Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hukumu ya Polisi Tz Ligi Kuu mbele ya Singida leo

Polisi Tanzania Hali Tete.jpeg Polisi Tanzania FC

Fri, 7 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tumaini pekee la kuhakikisha inasalia Ligi Kuu msimu huu Polisi Tanzania ni alama tatu leo Uwanja wa Liti itakapovaana na Singida Big Stars huku kocha wa Singida akichimba mkwara.

Polisi Tanzania ikifanikiwa kushinda itafikisha alama 22 na kuishusha Ruvu Shooting itakayocheza keshokutwa dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mchezo huo ni mgumu kwa Polisi sababu Singida inahitaji kujiimarisha zaidi katika nafasi ya tatu ambayo itamfanya msimu ujao ishiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata kama Singida itapoteza mchezo huo bado inauhakika wa kumaliza msimu ikiwa ndani ya 'top four' sababu hakuna timu inayoweza kuziondoa timu nne za juu.

Tayari timu nne za juu kwenye msimamo zimejulikana sababu Geita inayoshika nafasi ya tano kwa alama 34 hata kama itashinda michezo yote minne iliyosalia itafikisha alama 46 wakati Azam inayoshika nafasi ya nne ina alama 47.

Polisi Tanzania iliyopanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2020/21 sambamba na Namungo imekuwa kwenye wakati mgumu tangu mwanzo wa msimu jambo lililofanya uongozi kumtimua aliyekuwa kocha mkuu, Joslin Sharif.

Sharif alichukua mikoba ya Malale Hamsini ambaye baada ya msimu uliopita kumalizika alitimkia JKT Tanzania ambayo inaongoza Ligi ya Championship na ipo kwenye nafasi kubwa ya kupanda daraja kwenda Ligi Kuu.

Afisa Habari wa Polisi Tanzania, Frank Lukwaro alisema umekuwa msimu mgumu kwao licha ya mabadiliko yaliyofanywa lakini bado mambo yamekuwa bado. "Tunajua hali tunayopita sasa imekuwa changamoto sio kwa uongozi bali hata wapenzi wetu wamekuwa wakiona mwenendo ambao haufurahishi kwao.

"Kila jambo linakuwa na muda wake tunaimani mambo yatatulia na kwenda vyema sababu mipango inaendelea kuhakikisha timu inaimarika," alisema Lukwaro. Aliongeza baada ya mchezo wa leo dhidi ya Singida timu itarejea nyumbani kwa ajili ya michezo ijayo ambayo watakuwa Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Wakati huohuo Kocha wa SBS, Hans Pluijm alisema anahitaji ushindi kila mechi, kiufundi hauchukulii mchezo huo kirahisi, anatambua Polisi Tanzania ina kocha mzuri (Mwinyi Zahera) na inapambana isishuke daraja.

"Kila timu ina mipango yake, hivyo kila mechi kwetu ni muhimu kushinda, tunacheza na Polisi Tanzania inayojiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja, jambo litakaloongeza ushindani wa mchezo huo," alisema.

Kwa upande wa kocha wa Azam, Kally Ongala ambaye timu yake itavaana na Mtibwa Sugra alisema "Mchezo wa mwisho mechi ya ASFC tuliifunga Mtibwa Sugar mabao 2-0, tulicheza dakika 70, tukiwa pungufu Daniel Amouh alimchezea rafu Charles Ilanya, ila wachezaji walipambana sana, nataka waendeleze hali ya upambanaji ili tushinde mechi ya kesho(leo)."

Alisema kikosi chake kilikuwa na uzito wa uharaka wa maamuzi, hilo amelifanyia kazi kwenye mechi za kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar na KMC, wakati wa mapumziko ya ligi.

Naye kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Awadhi Juma hajakaa kinyonge alisema mchezo wa kesho wanahitaji uwatoe nafasi moja kwenda nyingine "Hatutaki uteja na Azam ambao walitutoa kwenye michuano ya ASFC, utakuwa mchezo mgumu tunahitaji pointi tatu."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live