Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huku nako kuna balaa zito

Yanga Algeria Tiziiiiii Huku nako kuna balaa zito

Fri, 24 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ladha ya michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu imerejea. Tanzania kwa sasa inawakilishwa na timu mbili, Simba na Yanga ambapo zote zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya muda mrefu sana kupita, hatimaye msimu huu Tanzania itawakilishwa na timu mbili kwa mpigo katika hatua hiyo na nzuri zaidi, ni timu pendwa zilizojaa utani wa jadi hivyo mji lazima utachangamka.

Simba imepangwa kundi B sambamba na timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast, Jwaneng Galaxy ya Botswana, na Wydad AC ya Morocco huku Yanga ambao ni vinara wa Ligi Kuu hadi sasa ikiwa imepangwa katika kundi D pamoja na vigogo Al Ahly ya Misri, CR Belouizdad ya Algeria na Medeama ya Ghana.

Hayo ni makundi ya moto. Kiufupi kila timu itavuna ilichopanda na timu mbili kwenye kila kundi zitatinga hatua ya robo fainali huku mbili zitakazochemsha zitakuwa zimeaga rasmi mashindano ya CAF kwa msimu huu.

Ukiachana na makundi hayo yenye timu pendwa za Kariakoo, kuna makundi mengine mawili ambayo moto wake ni wa kuotea mbali pia. Kundi A na kundi C, na Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea uchambuzi wa makundi hayo.

KUNDI A

Kuna hili Kundi A, lenye timu za Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Pyramids ya Misri, TP Mazembe ya DR Congo na FC Nouadhibou ya Mauritania.

Hakuna mwenye shaka juu ya ubora wa Mamelodi kwa msimu huu. Tayari imetwaa ubingwa wa African Football League ikiziondoa Petro de Luanda ya Angola na Al Ahly ya Misri katika hatua za awali kabla ya kuichapa Wydad AC kwenye fainali kwa jumla ya mabao 3-2, na kubeba kombe hilo jipya ikijiwekea rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutwaa taji hilo.

Hilo pekee linatosha kuzungumzia ubora wa Mamelodi ambayo imekuwa bora kwa miaka ya hivi karibuni na msimu uliopita iliishia nusu fainali ya michuano hii. Mamelodi ilitinga makundi kwa kuifunga Bamamuru ya Burundi jumla ya mabao 6-0, katika mechi mbili za mtoano.

Kwa upande wa FC Nouadhibou ya Mauritania, watu wengi hawaijui lakini ni timu nzuri iliyoanzishwa mwaka 1999 na kuwa na muendelezo mzuri.

Hawa ndio mabingwa wa Mauritania msimu uliopita ikiwa imetwaa taji hilo mara sita mfululizo na pia mara 11 kwenye historia kiujumla.

Mwaka 2003 na 2014 ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na mara zote iliishia hatua za awali na kuamua kuzama chimbo kujitafuta ambapo sasa imerudi ikiwa ya moto. Tusubiri kuona italeta maajabu gani. Nouadhibou ilifika hatua ya makundi baada ya kuiondosha Real Bamako ya Mali kwa jumla ya mabao 4-1.

Pia kuna Pyramids, kati ya timu tajiri Afrika ikishika namba tatu nyuma ya Ahly, Mamelodi na Zamalek na msimu huu imepangwa katika kundi hili.

Pyramids ilimaliza nafasi ya pili msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Misri na pia msimu wa 2019/2020 ilifanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ikifika hadi fainali. Ushindi wa jumla wa mabao 6-1 ilioupata Pyramids dhidi ya APR ya Rwanda ndio uliifanya kukata tiketi ya kuingia makundi msimu huu.

Timu nyingine inayokamilisha kundi hili ni TP Mazembe ambayo msimu huu imejitafuta na kujipata na sasa watu wanasubiri kuona imerejea kwa kasi gani.

Mazembe ni kati ya timu zilizobeba mara nyingi zaidi taji la Ligi ya Mabingwa Afrika ikilichukua mara tano, mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2015. Pia imebeba Kombe la Shirikisho CAF mara mbili mwaka 2016 na 2017 jambo linaloifanya kunogesha kundi hili A. Mazembe iliingia makundi baada ya kuifunga Nyassa Big Bullets ya Malawi kwa jumla ya mabao 5-0, kwenye mtoano.

KUND C

Hili ni kundi ambalo linachukuliwa poa lakini linaweza kushangaza wengi kutokana na timu zilizopo, zilivyojipanga na ushindani zitakaotoa.

Al Hilal ya Sudan baada ya kupotea kwa muda kwenye mashindano haya makubwa, msimu huu imerejea kwa kishindo na imekuwa na muendelezo bora chini ya kocha maarufu Florent Ibenge anayeisuka kibabe. Hilal msimu huu imetinga makundi kwa kuiondoisha Premiero de Agosto kwa jumla ya mabao 2-1.

Timu nyingine kwenye kundi hili ni mabingwa mara nne wa michuano hii, Esparance Sportive de Tunis kutoka Tunisia ikiwa kati ya timu shindani Afrika.

Msimu uliopita ilimaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya nchini kwao lakini pia ikaishia nusu fainali kwenye michuano hii jambo linaloifanya msimu huu kuwa na uchu zaidi wa kubeba taji hili.

Esparance imetinga makundi kwa kuiondoa AS Douanes ya Burkina Faso kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0.

Wababe wengine kwenye kundi hili ni Etoile Sportive du Sahel, mabingwa wa Ligi Kuu ya Tunisia kwa msimu uliopita na mabingwa mara moja wa michuano hii baada ya kubeba kombe mwaka 2007.

Msimu huu wamepania kurejesha utawala wao kwenye soka la Afrika na walifika hatua hii ya makundi baada ya kuifunga jumla ya mabao 3-1, AS Far ya Morocco inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi.

Timu inayokamilisha kundi hili ni Atletico Petroleos de Luanda ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Angola.

Hawa pia hawako kinyonge kwani msimu wa 2021-2022 walifika nusu fainali ya michuano hii lakini pia wamekuwa wakishiriki mara kwa mara michuano ya CAF.

Chanzo: Mwanaspoti