Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huko Jangwani, Mastaa wajazwa noti kuimaliza Simba

DJUMA AUCHO Mastaa wa Yanga

Sat, 15 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Yanga ikiwa kambini ikianza maandalizi ya kuwavaa watani wao Simba, beki Mkongoman Djuma Shaban ametuma salam kwa wekundu hao akisema gari lao la ushindi kwa sasa imekata breki, huku mastaa wa timu nzima wakijazwa noti ili kuongeza mzuka zaidi kabla ya kupigwa kwa derby.

Djuma aliyeanza kurudi katika kiwango chake ameliambia Mwanaspoti Yanga bado haijajihakikishia ubingwa na ili malengo yatimiea wanatakiwa kushinda mechi mbili zijazo kuanzia Kariakoo Derby itakayopigwa Jumapili kisha ile ya Singida Big Stars.

Beki huyo wa kulia alisema wanatambua kwamba mchezo utakuwa mgumu kwa vile Simba nao hawatakubali kupoteza kirahisi, ila moto wa ushindi walionao ndio utaamua matokeo siku hiyo.

Alisema ushindi wa mchezo huo pia utawapa nguvu kabla ya kuanza safari ya kucheza ugenini dhidi ya Rivers United ya Nigeria kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

"Timu yetu kwa sasa iko na ubora mkubwa tumekuwa na muendelezo mzuri wa kushinda licha ya mabadiliko ya kikosi chetu, unapopata nafasi lazima ufanye vizuri kwa kuwa kuna wengine nao wanaweza kufanya vizuri siku wakicheza," alisema Djuma na kuongeza;

"Hatujashinda ubingwa bado na ili tuchukue taji tunatakiwa kushinda mechi mbili na kuanzia hii ya Simba, hautakuwa mchezo rahisi hii ni mechi ngumu, lakini Yanga tutashinda mashabiki wetu waje.

Wakati Djuma akiyasema hayo matajiri wao wakafanya akili moja wakilipa posho za ushindi katika mechi tatu za kimataifa zilizopita.

Taarifa kutoka ndani ya kikosi hicho ni kwamba morali ya mastaa wa timu hiyo imezidi kuongezeka baada ya mabosi wa klabu hiyo kulipa zaidi ya sh 300 milioni ambazo ni posho za ushindi katika mechi za kimatraifa za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuivusha timu kuingia robo fainali.

Malipo hayo yanaifanya Yanga kubaki na posho ya malipo ya awamu moja tu wa mchezo wa Ligi Kuu wa mwisho uliopigwa dhidi ya Kagera Sugar na kushinda mabao 5-0.

"Kila kitu kimeshamalizwa na viongozi tumepata malipo ya posho zetu hii inatufanya sasa akili zetu kuwa tayari kwa maandalizi ya mchezo huu ujao," alisema mmoja wa mastaa wa timu hiyo anayecheza nafasi ya kiungo.

Tayari Yanga iko kambini ikiendelea na maandalizi ya mchezo huo ambapo kikosi hicho kilianzia gym kwa ratiba ya siku moja Jumatano huku kuanzia jana Alhamisi wakirudi uwanjani kwa ratiba nyingine.

Vinara hao wa Ligi Kuu Bara ndio watetezi wa taji na wikiendi hii watakuwa wageni wa Simba katika mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na matokeo ya ushindi yatawasogeza kwenye hatrua ya kubeba taaji kwa msimu wa pili mfululizo.

Chanzo: Mwanaspoti