Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huku Ronaldo, kule Suarez

Ron Suarez Huku Ronaldo, kule Suarez

Mon, 28 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Tunaendelea kuinjoi utamu wa fainali za Kombe la Dunia na sasa imefikia hatua ya mechi za mzunguko wa pili wa hatua ya makundi kabla ya kufikia mzunguko wa mwisho ambao ni wa tatu.

Katika hatua hii timu hujitahidi kupata matokeo mazuri yanayoweza kuwaweka salama kuelekea mechi za mwisho za makundi.

Baadhi ya timu kama Ufaransa tayari zimeshafanikiwa kufuzu hatua ya 16 bora na timu nyingine pia zinaangalia uwezekano wa kufuzu hatua hiyo kwa kushinda mechi zao za pili, pia kuna nyingine zinahitaji kushinda ili kurudisha matumaini. Hapa tumekuletea uchambuzi wa kina juu ya michezo yote itakayochezwa leo. Je? nani ni nani?

MZIGO UPO HIVI

Mchezo ambao utatazamwa sana na mashabiki wa soka barani Afrika ni kati ya Cameroon na Serbia unaotarajiwa kupigwa Al Janoub Stadium, Al Wakrah, saa 7:00 mchana. Kwa sasa timu zote hizi hazina alama hata moja, ikiwamoja itaibuka na ushindi katika mechi hii atakuwa ameweka matumaini ya kwenda hatua inayofuata kwa kuzingatia matokeo ya Brazil na Uswiss, Ikiwa timu moja kati ya hizo itaifunga mwenzake kwenye mechi zao za leo.

Historia inaonyesha timu hizi zimekutana mara moja na hiyo ilikuwa ni mwaka 2010 kwenye mchezo wa kirafiki na Cameroon ikaambulia kichapo cha mabao 4-3.

Mchezo wa kukata na shoka utakuwa wa Kundi H, kati ya Ureno na Uruguay na katika kundi hilo ni Ureno pekee ndiyo yenye alama tatu ikiwa kinara wa kundi wakati Korea Kusini na Uruguay zikiwa na alama moja zikishika nafasi ya pili na tatu na Ghana ikiburuza mkia.

Mchezo huu utawakutanisha mastaa wakubwa, Cristiano Ronaldo na Luis Suarez.

Ureno inahitaji sana kushinda mechi hiyo ili kujihakikisha nafasi ya kusonga mbele kwani ikifungwa itakuwa kwenye hati hati ya kufuzu hatua inayofuata na italazimika kushinda mechi ya mwisho ya kundi dhidi ya Korea Kusini ili kuweka matumaini ya kufuzu hatua inayofuata.

Wababe hawa wamekutana mara tatu na takwimu zinaonyesha kwamba walitoshana nguvu kwani Ureno ameshinda moja, Uruguay moja na mchezo mwingine ulimalizika kwa sare.

Zimekutana mara moja tu kwenye fainali za Kombe la Dunia ambayo ilikuwa mwaka 2018 ambapo Uruguay ilishinda mabao 2-1, mechi yao itapigwa Lusail Iconic Stadium, Lusail saa 4:00 usiku.

Mechi ya mwisho ya Kundi H kwa leo Jumatatu itakuwa ni kati ya Ghana na Korea Kusini ambapo timu zote mbili zinahitaji zaidi matokeo ya ushindi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata.

Kwa ujumla zimekutana mara tisa katika michuano tofauti na Ghana imeshinda mara nne, Korea Kusini imeshinda mara nne na mchezo mmoja ulimalizika kwa sare.

Hawajawahi kukutana kwenye michuano hii ya Kombe la Dunia, Ghana haijapata alama yoyote hadi sasa wakati Korea Kusini ina alama moja iliyopata baada ya kutoka sare dhidi ya Uruguay kwenye mchezo wa kwanza wakati Ghana ikifa mbele ya Ureno.

Mechi hii inatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa ducation City, Al Rayyan, kuanzia saa 10:00 jioni na mwamuzi atakayesimama pale katikati atakuwa ni Anthony Taylor kutoka England.

Kundi G, Brazil inayoonekana kuwa na moto, itakuwa na mchezo muhimu dhidi ya Timu ya Taifa ya Uswiss.

Brazil na Uswiss zote zina alama tatu na Brazil ndiyo inayoongoza kundi huku Uswiss ikishika nafasi yapili na nafasi ya tatu inashikiliwa na Cameroon huku Serbia ikiburuza mkia.

Ikiwa Uswiss itashinda mechi itakuwa imepaa hadi kileleni na mechi kati ya Serbia na Uswiss ikiisha kwa sare wao watakuwa wameshajihakikishia safari ya kwenda hatua ya 16 bora, ambapo itakuwa sawa na Brazil ambao pia ikishinda itakuwa imejihakikishia kufuzu hatua ya 16 bora kwa kuzingatia matokeo ya Cameroon na Serbia.

Katika kukutana timu hizi zimekutana mara tisa na Brazil ndio mbabe ikishinda mara tatu, mechi nne zikiisha kwa sare huku Uswiss ikishinda mara mbili.

Kwenye mashindano haya ya Kombe la Dunia zimekutana mara mbili, ya kwanza ikiwa ile mwaka 1950 katika michuano iliyofanyika nchini Brazil, mchezo huo ulikuwa wa mwisho wa hatua ya makundi na ukaisha kwa sare ya mabao 2-2.

Mara ya mwisho kukutana kwenye mashindano haya ilikuwa ni mwaka 2018 kule Urusi na mechi pia ilimalizika kwa sare ya bao 1-1. Uwanja ambao umetengenezwa kwa makontena, Stadium 974, uliopo Doha ndio utatumika kwa ajili ya mchezo huu ambao utasimamiwa na mwamuzi wa kati kutoka El Salvador Ivan Barton na mechi itaanza saa 1:00 usiku.

Chanzo: Mwanaspoti