Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huko kwenye La Liga ukizubaa umeachwa!

Madrid Mskl (1).jpeg Huko kwenye La Liga ukizubaa umeachwa!

Sat, 13 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Real Madrid imeweka pengo la pointi nane kwenye msimamo wa La Liga dhidi ya mahasimu wao Barcelona.

Kila timu imeshacheza mechi 30, lakini Los Blancos wapo kileleni na pointi 75, wakati Barca ipo nyuma na pointi 67. Mechi nane zimebaki kwa kila timu, sawa na pointi 24.

Shughuli bado ni pevu.

Barcelona itarusha kete yake kwenye kuifukuzia Real Madrid ugenini kwa Cadiz, huku ikiingia uwanjani kwenye mchezo huo ikiwa na mzuka baada ya kuichapa Paris Saint-Germain katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini, bahati mbaya kwa kikosi hicho cha Xavi ni kwamba kitacheza na Cadiz wakati Real Madrid ikiwa imeshacheza tayari, hivyo itakuwa imeshafamu kama pengo la pointi limeongezeka au kupungua. Patamu hapo.

Real Madrid na yenyewe itakuwa ugenini kukipiga na Real Mallorca, katika mchezo ambao ushindi utawafanya waweke pengo la pointi kufikia 11 na kuipa Barcelona mlima mrefu wa kupanda katika mchakamchaka wa kutetea taji lao la La Liga.

Bila shaka, Barca itakuwa kwenye sala za kuomba dua mbaya dhidi ya Madrid huku wao wakisaka ushindi kwenye mchezo wao na Cadiz ili kupunguza pengo la pointi lifikie tano na kufanya mchakamchaka wa ubingwa kunoga zaidi.

Miamba hiyo mbili kwenye mbio za ubingwa yote itashuka uwanjani leo Jumamosi kila moja ikisaka pointi za kibingwa. Itakuwaje? Pengo la pointi litakuwaje?

Kipute cha La Liga kilianza kwa mchezo mmoja jana Ijumaa, ambapo Real Betis ilikuwa nyumbani kukipiga na Celta Vigo.

Lakini, mechi nyingi zitapigwa leo Jumamosi, ambapo Atletico Madrid yenyewe itakuwa nyumbani Wanda Metropolitano kucheza na wagumu Girona.

Vijana wa Diego Simeone, Atletico Madrid inajaribu kupunguza pengo la pointi katika kuifukuzia Girona kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, jambo linalofanya mechi hiyo kuwa na mvuto mkubwa. Atletico Madrid inahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kuikimbia Athletic Bilbao iliyopo kwenye nafasi ya sita, endapo kama itashinda dhidi ya Villarreal kesho Jumapili na kisha Atletico ikitoka sare au kuchapwa, itashushwa kwenye msimamo. Girona ipo kafasi ya tatu na pointi zao 65, Atletico pointi 58 na Bilbao pointi 56. Girona inaitisha pia Barcelona, kwani endapo kama vijana hao wa Xavi watashindwa kuichapa Cadiz ugenini, kisha Girona ikaichapa Atletico ugenini, basi msimamo wa ligi hiyo utakuwa upo kwenye mabadiliko makubwa.

Mechi nyingine itakayokuwa na mvuto mkubwa ni ile ya Rayo Vallecano itakayokuwa nyumbani kukipiga na Getafe. Rayo inasaka pointi za kuwaweka mbali kwenye hatari ya kushika daraja, wakati Getafe yenyewe inapambana kuhakikisha inakuwa kwenye nafasi za kupata fursa ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.

Jumapili ukiachana na mechi ya Bilbao na Villarreal, vita nyingine itakuwa baina ya Las Palmas itakuwa nyumbani kucheza na Sevilla, wakati Granada itamaliza ubishi na Alaves, huku Real Sociedad itakuwa na mambo matamu ya kuonyeshana na Almeria. Utamu wa wikiendi hii kwenye La Liga ni kila mechi matokeo yake yana kitu kikubwa cha kubadilisha kwenye msimamo wa ligi hiyo. Hivyo, ukizubaa umeachwa kwenye mataa. Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja tu, Osasuna itakapokuwa nyumbani kuikaribisha Valencia katika moja ya mechi zinazotarajiwa kuwa na upinzani mkali uwanjani.

Chanzo: Mwanaspoti