenda kunasa saini ya mkali huyo kutoka Shakhtar Donetsk na hivyo kwenda kukipiga Stamford Bridge badala ya Emirates.
Fred - Shakhtar Donetsk kwenda Man City - akanaswa na Man United (2018)
Tukio jingine la umafia kwenye usajili alilofanyiwa Manchester City. Mwaka 2018, wakiwa na uhakika wa kumsajili kiungo wa Kibrazili, Fred kutokea Shakhtar Donetsk.
Ghafla tu mahasimu wao, Manchester United wakaibuka na kutoa ofa ya kulipa Pauni 50 milioni kunasa saini ya mchezaji huyo kitu ambacho kilikubalika na klabu ya Shakhtar na kumfanya staa huyo kwenda kukipiga Old Trafford badala ya kwenda Etihad.
Luis Diaz - Porto kwenda Tottenham - akanaswa Liverpool (2022)
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp anajua namna ya kuwakomesha wapinzani wake. Liverpool ilimwona staa Luis Diaz na kutaka kumsajili kwenye dirisha la majira ya kiangazi.
Lakini, baada ya kuona Tottenham imewafuata FC Porto na kutaka kumnasa kwenye dirisha la Januari na kuona wapo kwenye nafasi nzuri ya kuchukua saini yake, Liverpool wakaingia haraka na kwenda kumchukua staa huyo kumshusha huko Anfield.
Arjen Robben - PSV kwenda Man United - akanaswa na Chelsea (2004)
Bilionea Roman Abramovich alianza kuonyesha ubabe wake wa matumizi ya pesa baada ya kuimiliki Chelsea kwa kumsajili winga wa Kidachi, Arjen Robben.
Kwa muda mrefu, Manchester United chini ya kocha Sir Alex Ferguson ilikuwa ikimfukuzia Robben na mambo yalionekana kuwa vizuri kwamba staa huyo alikuwa anakwenda Old Trafford. Lakini, ghafla tu The Blues waliingilia kati dili hilo na kufanya umafia kwa kumasa Robben mbele ya Man United.
Ronaldinho - PSG kwenda Man United - akanaswa na Barcelona (2003)
Amini usiamini, Ronaldinho alikaribia kabisa kujiunga na Manchester United mwaka 2003, lakini kosa moja tu liliwafanya wapoteza nafasi ya kunasa huduma ya fundi huyo wa mpira kutoka Brazil.
Man United ilimhitaji Ronaldinho akarithi mikoba ya David Beckham, ambaye alinaswa na Real Madrid. Lakini, Barcelona wao baada ya kuona wamezidiwa na Madrid kwenye saini ya Beckham wakaamua kwenda kumsajili Ronaldinho.
Cristiano Ronaldo - Juventus kwenda Man City - akanaswa na Man United (2021)
Wakati Juventus ilipopanga kuachana na Cristiano Ronaldo kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka 2021 kila kitu kilionekana supastaa huyo wa Ureno anakwenda kujiunga na Manchester City.
Jambo hilo liliwashtua kuona staa wao wa zamani kwenda kujiunga na mahasimu wao Man City, hivyo wao wakaamua kuingilia kati na kwenda kunasa saini ya mchezaji huyo wakikatisha safari yake ya Etihad iwe ya Old Trafford.
Alexis Sanchez - Arsenal kwenda Man City - akanaswa na Man United (2018)
Licha ya Manchester City kuifunika Manchester United kwa mafanikio ya uwanjani kwa miaka ya karibuni, lakini linapokuja suala la usajili, wababe wa Old Trafford wamekuwa hatari zaidi kuliko wapinzani wao hao wa Etihad. Mwaka 2018, Man City ilikuwa kwenye nafasi nzuri ya kumsajili Alexis Sanchez kutoka Arsenal kabla ya Man United chini ya Jose Mourinho kuingilia kati na kumvuta staa huyo wa Chile huko Old Trafford.
Robinho - Real Madrid kwenda Chelsea - akanaswa na Man City (2008)
Dili hili limekuwa maarufu kwa kuwa lilifanyika kwenye siku ya mwisho kabisa ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Chelsea ilikuwa imeshafikia makubaliano binafsi na mshambuliaji huyo wa Kibrazili, Robinho kabla ya Manchester City kuingilia dili hilo na kumzidi ujanja bilionea Roman Abramovich wa Chelsea, akikosa saini ya mchezaji huyo wa kimataifa wa zamani wa Brazil kwenda kukipiga huko Etihad badala ya Stamford Bridge.
Emmanuel Petit - Monaco kwenda Tottenham - akanaswa na Arsenal (1997)
Emmanuel Petit aliwasili London kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Tottenham, alizungumza na mwenyekiti Alan Sugar kwa kipindi hicho kabla ya kuchukua taksi iliyokodiwa na Spurs. Arsene Wenger - ambaye alimnoa Petit walipokuwa Monaco - alisikia kuhusu uhamisho huo, hivyo akampigia simu na kumwambia asisaini.
Petit akamwomba Sugar wasogeze mbele kidogo na kuondoka, akitumia taksi ya Spurs kwenda kusaini Arsenal.
John Obi Mikel - Lyn kwenda Man United - akanaswa na Chelsea (2006)
Wakati anatimiza umri wa miaka 18, Manchester United ilitangaza kufikia makubaliano ya kumsajili kiungo Obi Mikel, Aprili 2005 kwa ajili ya dili litakaloanza Januari 2006. Chelsea naye ikadai imefikia makubaliano ya kumsajili staa na kudai kwamba wameporwa mchezaji na maofisa wa Old Trafford. Na Chelsea ilikubali kulipa fidia Man United na mchezaji huyo alisajili kwenda kukipiga Stamford Bridge.
Willian - Anzhi Mackhachkala kwenda Tottenham - akanaswa na Chelsea (2013)
Hii ilikuwa kali zaidi. Awali, Liverpool walikuwa mstari wa mbele kwenye mbio za kumsajili Willian kabla ya Tottenham kuingilia kati.
Spurs walionekana kuelekea kunasa saini ya mchezaji huyo kwa sababu ilishamfanyisha hadi vipimo vya afya kabla ya bilionea Roman Abramovich kuingilia kati tena na kumnasa mchezaji huyo kwenda kusaini kukipiga Chelsea. Mabosi wa Spurs wakiongozwa na Daniel Levy walikuwa wanamsubiri Willian aje kusaini.