Simba imefanya maamuzi mazito. Tena kimyakimya. Imewarudisha kundini watu wanne muhimu ambao wanajua jinsi ya kufanya umafia kwenye usajili nchini Tanzania. Na ikawapa majukumu ya kusimamia shoo kuanzia sasa kurejesha hadhi ya klabu hiyo.
Baada ya kukaa na kugundua kuwa kinachoikwamisha timu hiyo kwa kipindi cha misimu mitatu ni aina ya usajili ambao ilikuwa inafanya, tayari Simba imeshawarudisha Crecensius Magori, Mulamu Nghambi, Kassim Dewji na Sued Mkwabi kusimamia usajili wa timu hiyo.
Kabla ya sura hizo kupewa rungu,usajili wa Simba ulikuwa ukifanywa na viongozi wachache wa juu ambao hatahivyo ilidaiwa kwamba mtandao wao Afrika ulikuwa mdogo lakini hawakuwa pia na bajeti ya kutosha jambo ambalo liliwafanya kununua wachezaji wenye viwango vya wastani.
Baada ya kupewa kazi hiyo hivikaribuni, mabosi hao wenye roho ngumu kipindi cha usajili na wanaojua kona zote za soka la Bongo,tayari wanadaiwa kumamalizana na kiungo aliyekuwa anatakiwa na Yanga Yusuf Kagoma kutoka Singida Foutain Gate na kama mambo yatakwenda sawa atatangazwa mara tu baada ya dirisha kufunguliwa.
Habari zinasema kwamba Yanga walishamalizana Kagoma ili akawe mshindani wa Khalid Aucho lakini Simba ambao walikuwa na uhitaji pia kwenye nafasi hiyo wakafanya umafia fasta baada ya kubonyezwa kuwa Yanga walikuwa hawajamlipia staa huyo chochote zaidi ya mali kauli.
Timu hiyo ya watu wanne, imeshasema kuwa kama ikipewa fungu linalotakiwa basi kikosi hicho msimu ujao kitakuwa moto wa kuwakia mbali na kitaanza tena kasi ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho FA, pamoja na tageti ya kufika fainali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ni kweli Simba walikaa na kukubaliana kuwarudisha Magori, Mkwabi,Mulamu na KD kusimamia usajili wa dirisha hili huu ulikuwa ushauri wa Mwekezaji Mohammed Dewji, unajua mwanzo wakati timu inawasajili mastaa wakubwa kama kina Luis, Clatous Chama, Bernad Morisson kulikuwaga na kamati ya usajili ambayo inatambulika rasmi na bodi, lakini hapa katikati ikafutwa sasa matatizo ndiyo yakaanzia hapo wachezaji wengi wakaja wa kiwango cha chini sana.
“Tayari wameshaanza kazi na kuna kiungo mmoja na beki wameshawasajili, hawa ni wachezaji wa ndani, lakini wana majina kadhaa mezani kwao ambapo wanasubiri fedha tu kukamilisha na kuna mengine yalikuwa yamependekezwa lakini wameyagomea,” kilisema chanzo.
Magori ambaye siku za hivi karibuni amekuwa akionekana kwenye mechi za Simba na hata mazoezini amewahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, lakini pia alikuwa karibu sana na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba marehemu Zacharia Hans Pope.
Kassim maarufu kwa jina la’KD’kabla ya marehemu Hans Poppe, kupewa nafasi ya kuongoza kamati ya usajili, yeye ndiyo alikuwa anashikilia majukumu hayo ambapo alifanya kazi kubwa na za ndani kabisa ni kwamba vigogo wengi wanampenda kwavile ni mwepesi wa kufanya maamuzi yenye masilahi kwa klabu.
Kwa upande wa Mkwabi ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa kundi maarufu la Friends of Simba alikuwa Mwenyekiti wa Simba kabla ya kung’atuka na kukaa pembeni kwa muda mrefu na sasa amerejea. Ni miongoni mwa viongozi vijana wenye mtandao mkubwa kwenye soka la ndani.
Mbali na Kagoma, lakini inaelezwa kuwa mabosi hao wameshakamilisha usajili wa beki wa Coastal Union, Lameck Lawi ambaye awali alikuwa anatajwa kuwa anaweza kujiunga na Azam.
Mbali na usajili, inaelezwa kuwa wamepewa pia kazi ya kutafuta kocha mpya wa timu hiyo ambaye atatangazwa kabla ya Julai 20, mwezi huu.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Hassan Dalali ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa Simba alishauri kurejeshwa kwa kamati hiyo lakini akataka viongozi hao wawe karibu zaidi na timu kuanzia kambini hadi viwanjani akijinasibu kwenda uwanjani mechi zote za Simba kipindi akiwa madarakani.