Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huko ulaya ni kivumbi na jasho

Arsenal Vs Man United Kikosi cha Arsenal

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Watatoboa? Swali hilo kuhusu majariwa ya Manchester United wakati itakaporusha kete yake ya tatu kwenye mchakamchaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa leo Jumanne huko Old Trafford.

Man United imepoteza mechi zote mbili za kwanza ilizocheza kwenye Kundi A, usiku wa leo itakipiga na FC Copenhagen katika mchezo ambao chama hilo la Kocha Erik ten Hag litahitaji ushindi wa kwanza ili kufufua matumaini yake ya kutinga raundi ya mtoano ya michuano hiyo. Kwenye kundi hilo, Man United haina pointi yoyote, wakati wapinzani wake wa leo, Copenhagen wana pointi moja, kufuatia sare waliyopata dhidi ya Galatasaray katika mchezo wa kwanza. Bayern Munich, itakipiga na Galatasaray, ambayo ina pointi nne, yenyewe imekusanya pointi sita, ikishinda mechi zake mbili za kwanza.

Bayern haijawahi kupoteza mchezo wowote wa hatua ya makundi mara 36 ilizocheza hadi sasa, ikishinda 33 na sare tatu, huku Copenhagen haijashinda mechi kwenye hatua ya makundi katika mechi nane zilizopita, sare nne na vichapo vinne. Patachimbika.

Kasheshe hilo la Ligi ya Mabingwa Ulaya litaendelea kwenye Kundi B, ambapo Arsenal baada ya kuchapwa na Lens kwenye mechi iliyopita, usiku wa leo itakuwa ugenini huko Hispania kukipiga na Sevilla, ambayo itahitaji kuandikisha ushindi wake wa kwanza baada ya kupata sare mbili kwenye mechi zilizopita ilipokipiga na Lens na PSV. Arsenal yenyewe imekusanya pointi tatu kwenye mechi mbili, huku Lens ikiwa vinara wa kundi hilo baada ya kuwa na pointi nne. Usiku wa leo, Lens itakuwa nyumbani kucheza na PSV, wakati Arsenal itakuwa ugenini, kujaribu kukwepa hatari ya kushuka hadi nafasi ya tatu au nne katika kundi hilo endapo kama itachapwa. Ni kivumbi na jasho.

Real Madrid itakuwa mzigoni ugenini kukipiga na SC Braga kwenye Kundi C, huku mechi nyingine katika kundi hilo itazikutanisha Union Berlin na Napoli. Braga ina mzuka wa kushinda ugenini, ilipotoka kuichapa Union Berlin, lakini Real Madrid nayo ilishinda ugenini dhidi ya Napoli kwenye mchezo wake, jambo linalofanya mashabiki kusubiri utamu wa kutosha katika mchezo huo utakaopigwa Ureno.

Real Madrid inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi sita, ikifuatiwa na Napoli na SC Braga zenye pointi tatu kila mmoja, wakati Union Berlin ikiwa kibonde wa kundi kwa kutokuwa na pointi yoyote hadi sasa.

Mechi za mwisho za usiku wa leo, Inter Milan itakuwa nyumbani kucheza na FC Salzburg, wakati Benfica itaikaribisha Real Sociedad kwenye Kundi D. Kundi hilo linaonekana kuwa na upinzani, ambapo hadi sasa vinara ni Sociedad wenye pointi nne, ikifuatiwa na Inter yenye pointi nne pia na Salzburg wenye pointi tatu, huku Benfica wakiwa wanyonge kwa kutokuwa na pointi yoyote hadi sasa. Mambo ni moto.

Mchakamchaka huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya utaendelea kesho, Jumatano ambapo kwenye Kundi E, Feyenoord itakuwa nyumbani kucheza na Lazio, huku Celtic itakuwa kwao, Scotland kukipiga na Atletico Madrid. Upizani ni mkali kwenye kundi hilo, Atletico ikiongoza kwa kukusanya pointi nne, sawa na Lazio, huku Feyenoord ikiwa na pointi na Celtic ikiburuza mkia kwa kutokuwa na pointi yoyote.

Utamu utaendelea kwenye Kundi F, ambapo Newcastle United itajitupa St James’ Park kucheza na Borussia Dortmund, wakati kasheshe zito kwenye kunsi hilo litakuwa huko Parc des Princes, ambapo Paris Saint-Germain itakuwa na kazi ya kuikabili AC Milan. Newcastle United inaongoza kundi hilo kwa kukusanya pointi nne katika mechi mbili, ikifuatiwa na PSG yenye pointi tatu, kisha AC Milan yenye pointi mbili na Dortmund ikiwa ya mwisho ikiwa na pointi yake moja. Mambo yatakuwaje usiku wa kesho?

Mabingwa watetezi, Manchester City wao watarusha kete yao wakiwa ugenini kukipiga na Young Boys kwenye Kundi G, wakati mchezo mwingine utakuwa baina ya RB Leipzig na FK Crvena Zvezda huko Ujerumani.

Man City inaongoza kundi kwa kuwa na pointi sita, ikifuatiwa na Leipzig yenye pointi tatu, wakati Young Boys na FK Crvena Zvezda zenyewe zimevuna pointi moja kila moja.

Kwenye Kundi H kutakuwa na mechi za kibabe, ambapo Barcelona itakuwa nyumbani kucheza na Shakhtar Donetsk, huku Royal Antwerp watakuwa na kazi nzito mbele ya FC Porto.

Barca inaongoza kundi hilo baada ya kukusanya pointi sita katika mechi mbili, ikifuatiwa na FC Porto yenye pointi tatu, sawa na Shakhtar Donetsk, huku Royal Antwerp ikiwa haina pointi yoyote ikishuka uwanjani kurusha kete yake ya tatu.

Chanzo: Mwanaspoti