Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huko Ruvu shooting nako!

Makata Mbwana Mbwana Makata

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ruvu Shooting inahaha kujiokoa isishuke daraja ikiwa inaburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 14 katika michezo 21, huku mastraika wa timu wakibebeshwa lawama kwa kushindwa kutupia kambani.

Maafande hao wanaonekana kuwa na kibarua kigumu kusalia Ligi Kuu kutokana na kikosi chake kilivyo licha ya kuburuza mkia lakini ndio timu iliyofunga mabao machache zaidi ikifunga 10 tu.

Kinara wa mabao wa kikosi hicho ni Abalkassim Suleman mwenye mabao manne, Rashid Juma aliyefunga matatu kabla ya kuhama kwenda Ihefu, huku Ally Bilaly na Rolland Msonjo kila mmoja akiwa na bao moja.

Wakati safu ya ushambuliaji ikiwa na idadi hiyo ya mabao, safu ya ulinzi nayo imekuwa na tatizo la kuruhusu mabao ambapo katika michezo 21 imeruhusu mabao 24 sawa na bao moja kwa kila mchezo.

Wikiendi hii itakuwa nyumbani kucheza na KMC, kocha wa kikosi hicho Mbwana Makatta alisema wana kibarua kigumu lakini amekiandaa vyema kikosi chake.

"Mapungufu hayo tulishayaona ndio maana tulifanya maboresho wakati wa dirisha dogo la usajili la wachezaji na sahivi kinachofuata ni utekerezaji."

Timu hizo zimekutana mara 11 tangu KMC ilipopanda msimu wa mwaka 2018/19 na katika michezo hiyo, Ruvu imeshinda mara moja pekee kwa bao 1-0 lililofungwa na Santos Mazengo Oktoba 30, 2019.

KMC imeshinda michezo minne na kupata sare sita na katika mchezo uliopita wa duru la kwanza msimu huu zilitoka suluhu.

Kwa misimu sita ya nyuma Ruvu imekuwa ikuruhusu zaidi mabao ya kufungwa kuliko kufunga, kwani msimu uliopita ilifungwa mabao 39 ikafunga 28, msimu wa 2020/21 ilifungwa mabao 38 ikafunga 34, msimu wa 2019/20 ilifungwa mabao 42, msimu wa 2018/19 ilifungwa mabao 43.

Katika mechi zao za nyumbani msimu huu wameshinda mbili tu kati ya 11 na sare mbili, wameambulia pointi nane tu wakati ugenini wamepata pointi sita.

Chanzo: Mwanaspoti