Kiungo wa zamani wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na Simba, Abdulhalim Humud amesema hajawahi kukata tamaa katika maisha yake ya soka na anaendelea kupambana kuhakikisha kiwango chake kinazidi kuwa bora.
Akizungumza nasi, kiungo huyo anayekipiga Fountain Gate FC inayoshiriki Championship alisema katika maisha yake hajawahi kukata tamaa na mambo mazuri zaidi yanakuja kutoka kwake.
“Sijawahi kukata tamaa, nacheza popote, kikubwa tusubiri msimu umalizike tutajua naenda wapi,” alisema na kuongeza anayafurahia maisha ya Championship kwani kuna ushindani wa kweli na kila mechi ni fainali.
“Naomba nikuambie, maisha ni popote na huku ndio naenjoy zaidi, hata vijana wanaotaka kucheza waje wacheze huku watajifunza vitu vingi, huku lazima uwe fiti ili uweze kucheza,” alisema.
Humud alisema amecheza soka kwa muda mrefu na kugundua Championship ni ngumu kuliko Ligi Kuu.
“Championship kuna ugumu kucheza, tena sio kidogo.Tumepambana na Fountain Gate umeona ndio tumeishia hapa,” alisema.
Hata hivyo, amewataka wachezaji wenye ndoto za kufanikiwa kutokukata tamaa na badala yake kuendelea kuzitafuta fursa mbalimbali kupitia soka.
“Cheza popote hata huku Championship poa hakujifichi na kipaji siku zote hakijifichi,” alisema.
Kiungo huyo ambaye humudu kucheza namba sita, nane na 10 amewahi kupita pia timu za Coastal Union ya jijini Tanga, Majimaji ya Songea, Ashanti, Mtibwa, Azam na Sofapaka ya nchini Kenya.