Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huku Ninja, kule Mpole mechi ya mtoano Congo

Ninja Mpoleee Huku Ninja, kule Mpole mechi ya mtoano Congo

Sat, 13 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Beki wa Lubumbashi Sport ya DR Congo, Abdallah Shaibu 'Ninja' juzi timu yake imefungwa bao 1-0 na FC Lupopo anayoichezea Mtanzania mwenzake George Mpole.

Katika mchezo huo, Ninja na Mpole wote walianza katika kikosi cha kwanza, wameuzungumzia ushindani ulivyokuwa na ugumu wa ligi ilipofikia.

Ligi ya DR Congo kwa sasa imefikia hatua ya mtoano wa kusaka bingwa wa nchi, ambapo zinachezwa timu nane, kutoka kanda ya Lubumbashi na Kinshasa.

Ukanda wa Lubumbashi kuna TP Mazembe, FC Lupopo, Lubumbashi Sport na Don Bosco, wakati ukanda wa Kinshasa zipo AS Vita, Maniema, AF Congo na Douphine Noir.

Ninja amesema mchezo ulikuwa mgumu na Mpole alicheza kwenye kiwango cha juu, kilichokuwa kinawafanya mabeki wa Lubumbashi Sport kumuangalia kwa jicho la kumzuia asifike golini.

"Tulifungwa bao la penalti katika dakika za mwisho, wakati Mpole ametoka, lakini alifanya kazi kubwa kuipigania timu yake, kwa upande wangu nilicheza dakika 90," amesema Ninja na kuongeza;

"Awali, ligi ilikuwa haionyeshwi, ila kwa sasa inaonyeshwa, imekuwa ngumu hapo kila timu inasaka nafasi ya kucheza michuano ya CAF mwakani."

Ninja alijiunga na timu hiyo, baada ya kuachana na Yanga msimu ulioisha.

Kwa upande wa Mpole amesema; "Mchezo ulikuwa mgumu ila tunashukuru tumepata pointi muhimu, nimefurahi kucheza sehemu moja na Ninja kama Mtanzania mwenzangu, kaonyesha kiwango cha juu.

"Timu ninazoziona zina nafasi za kunyakua taji la nchi ni Lupopo na TP Mazembe," amesema Mpole ambaye wakati anaondoka nchini kwenda kucheza DR Congo alikuwa mfungaji bora wa mabao 17 akiwa na Geita Gold msimu wa 2021/22 akifuatiwa na Fiston Mayele aliyekuwa wa Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti